Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Ni Nini Lazima Kibadilike?

Ni Nini Lazima Kibadilike?

Ni Nini Lazima Kibadilike?

“Serikali si suluhisho la matatizo yetu; serikali ndiyo tatizo.” —Ronald W. Reagan, katika hotuba yake ya kuapishwa kuwa rais wa 40 wa Marekani.

ZAIDI ya miaka 30 imepita tangu Ronald Reagan atamke maneno hayo. Wakati huo, Marekani ilikuwa ikipambana na tatizo kubwa sana—“pigo kubwa sana la kiuchumi,” kama Reagan alivyoliita. Alieleza hivi: “Katika historia ya nchi yetu, gharama hazijawahi kuongezeka na kuendelea kuwa za juu kwa muda mrefu kama ilivyo wakati huu, . . . Kwa miaka mingi tumejikusanyia deni kubwa sana na tumefanya maamuzi ya kiuchumi ambayo yametufaidi kwa sasa lakini yatahatarisha wakati wetu ujao na ule wa watoto wetu. Tukiendelea kufanya hivyo, bila shaka tutapatwa na matatizo makubwa ya kijamii, kitamaduni, kisiasa, na kiuchumi.”

Ingawa huenda ikaonekana kwamba Reagan alikuwa amekata tamaa, bado alikuwa na matumaini. Alisema hivi: “Matatizo ya kiuchumi yanayotukumba leo ni matokeo ya mambo ambayo yametukia kwa makumi ya miaka. Hayatakwisha baada ya siku, majuma, au miezi kadhaa, lakini bila shaka yatakwisha.”—Italiki ni zetu.

Hali ikoje leo? Ripoti ya 2009 iliyotolewa na Wizara ya Makao na Ustawi wa Majiji ya Marekani ilisema hivi: “Watu wengi wanashindwa kuboresha maisha yao . . . kwa sababu ya kutumiwa kupita kiasi kwa miundo-misingi kama vile barabara na huduma za maji na umeme, ukosefu wa makao, na kuwepo kwa mifumo ya afya iliyopitwa na wakati. Mradi wa Umoja wa Mataifa unaoshughulikia makao (UN-HABITAT) unakadiria kwamba katika kipindi cha miaka 30 ijayo, mtu mmoja kati ya watatu ataishi bila tumaini la kuboresha hali yake kwa sababu ya kukosa mfumo bora wa kuondoa maji machafu na takataka, maji safi, akikabiliwa na madhara ya kubadilika kwa hali ya hewa, na hilo litachochea kuenea kwa magonjwa na hata tauni.”

Hangaiko la Ulimwenguni Pote

Iwe unaishi wapi, fikiria maswali yafuatayo:

● Je, unahisi kuwa hali yako ya kiuchumi ni salama zaidi kuliko ilivyokuwa miaka 10 iliyopita?

● Je, unaona kwamba wewe na familia yako mnapata huduma za afya za kutosha?

● Je, mazingira ni safi zaidi na yanazidi kuwa bora?

● Unapofikiria kuhusu wakati ujao, je, unaona mambo yatakuwa bora zaidi katika miaka 10, 20, au 30 ijayo?

Mkataba na Jamii

Serikali nyingi zimefanya kile kinachoitwa mkataba na jamii, yaani, makubaliano ya kuandikwa au ya kuwaziwa kati ya watawala na raia ambayo yanaeleza waziwazi haki na wajibu wa pande zote mbili. Kwa mfano, raia wanatarajiwa watii sheria za nchi, walipe kodi, na wasaidie kufanya mazingira yawe salama. Kwa upande mwingine, watawala huahidi kuhakikisha kwamba kuna huduma zinazofaa za afya, usawa, na usalama wa kiuchumi.

Je, serikali zimehakikisha kuna mambo hayo matatu? Chunguza uthibitisho uliopo katika kurasa tatu zinazofuata.

Huduma Zinazofaa za Afya

Mambo ambayo watu wangependa kuona: Matibabu wanayoweza kugharimia na yanayofaa.

Ukweli wa mambo:

● Ripoti iliyotolewa na Benki ya Dunia kuhusu mifumo ya kuondoa maji machafu na takataka na kudumisha usafi ilisema kwamba “kila siku watoto 6,000 hufa kutokana na magonjwa yanayohusianishwa na ukosefu wa mfumo wa kuondoa maji machafu na takataka, ukosefu wa usafi, na ukosefu wa maji safi ya kunywa. Ugonjwa wa kuharisha peke yake huua mtoto moja kila sekunde 20.”

