Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

3. Tayarisha na Uhifadhi Chakula Vizuri

3. Tayarisha na Uhifadhi Chakula Vizuri

3. Tayarisha na Uhifadhi Chakula Vizuri

M PISHI mmoja katika Israeli la kale ambaye hakuwa mwangalifu alikusanya maboga ya mwituni ambayo ‘hakuwa anayafahamu.’ Aliyatia ndani ya mchuzi. Walaji, waliohofia kwamba chakula hicho kilikuwa na sumu walilia na kusema: “Kuna kifo ndani ya chungu hiki.”—2 Wafalme 4:38-41.

Kama mfano uliotajwa unavyoonyesha, tunapaswa kuwa waangalifu kuhusu chakula ambacho hakikutayarishwa vizuri kwa kuwa kinaweza kutudhuru au hata kutuua. Kwa hiyo, ili kuzuia magonjwa yanayosababishwa na vyakula, jifunze kutayarisha na kuhifadhi chakula kwa uangalifu. Fikiria mapendekezo manne yafuatayo:

Nyama iliyoganda isiyeyushwe nje ya friji.

Wizara ya Kilimo ya Marekani inasema kwamba “hata ingawa sehemu ya katikati ya nyama huwa bado imeganda inapoyeyuka nje ya friji, huenda sehemu ya nje ya nyama hiyo ikawa na joto la kati ya nyuzi 4 Selsiasi na nyuzi 60 Selsiasi, kiwango kinachosemwa kuwa hatari kwa sababu bakteria huongezeka haraka.” Badala yake, yeyusha chakula ndani ya friji, kwenye mikrowevu, au kitumbukize ndani ya maji baridi kikiwa kimepakiwa.

Pika chakula hadi kiive kabisa.

Shirika la Afya Ulimwenguni linasema kwamba “karibu viini vyote hatari hufa chakula kinapopikwa na kuiva kabisa.” Unapopika chakula hakikisha kwamba kinaiva kabisa, hasa ikiwa kina supu au mchuzi. * Kwa kuwa inaweza kuwa vigumu kujua halijoto ya vyakula fulani, wapishi wengi hutumia kifaa cha kupima joto la nyama. Au mtu anaweza kudunga nyama kwa kutumia uma au kuikata katikati ili kuhakikisha kwamba imeiva kabisa.

Chakula kiliwe punde tu baada ya kupikwa.

Chakula kilichopikwa hakipaswi kuachwa nje kwa muda mrefu, kwa hiyo hakikisha kinaliwa punde tu baada ya kupikwa ili kisiharibike. Chakula baridi kinapaswa kuliwa kikiwa baridi na chakula moto kinapaswa kuliwa kikiwa moto. Ili chakula chako kisipoe, kiweke ndani ya joko lenye halijoto ya nyuzi 93 Selsiasi. Ikiwa huna joko, unaweza kuacha chakula juu ya jiko lisilo na moto mwingi.

Chakula kinachosalia kishughulikiwe vizuri.

Anita, mama anayeishi huko Poland, hupakua chakula mara tu baada ya kukipika. Lakini ikiwa kuna chakula kilichobaki, “mimi hukipakia katika vifurushi vidogo-vidogo na kukigandisha ili iwe rahisi kukiyeyusha baadaye.” Ikiwa unahifadhi masalio ya chakula kwenye friji, lazima kiliwe kabla ya siku tatu au nne kwisha.

Unapoenda kwenye mkahawa unalazimika kula chakula kilichotayarishwa na mtu mwingine. Kwa hiyo, unawezaje kuilinda familia yako mnapokula kwenye mkahawa?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Nyama za aina fulani zinahitaji kupikwa kwa muda mrefu zaidi.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

WAZOEZE WATOTO WAKO: “Watoto wangu wanapopika chakula mimi huwakumbusha wasome na kufuata maagizo yaliyoonyeshwa.”—Yuk Ling, Hong Kong