Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

“Wadudu wa Baharini” Mlo Wenye Kufurahisha

“Wadudu wa Baharini” Mlo Wenye Kufurahisha

“Wadudu wa Baharini” Mlo Wenye Kufurahisha

Wateja wenye njaa wamekaa ndani ya mkahawa huko New York City. Wakitumia vifaa vya chuma wanavunja kwa ustadi magamba ya viumbe wakubwa walio mbele yao wanaofanana na wadudu. Huku wakipuuza macho ya wadudu hao walio kwenye sahani ambayo ni kana kwamba yanawatazama, walaji hao wenye hamu ya kula wanatafuna nyama tamu na laini ya wadudu hao. Watu hao wanakula nini? Wanakula “wadudu wa baharini” —kwa kawaida wanajulikana kama kamba-mti.

KWA nini kamba-mti huitwa wadudu wa baharini? Wavuvi walipowatazama viumbe hao wa baharini wenye magamba magumu wakitambaa kwenye mashua zao waliona kuwa wanafanana sana na wadudu.

Lakini wanafanana na wadudu kwa njia nyingine pia. Katika miaka ya 1700, kamba-mti walikuwa wamejaa kama kundi la wadudu kwenye pwani ya kaskazini-mashariki ya Marekani. Viumbe hao walivuliwa na kutandazwa kwenye mashamba ili wawe mbolea. Walitumiwa kama chambo cha kuvulia samaki. Walikuwa chakula cha wafungwa. Siku hizo, kamba-miti walikuwa kwengi sana hivi kwamba kikundi fulani cha vibarua katika eneo hilo walishinda kesi mahakamani ya kupinga kulishwa kamba-mti zaidi ya mara tatu kwa juma!

Tofauti na hilo, watu walioishi katika majiji ya mbali, walifurahia sana kula kamba-mti kwa kuwa hawakuwapata kwa urahisi. Kwa nini? Kwa sababu kamba-mti anapokufa anaoza haraka na hawawezi kuhifadhiwa kwa kutiwa chumvi au kwa kukaushwa. Hata hivyo, kufikia katikati ya miaka ya 1800, kamba-mti walianza kutiwa ndani ya mikebe, na hivyo watu wengi zaidi waliweza kufurahia ladha yao tamu. Kwa kuongezea, kuvumbuliwa kwa reli kulifanya iwezekane kusafirisha kamba-mti walio hai hadi sehemu zote za Marekani. Kwa sababu hiyo, kamba-mti walianza kuagizwa kwa wingi sana. Hata hivyo, ilikuwa gharama kubwa kusafirisha kamba-miti wakiwa hai, kwa hiyo matajiri tu ndio walioweza kuwafurahia.

Siku hizi wavuvi wanavua kamba-mti wa aina mbalimbali kwenye maeneo yote ya pwani ulimwenguni. Kamba-mti wa Marekani wanaweza kupatikana katika Bahari ya Atlantiki kuanzia Newfoundland hadi North Carolina. Soko moja la kimataifa la kamba-mti liko huko Maine, kaskazini-mashariki mwa Marekani. Kutoka huko kamba-mti waliopikwa na walio hai husafirishwa duniani pote. Wauzaji wanaweza kusafirisha kilogramu 36,287 za kamba-mti katika ndege moja.

Kwa kawaida, viwanda huzalisha chakula kingi kinachopendwa ulimwenguni pote ili vipate faida kubwa. Lakini hali ni tofauti kuhusiana na kamba-mti. Kwa sehemu kubwa, wavuvi wa kamba-mti ni wakazi wenyeji waliojiajiri. Hawafugi kamba-miti kwenye vidimbwi vya kuzalishia, badala yake wanasafiri hadi kwenye maeneo yao ya asili ili kuwakamata—kwenye Bahari ya Atlantiki.

Jinsi ya Kuvua Kamba-Mti

Wavuvi huwavuaje kamba-mti? Ili kujibu swali hilo, mwandishi wa Amkeni! alizungumza na Jack, ambaye familia yao imekuwa ikivua kamba-mti kwa vizazi vinne huko Bar Harbor, Maine. Jack alianza kuvua akiwa na umri wa miaka 17, katika ghuba ileile ambayo babu ya baba yake alikuwa akivua. Annette, mke wa Jack, pia ni mvuvi. “Niliolewa na mvuvi,” anasema Annette. “Kwa miaka miwili nilijifunza kuvua kwenye mashua ya Jack, na baadaye nikanunua mashua yangu mwenyewe.”

