Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Idadi ya watu duniani ilipita bilioni 7 mwishoni mwa mwaka wa 2011, “idadi hiyo ilikuwa bilioni 6 katika mwaka wa 1999.”—CHUO CHA AFYA YA UMMA CHA HARVARD, MAREKANI.
“Kwa ujumla, asilimia 58.8 ya watu huko [Uingereza] wanasema kwamba walihisi kuwa familia yao ingefaidika ikiwa wangetenga wakati wa kutotumia teknolojia ambapo wangezima vifaa vyote vya mawasiliano. . . . Mmoja kati ya watu watatu amefadhaika kiasi cha kwamba angependa kuishi bila vifaa vya mawasiliano.”—CHUO KIKUU CHA CAMBRIDGE, UINGEREZA.
“Tangu mwaka wa 1976, kongamano la maaskofu wa Wakatoliki wa Marekani wametoa taarifa . . . kabla ya kila mwaka ambapo kunakuwa na uchaguzi wa rais ili kuwasaidia Wakatoliki wachague mwanasiasa aliye na imani kama yao.”—CHUO KIKUU CHA FORDHAM, MAREKANI.
“Ikiwa wahalifu wangetaka, wangeweza kutokeza fujo mitaani. . . . Kiwango cha maadili kimeshuka sana kati ya vijana Waingereza, nacho kikundi hicho ni kikubwa kiasi cha kwamba wanaweza kusumbua na kuaibisha nchi nzima.”—THE ECONOMIST, UINGEREZA.
Kuna Jamii Ngapi za Viumbe Duniani?
Wanasayansi ambao utafiti wao uliandikwa katika jarida la PLoS Biology wanasema hivi: “Bado hatujui kuna jamii ngapi za viumbe duniani, na hilo linaonyesha tuna ujuzi mdogo sana kuhusu uhai ulio katika Dunia.” Ingawa wanasayansi hao wanakadiria kwamba kuna jamii kati ya milioni 7.5 na milioni 10 duniani, wataalamu wengine wanasema kwamba kuna jamii kati ya milioni 3 na milioni 100. Kufikia sasa ni jamii milioni 1.2 pekee ambazo zimeainishwa, na inaaminiwa kwamba kulingana na jinsi kazi hiyo inavyofanywa kwa sasa, inaweza kuchukua zaidi ya miaka 1,000 kuainisha jamii zilizosalia. “Kwa kuwa kazi hiyo ya kuainisha jamii za viumbe inafanywa polepole sana, huenda viumbe fulani wakatoweka hata kabla ya tujue kwamba waliwahi kuishi,” wanasema watafiti hao.
Setilaiti Zinasaidia Kuchimbua Vitu vya Kale
Wachimbuaji wa vitu vya kale wanatumia mbinu mpya ya kutafuta maeneo yanayowavutia. Wanatumia programu za kompyuta zinazowasaidia kutambua picha za magofu ya kale yaliyo chini ya ardhi, zilizopigwa kutoka kwenye setilaiti kwa kutumia kamera zenye uwezo mkubwa na miale ya infrared. Kwa mfano, inaripotiwa kwamba picha zilizopigwa kilomita 700 juu ya Misri, zimefichua maeneo 17 yaliyokuwa na piramidi ambazo hazikuwa zinajulikana, makaburi 1,000 ya kale, na vijiji 3,000 hivi vilivyotoweka. Kwa sababu miale ya infrared inaweza kupenya na kupiga picha chini ya ardhi, teknolojia hiyo inasaidia kufichua vitu vilivyozikwa zamani na kusahauliwa, ambavyo mtu hawezi kuviona akiwa juu ya ardhi.