● Uchunguzi mkubwa uliofanywa katika mwaka wa 2008 na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kuhusu jinsi ambavyo huduma za afya hutolewa katika “nchi tajiri na nchi maskini” ulionyesha kwamba “kuna ukosefu mkubwa sana wa usawa” na “huduma hizo hazitimizi mahitaji ya watu, hazitolewi kwa usawa, ni ghali sana, na hazitolewi kwa wakati unaofaa.”

Miaka miwili baadaye, uchunguzi wa WHO ulionyesha kwamba “serikali ulimwenguni pote zinashindwa kugharimia huduma za afya. Kadiri watu wanavyozidi kuzeeka, kadiri watu wengi zaidi wanavyopatwa na magonjwa ya kudumu, na kadiri mbinu mpya za matibabu na zilizo ghali zinavyozidi kugunduliwa, ndivyo na gharama za matibabu zinavyozidi kupanda.”

● Tatizo lingine hatari limetokea katika utoaji wa huduma za afya: Dawa zilizoonwa kuwa zinafanya kazi kimuujiza huenda zisifanye kazi kama ilivyotarajiwa. Magonjwa ya kuambukiza yaliyokuwa yakiwaua mamilioni ya watu miaka mingi iliyopita kama vile, ukoma na kifua kikuu, yalidhibitiwa kwa dawa za kuua viini. Dawa ya kwanza ya aina hiyo iligunduliwa katika miaka ya 1940. Lakini sasa, kulingana na ripoti ya WHO inayoitwa World Health Day 2011, “kumetokea viini na virusi sugu ambavyo haviwezi kutibiwa kwa dawa hizo, na vinaenea haraka. Dawa nyingi muhimu zinashindwa kufanya kazi. Kuna upungufu mkubwa wa dawa zinazoweza kupambana na viini hivyo sugu.”

Ni nini lazima kibadilike: Tunahitaji kuona utimizo wa unabii wa Biblia unaotabiri kwamba kuna wakati ambapo “hakuna mkaaji atakayesema: ‘Mimi ni mgonjwa.’”—Isaya 33:24.

Haki na Usawa

Mambo ambayo watu wangependa kuona: Kukomeshwa kwa ubaguzi dhidi ya jamii zenye watu wachache na kutendewa vibaya kwa wanawake; usawa kati ya matajiri na maskini.

Ukweli wa mambo:

● Ripoti ya shirika moja la kutetea haki za raia huko Marekani (Leadership Conference on Civil Rights Education Fund) ilisema hivi: “Matendo ya jeuri dhidi ya watu mmojammoja, nyumba za ibada, na taasisi za kijamii kwa sababu ya ubaguzi wa rangi, dini, mapendezi ya mtu kuelekea ngono, au taifa la mtu bado yanaongezeka na yanaendelea kuwa tatizo kubwa nchini Marekani.”

● “Mamilioni ya wanawake ulimwenguni pote bado wanaendelea kutendewa isivyo haki, wanatendewa kwa jeuri na ukosefu wa usawa nyumbani, kazini, na katika shughuli za kawaida,” inasema ripoti moja ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari inayotegemea ripoti inayoitwa Progress of the World’s Women: In Pursuit of Justice. Kwa mfano, nchini Afghanistan, asilimia 85 hivi ya wanawake hawapati msaada wowote wa kitiba wanapojifungua. Huko Yemen, hakuna sheria zozote dhidi ya jeuri nyumbani. Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kwa wastani, zaidi ya wanawake elfu moja hulalwa kinguvu kila siku.

● Mnamo Oktoba 2011, Katibu Mkuu wa U.M. Ban Ki-moon alisema hivi: “Ulimwengu wetu una hali zinazopingana kabisa. Kuna chakula kingi lakini watu bilioni moja hukosa chakula. Watu wachache wanaishi maisha ya starehe, huku wengi wakiishi katika umaskini. Maendeleo makubwa ya kitiba yamefanywa, lakini kila siku akina mama wanakufa wakijifungua . . . Mabilioni ya pesa hutumiwa kununua silaha zinazowaua watu badala ya kuwalinda.”

Ni nini lazima kibadilike: Tunahitaji kuona haki ikitekelezwa kwa ajili ya jamii zenye watu wachache na kwa ajili ya wanawake na watu ‘wanaowanyang’anya haki wale wanaoteseka’ wanapaswa kuondolewa.—Isaya 10:1, 2.

Usalama wa Kiuchumi

Mambo ambayo watu wangependa kuona: Kila mtu akiwa na kazi; usalama wa kifedha.

