Kombe la Ulaya la 2012—Tukio la Kihistoria
Kombe la Ulaya la 2012—Tukio la Kihistoria
JE, WEWE hufurahia kutazama mechi yenye kusisimua ya kandanda—au hata labda kucheza? Ikiwa ndivyo, basi huenda unatambua kwamba kutakuwa na Kombe la Ulaya la 2012 la UEFA (Muungano wa Mashirikisho ya Soka Barani Ulaya) linalotazamiwa kuanza Juni 8, huko Warsaw, Poland, na mechi ya mwisho ikichezwa Julai 1, huko Kiev, Ukrainia. Hilo ni kombe gani, na ni matayarisho gani ambayo yamefanywa? Ni nini kinacholifanya liwe tukio la kihistoria?
“Kuandika Historia Pamoja”
Tangu mwaka wa 1960, kombe hilo la mpira limekuwa likiandaliwa barani Ulaya kila baada ya miaka minne. Nchi tofauti ambazo zimewahi kuandaa kombe hilo ni Austria, Hispania, Italia, Sweden, Ubelgiji, Ufaransa, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Ureno, Uswisi, na Yugoslavia.
Mwaka huu, nchi ya Poland na Ukrainia zitashirikiana kuandaa kombe hilo. Huko Poland, mechi hizo zitachezwa katika majiji ya Gdańsk, Poznan, Warsaw, na Wroclaw. Nchini Ukrainia, mechi zitachezwa huko Donetsk, Kharkiv, Kiev, na L’viv.
Kulingana na shirika la UEFA, hiyo “itakuwa mara ya tatu kwa nchi mbili kushirikiana kuandaa kombe hilo (liliandaliwa huko Ubelgiji na Uholanzi mwaka wa 2000 [kisha] Austria na Uswisi mwaka wa 2008).” Hata hivyo, kombe la mwaka wa 2012 ni la kihistoria. Kwa njia gani?
Mbali tu na kuwa ushirikiano kati ya nchi mbili, kombe la mwaka huu ndilo la kwanza kuandaliwa na nchi zilizo katika Ulaya ya Kati na ya Mashariki. Kwa hiyo, maneno yaliyochaguliwa kusimamia kombe la mwaka huu ni “Kuandika Historia Pamoja.”Matayarisho
Bila shaka, jambo moja muhimu linalohusika katika kuandaa mechi yoyote ni kupata uwanja unaofaa wa kuchezea. Kwa sababu hiyo, majiji ya Poznan na Kharkiv yamerekebisha viwanja vyao, huku viwanja katika majiji yale mengine sita ni vipya kabisa. Inakadiriwa kwamba mashabiki 358,000 wanaweza kutoshea ndani ya viwanja hivyo.
Kwa kuwa inatazamiwa kuwa kutakuwa na mashabiki wengi kadiri hiyo, majiji yanayoandaa mechi hizo yamejitahidi sana kuzingatia usalama. Maelfu ya walinzi wamekuwa wakizoezwa kwa ajili ya kombe hilo. Kulingana na jarida Science & Scholarship in Poland, mazoezi yao yanahusisha “kuzoezwa mbinu za usalama katika nyanja 140 tofauti zinazohusisha . . . kudhibiti umati, kutokeza maeneo salama ambayo watu wanaweza kukimbilia kunapokuwa na dharura, na kushirikiana na vikundi vya usalama vya kigeni.”
Kwa nini matayarisho kama hayo ni ya lazima? Sababu moja ni kwamba wenye mamlaka wanatambua magaidi wanaweza kushambulia wakati ambapo kuna michezo mikubwa. Pia wanajua kwamba mashabiki wenye fujo wanaweza kuhatarisha uhai wao na wa wengine, kama visa ambavyo tayari vimetendeka vimeonyesha.
Maoni Yenye Usawaziko
Kwa kusikitisha, mashabiki wengine hupendezwa kupita kiasi na michezo. Shabiki mmoja anasema hivi: “Furaha yangu maishani hupungua na hakuna jambo linaloniridhisha ikiwa timu yangu [ya mpira] haifanyi vizuri. Ninaamini kwamba kama kungekuwa na uwezekano wa kutokea kwa vita vya kinyuklia, hangaiko langu kuu lingekuwa ikiwa mechi za mwisho-juma zitaathiriwa.”
Tofauti na hilo, hebu fikiria maoni yenye usawaziko kuhusu burudani yanayopatikana katika kitabu cha kale kilicho na maneno ya hekima—Biblia. Inatambua umuhimu wa kuwa na pindi za kujifurahisha maishani, ikisema kwamba kuna “wakati wa kucheka . . . na wakati wa kurukaruka.” (Mhubiri 3:1-4) Pia Biblia inatutia moyo tuwe na kiasi. (1 Timotheo 3:2, 11) Hivyo, tunapoamua ni nini tutakachotanguliza maishani, ni jambo la hekima kufikiria shauri la Biblia kwamba “tutambue tofauti kati ya mambo ya maana na yale ambayo si ya maana,” kisha “tuchague mambo ya maana.”—Wafilipi 1:10, Easy-to-Read Version.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]
HAKUNA KUTUMIA TUMBAKU KATIKA KOMBE LA ULAYA LA 2012
Oktoba 20, 2011, shirika la UEFA lilitangaza kwamba “litaweka sheria inayopiga marufuku utumiaji, uuzaji, na utangazaji wa tumbaku katika viwanja vyote vinavyohusika na Kombe la Ulaya la 2012 la UEFA.” Kwa nini marufuku hiyo imewekwa? “Tunapiga marufuku utumiaji wa tumbaku wakati wa Kombe la Ulaya la 2012 kwa sababu tunaheshimu afya ya mashabiki na ya wote wanaohusika katika kombe hilo,” akasema Michel Platini, rais wa shirika la UEFA. Miongoni mwa watu wanaounga mkono marufuku hiyo ni Kamishna wa Ulaya Androulla Vassiliou, ambaye aliyasihi majiji yanayoandaa michezo hiyo yafanye maeneo mengine pia kuwa maeneo ambayo watu hawavuti sigara, kama vile ndani ya hoteli na katika usafiri wa umma. “Kandanda na michezo inahusiana na afya na utendaji” anasema “na tumbaku inadhuru afya na kuzuia watu wasiwe watendaji: mambo haya mawili hayapatani kamwe.”
[Ramani katika ukurasa wa 24]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
POLAND
WARSAW
Gdańsk
Poznan
Wroclaw
UKRAINIA
KIEV
L’viv
Kharkiv
Donetsk
[Picha katika ukurasa wa 24]
Mechi ya mwisho ya Kombe la Ulaya la 2008 kati ya Ujerumani na Hispania, iliyochezwa katika Uwanja wa Ernst Happel huko Vienna, Austria
[Picha katika ukurasa wa 25]
Uwanja wa Olympic huko Kiev, Ukrainia
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]
Pages 24 and 25, both photos: Getty Images