Batiki—Kitambaa Maridadi cha Indonesia
Batiki—Kitambaa Maridadi cha Indonesia
KITAMBAA cha batiki kimekuwepo kwa muda mrefu, na bado hakijapitwa na wakati. Wafalme huvaa batiki wakati wa karamu zao za kifahari, na pia wachuuzi sokoni huvalia batiki. Batiki ni kitambaa maridadi, chenye rangi za kuvutia, na kina unamna-namna wa michoro. Hata hivyo, batiki ni nini? Kinatengenezwaje? Kilitoka wapi? Na kinatumiwaje leo?
Batiki ni kitambaa kilichoanza kutumiwa zamani. Michoro ya batiki hutokezwa kwa kutumia mbinu ya pekee ya kuzuia rangi isishike sehemu fulani-fulani za kitambaa na sanaa hiyo imekuwa sehemu ya maisha na utamaduni wa watu nchini Indonesia. Vitambaa vya aina hiyo ni maarufu duniani kote.
Kutumia Rangi na Nta
Msanii hutumia kifaa kidogo cha shaba kilichojazwa nta iliyoyeyushwa ili kuchora kwa mkono michoro mbalimbali ya pekee kwenye kitambaa. Baada ya nta hiyo kukauka, kitambaa hicho hutiwa ndani ya rangi. Sehemu zilizopakwa nta huhifadhi rangi yake ya asili, kwa kuwa hazishiki rangi. Ili kutokeza unamna-namna wa mitindo, mbinu hiyo hurudiwa tena na tena kwa kutumia rangi tofauti-tofauti.
Katikati ya karne ya 19, wasanii wa Batiki walitumia stempu za shaba kutia nta. Njia hiyo ilikuwa ya haraka kuliko kutumia kifaa cha shaba na ingeweza kutumiwa kutengeneza vitambaa vinavyofanana. Katika karne ya 20, viwanda vilianza kutumia wavu fulani uliotengenezwa kwa hariri unaowekwa kwenye mashine ili kutokeza picha kwenye kitambaa. Lakini bado unaweza kununua kitambaa cha batiki kilichotengenezwa kwa mikono. Hata hivyo, vitambaa vya batiki vinavyotengenezwa viwandani ndivyo vinavyopatikana kwa wingi.
Kwa kawaida, vitambaa vya pamba na hariri hutumiwa kutengeneza batiki. Rangi zinazotumiwa hutengenezwa kutokana na majani, mbao, maganda ya mti, na vikolezo, ingawa rangi zinazotengenezwa viwandani hutumiwa pia. Kabla ya nta kuanza kutumiwa, majani yaliyopondwa, mafuta ya wanyama, na hata matope yalitumiwa kutokeza michoro. Siku hizi nta inayotumiwa hutengenezwa viwandani. Hata hivyo, bado watu wanatumia mchanganyiko wa mafuta ya taa na nta ya nyuki.
Vilianza Kutokezwa Zamani na Vitaendelea Kutokezwa
Hakuna mtu anayejua ni lini na ni wapi hasa kitambaa cha kwanza cha batiki kilipotengenezwa. Nchini China, vipande fulani vya vitambaa vya batiki vimepatikana vinavyokadiriwa kuwa ni vya kabla ya karne ya sita W.K. Bado haijajulikana wazi ni lini mbinu ya kutengeneza batiki ilianza kutumiwa nchini Indonesia, lakini kufikia karne ya 17 inaonekana kwamba wafanyabiashara walileta vitambaa vya batiki nchini Indonesia na wengine walivinunua kutoka nchini humo.
Katika miaka ya hivi karibuni, vazi la batiki limekuwa maarufu zaidi na limekuja kuwa vazi linalotambulisha taifa la Indonesia. Mnamo 2009, ili kutambua historia ndefu ya batiki nchini Indonesia na jinsi ambavyo limeathiri utamaduni wa nchi hiyo, shirika la UNESCO liliorodhesha sanaa ya batiki kuwa sehemu ya “Utamaduni wa Kiasili Uliorithiwa” wa nchi hiyo.
Mavazi ya Batiki
Kuna njia za kitamaduni za kuvaa, kukunja, na kutengeneza batiki ambazo zinatokana na mila na ushirikina wa watu wa Indonesia. Mikoa mingi ya Indonesia ina aina zao za rangi za batiki na michoro. Kwa mfano, batiki kutoka pwani ya kaskazini ya Java, huwa na rangi nyangavu na mara nyingi zinakuwa na michoro ya maua, ndege, na wanyama wengine. Hata hivyo, batiki inayotoka Java ya kati kwa kawaida huwa na rangi chache ambazo zinakaribia kufanana, na mara nyingi
zinachorwa maumbo ya kijiometriki. Kuna aina 3,000 hivi za mchoro ya batiki zilizorekodiwa.Vazi la kitamaduni la batiki ni selendang, ambalo hutumiwa kama mtandio au nguo ya kubebea vitu ambayo wanawake huvaa au kujitanda mabegani. Mara nyingi, wanawake huitumia kama mbeleko ya kubebea watoto au bidhaa za sokoni. Hata hivyo, kunapokuwa na jua kali mtandio huo hutumiwa kufunika kichwa.
Wanaume hutumia kitambaa fulani cha kitamaduni kufunika kichwa kinachoitwa iket kepala. Kitambaa hicho cha batiki chenye umbo la mraba hufungwa kichwani na kufanyiza kilemba. Mara nyingi, kilemba hicho huonwa kuwa vazi rasmi la sherehe.
Kitambaa kingine cha batiki chenye umbo la mstatili kinachopendwa sana na ambacho hufungwa kuzunguka mwili kinaitwa sarong. Wakati mwingine pindo mbili za mwisho huunganishwa. Sarong ya kawaida hufunika miguu, kisha mkunjo hufanyizwa kiunoni, na hivyo huwa kama sketi kubwa. Sarong huvaliwa na wanaume na wanawake.
Vitambaa vya batiki hutumiwa kutengeza aina nyingi sana za nguo, iwe ni suruali za kawaida tu au hata magauni ya hali ya juu. Lakini vitambaa hivyo hutumika kuchorea picha, mapambo ya kuning’inizwa, vitambaa vya meza, mashuka ya kupamba vitanda, na kadhalika. Watalii wanapotembelea soko la vitambaa vya batiki nchini Indonesia wanaweza kupata aina tofauti-tofauti za mifuko, sapatu, chengeu, na hata mfuko wa kufunika kompyuta zinazoweza kubebwa. Kwa kweli, kina matumizi mengi yasiyoweza kuhesabika—kitambaa maridadi sana!
[Picha katika ukurasa wa 23]
Kifaa kidogo cha shaba kilichojazwa nta iliyoyeyushwa hutumiwa kuchora michoro maridadi kwenye kitambaa
[Picha katika ukurasa wa 23]
Kitambaa chenye michoro yenye nta hutiwa ndani ya rangi mara kadhaa
[Picha katika ukurasa wa 23]
Mavazi ya Batiki
1. Selendang
2. Iket kepala
3. Sarong