Ua Kubwa Zaidi Duniani
Ua Kubwa Zaidi Duniani
“NIFUATE Bwanangu, njoo uone ua kubwa sana, linapendeza, na ni zuri ajabu,” akasema mwanaume aliyekuwa akimwongoza Joseph Arnold ambaye alikuwa akikusanya mimea kwa ajili ya utafiti kwenye kisiwa cha Indonesia cha Sumatra. Arnold, aliyekuwa mtaalamu wa mimea Mwingereza, alipomfuata mwanamume huyo alisema kwamba aliona kitu chenye “kushangaza sana.” Lilikuwa ua lenye kustaajabisha sana. Karibu miaka 200 hivi baadaye, ua hilo aliloona katika safari yake ya ugunduzi ya mwaka wa 1818, yaani ua lenye kustaajabisha la rafflesia, bado ndilo ua kubwa zaidi duniani.
Kuna jamii mbalimbali za rafflesia, na zote zinapatikana kwenye misitu ya Kusini-mashariki mwa Asia. Hata hivyo, jamii mpya zinaendelea kugunduliwa. Jamii inayotokeza ua kubwa zaidi inaitwa Rafflesia arnoldii, jina lilitokana na Joseph Arnold na mgunduzi mwenzake, Bwana Thomas Stamford Raffles, ambaye alikuwa mwanzilishi na gavana wa Singapore. Hata hivyo, licha ya kwamba ua hilo linapendeza, ni vigumu sana kulichuma ili uliweke katika shada la maua.
Kwanza, fikiria ukubwa wake. Rafflesia linaweza kukua hadi kufikia kipenyo cha mita moja hivi—ukubwa sawa na gurudumu la basi—na lina uzito wa kilogramu 11. * Ua hilo lina petali tano, nene, zenye rangi ya waridi iliyochanyika na kahawia na iliyo na madoa yenye rangi hafifu. Sehemu ya katikati ya ua hilo inafanana na shimo kubwa lililo kama chungu linaloweza kubeba lita 6 hivi za maji.
Pili, fikiria harufu yake. Kulingana na ufafanuzi fulani wa wazi, ua la rafflesia linanuka kama “mzoga wa nyati aliyeoza kabisa,” na hapo ndipo majina mengine yanayolifaa sana ua hilo yanapotokea kama vile ua-mzoga na * Nzi wanaokula mizoga ndio wachavushaji wakuu wa maua hayo kwani uvundo huo huwavutia.
yungiyungi linalonuka kama mzoga.Ua la rafflesia halina shina, majani, au mizizi na kwa sababu hiyo linategemea mimea fulani inayotambaa ya msituni. Tumba jipya la rafflesia linapotoka katika ganda la mmea unaolitegemeza, inachukua miezi kumi kwa tumba hilo kukua na mara nyingi linafikia ukubwa wa kabeji kubwa. Kisha, inachukua muda wa saa kadhaa kwa ua hilo kuchanua, wakati ambapo petali nene za ua hilo zinapofunguka na kuonyesha umaridadi wake. Sehemu ya katikati ya ua hilo ina vitu kadhaa vilivyojitokeza kama miiba vinavyoitwa processes. Kazi ya miiba hiyo bado haieleweki sana, hata hivyo watafiti fulani wanafikiri kwamba miiba hiyo inafanya kazi ya kusambaza joto na hivyo kuzidisha uvundo.
Hata hivyo, umaridadi usio wa kawaida wa ua hilo haudumu kwa muda mrefu. Baada ya siku chache tu, ua hilo linakufa na linaanza kuoza na kuacha ute mweusi wenye kuchukiza.
Ua la Rafflesia arnoldii halipatikani kwa urahisi na liko katika hatari ya kutoweka. Kwa nini? Maua ya kiume na ya kike lazima yachanue yakiwa karibu-karibu ili yaweze kuchavushana, hata hivyo matumba mengi ya maua hayo hayakomai wala kuchanua. Sababu ni kwamba matumba mengi huvunwa ili yatumiwe kama dawa za kienyeji au ili yaliwe. Hilo limefanya idadi ya maua hayo ipungue sana mwituni. Tisho lingine kubwa ni uharibifu unaoendelea wa misitu ya mvua ambamo ua hilo linapatikana.
Kuona ua la rafflesia ni tukio la pekee sana. Ukubwa wake unastaajabisha. Harufu yake haisahauliki. Na ni ua lenye umbo na rangi yenye kupendeza sana. Bila shaka, ua kubwa zaidi duniani ni moja tu kati ya kazi nyingi za ajabu za Muumba wetu. Zaburi 104:24 inasema hivi: “Jinsi kazi zako zilivyo nyingi, Ee Yehova! Zote umezifanya kwa hekima. Dunia imejaa vitu ulivyotokeza.”
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Maua mengine ya jamii ya rafflesia yana kipenyo cha sentimita 10 tu.
^ fu. 5 Ua la titan arum (Amorphophallus titanum) pia limepewa jina la utani ua-mzoga na nyakati nyingine watu hudhani ni ua la rafflesia.—Ona Amkeni! Juni 22, 2000, ukurasa wa 31.
[Ramani katika ukurasa wa 17]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
MALASIA
SUMATRA
[Picha katika ukurasa wa 17]
Tumba la “rafflesia” likiwa karibu kuchanua