Jack na Annette wanawatega kamba-mti jinsi gani? Annette anaeleza hivi, “Tunachukua mgono, yaani, mtego wa chuma wenye umbo la mstatili ulio na tundu dogo na ndani yake tunatia mfuko wa wavu uliojaa chambo, hasa heringi.” Wavuvi wanafunga boya kwenye kila mtego. Annette anasema, “wavuvi hupaka maboya yao rangi tofauti ili baadaye waweze kuyatambua.”

Mara tu mtego unapotupwa baharini, unazama, na boya lililopakwa rangi linaelea juu ya maji ili wavuvi waweze kutambua mahali ambapo mitego yao ipo. “Tunaiacha mitego ndani ya maji kwa siku chache,” anasema Annette, “kisha tunarudi na kuivuta ndani ya mashua. Iwapo kuna kamba-mti ndani, tunamtoa nje na kumpima.” Wavuvi wanaojali hali ya wakati ujao kama Jack na Annette huwarudisha kamba-mti wadogo baharini; pia baadhi ya kamba-mti wa kike huachiliwa ili waendelee kutokeza kamba-mti zaidi.

Baadaye, wavuvi huelekea kwenye bandari za karibu ili kuuza kamba-mti waliowapata. Mbali na watu wachache wanaofanya kazi pamoja, hakuna mikataba iliyowekwa sahihi kati ya wavuvi na wanunuzi—wavuvi wenyeji huwauzia watu wa eneo hilo. Kama ilivyotajwa mapema, imekuwa vigumu sana kufuga kamba-mti kwenye vidimbwi vya kuzalishia. “Baadhi ya wavuvi wamepewa ruhusa ya kuvua kamba-mti wa kike wenye mayai,” anasema Jack. “Wanaangua mayai na kutunza kamba-miti wadogo kwa muda mfupi, kisha wanawarudisha baharini. Kufanya hivyo kunasaidia idadi yao isishuke sana.”

Huenda uvuvi wa kamba-mti usiwe njia rahisi ya kujipatia riziki au kuwa tajiri. Lakini ukiwauliza wavuvi hawa watakueleza kuhusu faida wanazopata—uhuru wa kuwa na biashara zao wenyewe ndogo au kuendeleza utamaduni wa kijamii na wa familia au kupata shangwe inayotokana na kuishi na kufanya kazi kwenye eneo la pwani. Jambo bora zaidi ni kwamba wavuvi hao wanapata uradhi mwingi kwa kujua kwamba watu wenye njaa ulimwenguni pote watafurahia mlo wa “wadudu wa baharini.”

[Sanduku/​Picha katika ukurasa wa 12]

HATARI ZA UVUVI WA KAMBA-MTI

Huenda mtu akafikiri kuwa kazi ya kuvua kamba-mti ni salama. Lakini sivyo. Kwa mfano, Taasisi ya Kitaifa ya Usalama na Afya Kazini (NIOSH) inasema kwamba “kuanzia mwaka wa 1993 hadi 1997, kati ya wavuvi 100,000 wa kamba-mti walio na leseni, 14 walikufa wakifanya kazi hiyo huko Maine. Idadi hiyo ni mara 2.5 ya wastani wa kitaifa (4.8 kati ya wafanyakazi 100,000) ya watu wote wanaokufa wakiwa kazini.”

Kulingana na NIOSH, uchunguzi uliofanywa na Walinzi wa Pwani wa Marekani unaonyesha kwamba “mara nyingi wavuvi wa kamba-mti hunaswa na kamba zilizoshikilia mtego, wanavutwa majini, na kuzama wanaposhindwa kujinasua au kupanda tena kwenye mashua.” Uchunguzi uliofanywa kuanzia 1999 hadi 2000, uliohusisha wavuvi 103 wa kamba-mti uliripoti kwamba wavuvi 3 kati ya 4 wamewahi kunaswa na kamba hizo, ingawa si wote waliovutwa majini. Njia salama zimependekezwa ili kuzuia wavuvi wa kamba-mti wasinaswe katika kamba hizo na pia wawe na vifaa vya kukata kamba hizo wanaponaswa.

[Picha katika ukurasa wa 10, 11]

1. Jack akivuta mtego wa kuvulia kamba-mti

2. Annette na Jack wakiwatoa kamba-mti kupitia tundu dogo kutoka kwenye mtego wa chuma

3. Kila kamba-mti anapimwa kwa kutumia chombo cha kupimia kamba-mti