Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Hakikisha Chakula Hakikudhuru

Hakikisha Chakula Hakikudhuru

Hakikisha Chakula Hakikudhuru

“Shule Nchini Ujerumani Yafungwa kwa Sababu ya Bakteria ya E. Coli.”—SHIRIKA LA HABARI LA REUTERS, UJERUMANI.

“Miche Yashukiwa Kueneza Bakteria ya Salmonela Katika Majimbo Matano.”—USA TODAY.

“Nyama ya Ng’ombe 6 Waliolishwa Nyasi Yenye Sumu ya Nyuklia Yauzwa Katika Wilaya 9.”—THE MAINICHI DAILY NEWS, JAPANI.

HIVYO vilikuwa vichwa vikuu vya habari katika kipindi cha majuma mawili mwaka jana. Watafiti wanakadiria kwamba kila mwaka karibu asilimia 30 ya watu katika nchi zinazoendelea hupatwa na magonjwa yanayosababishwa na vyakula.

Wewe unaathiriwaje na habari hizo? Baba mmoja nchini Hong Kong anayeitwa Hoi anasema hivi: “Mambo hayo hunitia wasiwasi na kunikasirisha. Nina watoto wawili, nami huwa na wasiwasi chakula wanachokula kimetayarishwa wapi na jinsi gani.”

Katika nchi maskini, kila mwaka mamilioni ya watu, hasa watoto, hufa kutokana na magonjwa yanayosababishwa na vyakula na maji machafu. “Katika masoko ya huku, vyakula huachwa wazi na hivyo kuchafuliwa na nzi, mvua, upepo, na vumbi,” anasema Bola, anayeishi nchini Nigeria. “Ninaposoma au kusikia kuhusu magonjwa yanayosababishwa na vyakula mimi huogopa. Ninataka kuilinda familia yangu.”

Je, inawezekana kuilinda familia yako kutokana na chakula kinachoweza kutokeza madhara? Shirika la Kukagua Chakula la Kanada linasema hivi: “Chakula hatari kinapouzwa madukani, jambo hilo linatangazwa kotekote na vyombo vya habari. Na hilo linafaa. Lakini chakula kinaweza kusababisha magonjwa ikitegemea jinsi tunavyokitayarisha tunapokuwa nyumbani.”

Unaweza kufanya nini ili kuilinda familia yako kutokana na magonjwa yanayosababishwa na vyakula? Tutazungumzia njia nne za kuzuia chakula chako kisikudhuru.

[Sanduku katika ukurasa wa 3]

NI NANI WALIO HATARINI?

Watu wafuatao wanaweza kupatwa kwa urahisi na magonjwa yanayosababishwa na vyakula:

● Watoto walio chini ya umri wa miaka mitano

● Wanawake waja-wazito

● Watu walio na umri wa zaidi ya miaka 70

● Watu walio na mfumo dhaifu wa kinga

Ikiwa wewe au yeyote anayekula pamoja nawe yuko katika kikundi hiki, unapaswa kuwa mwangalifu sana kuhusu chakula unachotayarisha, kupakua, na kula.

[Hisani]

Chanzo: Shirika la Usimamizi wa Chakula la New South Wales, Australia