Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Limau-Tunda Lenye Matumizi Mengi

Limau-Tunda Lenye Matumizi Mengi

HEBU wazia tunda linaloweza kutumiwa kama dawa, sabuni, dawa ya kuua viini, na kipodozi. Unaweza kulila, kunywa maji yake, na kukamua mafuta yake. Lina rangi yenye kupendeza, linapatikana ulimwenguni pote, na si ghali. Huenda hata sasa una tunda hilo jikoni. Ni tunda gani hilo? Ni limau!

Inadhaniwa kwamba malimau yalikuzwa kwanza Kusini-mashariki ya Asia. Lakini baada ya muda, yalisafirishwa hadi upande wa magharibi, kuelekea bahari ya Mediterania. Milimau hukua vizuri katika eneo lenye baridi na joto la kiasi, na kwa sababu hiyo, miti hiyo hukua vizuri sana huko Argentina, Hispania, Italia, Mexico, na hata sehemu za Afrika na Asia. Ikitegemea aina ya limau na eneo, mti uliokomaa unaweza kutokeza kati ya malimau 200 hadi 1,500 kwa mwaka. Aina mbalimbali za milimau huchanua maua katika majira tofauti, kwa hiyo malimau yanaweza kuvunwa mwaka mzima.

Milimau Inakita Mizizi Italia

Kuna ubishi mkali kuhusu ikiwa Waroma wa kale walikuza malimau. Hata hivyo, kuna maandishi yanayothibitisha kwamba Waroma walijua kuhusu furungu, tunda la jamii ya machungwa ambalo linafanana sana na limau kubwa. Katika kitabu chake Natural History, mwanahistoria Mroma Plini Mkubwa alitaja kihususa mfurungu na tunda lake. Hata hivyo, wataalamu maarufu wanasema kwamba Waroma walijua pia kuhusu malimau. Kwa nini? Kwa sababu picha zilizochorwa ukutani na picha nyingine zinaonyesha malimau na si mafurungu. Mfano mmoja ni nyumba kubwa iliyofukuliwa huko Pompeii, inayoitwa kwa kufaa, Nyumba ya Miti ya Matunda, kwa sababu imepambwa kwa picha zilizochorwa ukutani za mimea mbalimbali kutia ndani mlimau. Ni kweli kwamba wakati huo, huenda mti huo ulionwa kuwa wa pekee na yaelekea ulitumiwa kama dawa tu. Ni vigumu kujua ikiwa ilikuwa rahisi kukuza malimau na ikiwa yalikuzwa kwa wingi.

Kisiwa cha Sicily, ambacho huwa na majira marefu ya kiangazi yenye joto la kiasi na majira yenye baridi ya kiasi ndilo eneo ambalo hutokeza matunda ya jamii ya machungwa na malimau kwa wingi. Hata hivyo, kuna maeneo mengine, hasa ya pwani, ambapo malimau mazuri hukuzwa.

Mji maridadi wa Sorrento uko kusini kidogo ya Naples, na upande wake wa kusini kuna pwani maridadi ya Amalfi, iliyo na urefu wa zaidi ya kilomita 40. Miji maridadi ya Amalfi, Positano, Vietri sul Mare, na miji mingine iko kwenye ghuba ndogo zilizo kwenye pwani hiyo. Malimau yanayokuzwa Sorrento na pwani ya Amalfi yana cheti cha kutambulisha kwamba yamekuzwa katika eneo hilo. Wenyeji wa miji hiyo wana haki ya kulinda utambulisho wa milimau yao kwa kuwa miti hiyo imepandwa kwa ustadi kwenye matuta yaliyo ubavuni mwa mlima ambapo inapata mwangaza wa jua na kutokeza malimau yenye maji mengi na harufu nzuri.

Mtu hahitaji eneo kubwa ili kupanda mlimau. Hata unaweza kuupanda kwenye veranda iliyo na mwangaza wa kutosha wa jua, kwa kuwa milimau midogo inaweza kukua katika vyungu na inaweza kutumiwa kama mapambo. Mimea hiyo husitawi mahali penye joto na pasipo na upepo, na hasa ikiegemea ukuta. Hata hivyo, kunapokuwa na baridi kali kupita kiasi, mimea hiyo inahitaji kufunikwa au kuingizwa ndani ya nyumba.

Hayatumiwi Tu Katika Vyakula

Wewe hutumia malimau mara ngapi? Watu fulani hutia kipande katika kikombe cha chai; wengine hutumia ganda lake au maji yake katika keki. Labda wewe hukamua maji yake na kuyachanganya na maji na sukari. Wapishi ulimwenguni pote hawakosi kuwa na malimau kwa sababu wanaweza kuyatumia kwa njia mbalimbali katika mapishi. Lakini umewahi kutumia maji ya limau kama dawa ya kuua viini au kuondoa madoa?

Watu fulani hutumia nusu kipande cha limau kusafisha na kuua viini katika mbao zinatumika wakati wa kukatia vyakula. Badala ya kutumia dawa zenye klorini kuondoa madoa au kusafisha sinki, watu fulani hutumia mchanganyiko wa maji ya limau na magadi. Inasemekana kwamba kuweka nusu kipande cha limau ndani ya friji au mashine ya kuosha vyombo huondoa harufu mbaya na kufanya vifaa hivyo viwe na harufu nzuri.

Malimau hutokeza asidi sitriki, ambayo hutumika kuhifadhi na kufanya vyakula na vinywaji viwe na ladha chachu. Ganda la limau na upande wake wa ndani hutokeza pektini ambayo hutumiwa katika viwanda vya vyakula. Pia, mafuta yanayotolewa kutoka katika ganda lake hutumiwa katika vyakula, dawa, na vipodozi. Kuna matumizi mengine mengi ya tunda hilo. Kwa kweli, limau ni tunda lenye rangi yenye kupendeza, lenye ladha nzuri, na lenye matumizi mengi.