Ukweli wa mambo:

● Taasisi ya Worldwatch inaripoti kwamba “kuna wafanyakazi wa kutosha kupanua uchumi wa ulimwengu, lakini hakuna nafasi za kutosha za kazi kwa ajili yao. Tukizingatia hali mbaya ya sasa ya kiuchumi, Shirika la Wafanyakazi Ulimwenguni (ILO) linakadiria kwamba idadi ya watu wasio na kazi ilifikia watu milioni 205 katika mwaka wa 2010.”

● “Shirika la Wafanyakazi Ulimwenguni (ILO) limeonya kwamba uchumi wa ulimwenguni pote unaelekea kusababisha kipindi kipya na kibaya zaidi cha watu kupoteza kazi na hilo linaweza kutokeza msukosuko katika jamii,” inasema ripoti moja ya Shirika la Habari la BBC. “Kupungua kwa ukuzi wa kiuchumi kunaonyesha kwamba ni nusu ya nafasi za kazi zinazohitajika ndizo zitakazotokezwa. . . . Pia shirika hilo [ILO] lilikadiria kiwango cha watu kutoridhika kwa sababu ya ukosefu wa kazi na hasira zinazotokea kwa sababu watu fulani wanahisi kuwa wengine hawashirikiani katika jitihada za kutatua tatizo hilo la kiuchumi. Lilisema kwamba nchi nyingi zaidi zinakabili uwezekano wa kuwa na msukosuko wa kijamii, hasa nchi za Muungano wa Ulaya na za Uarabuni.”

● Huko Marekani, “kwa wastani, deni la kadi za mkopo sasa limezidi dola 11,000, mara tatu ya kiasi kilichokuwapo katika mwaka wa 1990,” kinasema kitabu The Narcissism Epidemic kilichochapishwa katika mwaka wa 2009. Waandishi wa kitabu hicho wanasema kwamba watu wengi huingia katika madeni ili tu waonekana kuwa matajiri. Kitabu hicho kinasema: “Wamarekani wanapomwona mtu akiwa na magari ya kifahari na mavazi ya bei ghali wanadhani yeye ni tajiri. Ukweli ni kwamba ni afadhali kusema watu hao wana madeni.”

Ni nini lazima kibadilike: Kila mtu anapaswa kuwa na kazi, na pia watu wanapaswa kuwa na maoni yanayofaa kuhusu matumizi ya pesa. Biblia inakubali kwamba “pesa ni ulinzi” lakini pia inaonya kwamba “kupenda pesa ni chanzo cha mambo mabaya ya namna zote.”—Mhubiri 7:12; 1 Timotheo 6:10.

Kutokana na habari iliyo kwenye ukurasa wa 4 hadi 8 huenda ikaonekana kwamba hakuna msingi wa kuwa na uhakika kuhusu wakati ujao. Hata hivyo, bado kuna tumaini. Hali katika ulimwengu wetu zitabadilika na kuwa nzuri—lakini mabadiliko hayo hayataletwa na serikali za wanadamu.

[Sanduku/​Grafu katika ukurasa wa 5]

Ni mambo gani ambayo vijana wanasema wangebadili katika ulimwengu? Kulingana na Tovuti ya 4children.org, uchunguzi uliofanywa kati ya watoto 2,000 hivi huko Uingereza walio na umri wa kati ya miaka 4 na 14 ulionyesha kwamba wangefanya mambo yafuatayo:

[Grafu]

(Ona fully mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Asilimia 100

KUKOMESHA NJAA

KUKOMESHA VITA

KUONDOA UMASKINI

Asilimia 75

KUFANYA WATU WOTE WATENDEWE KWA USAWA

KUKOMESHA KUONGEZEKA KWA JOTO DUNIANI

Asilimia 50

Asilimia 25

Asilimia 0

[Sanduku/​Grafu katika ukurasa wa 5]

Utafiti uliofanywa mwaka wa 2009 na Shirika la Bertelsmann nchini Ujerumani ulifunua mahangaiko makuu ya vijana 500 hivi walio na umri wa kati ya miaka 14 na 18.

Baadhi ya masuala ambayo vijana hao waliona kuwa si muhimu sana ni ugaidi na kuongezeka kwa idadi ya watu. Hata hawakuorodhesha kuzorota kwa uchumi miongoni mwa mambo ya maana sana. Kulingana na Shirika la Bertelsmann, huenda vijana hao walikuwa na maoni hayo kwa sababu bado hawajaathiriwa na matatizo hayo maishani.

[Grafu]

(Ona fully mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Asilimia 100

Asilimia 75

UMASKINI

KUBADILIKA KWA HALI YA HEWA NA KUHARIBIWA KWA MAZINGIRA

UKOSEFU WA CHAKULA NA MAJI YA KUNYWA

MAGONJWA YA KUAMBUKIZA NA MARADHI

Asilimia 50

Asilimia 25

Asilimia 0