Je ni kazi ya Ubuni?
Haltere ya Nzi
Kwa nini nzi anaweza kupaa kwa ustadi na kwa njia ya pekee? Anapopigwa na upepo, anawezaje kujisawazisha kwa haraka na kudumisha mwendo wake? Jibu linahusisha, kwa sehemu, viungo vidogo vilivyo nyuma ya kila bawa vinavyoitwa haltere. *
Fikiria hili: Viungo hivyo vinafanana na fimbo ya kupigia ngoma yenye umbo la mviringo kwa mbele. Mdudu huyo anaporuka, viungo hivyo husonga juu na chini kwa mwendo uleule kama wa mabawa lakini kuelekea upande tofauti. Wanasayansi wamegundua kwamba viungo hivyo ni kama aina fulani ya magurudumu yaliyokingamana yanayosaidia wadudu hao kuwa imara wanaporuka. *
Kwa kuwa sehemu ya mbele ya haltere ina umbo la mviringo, viungo hivyo “hupiga kuelekea upande mmoja, kama penduli ya saa,” kinasema kitabu Encyclopedia of Adaptations in the Natural World. Mdudu huyo anapogeuka ghafla iwe kwa kukusudia au kwa sababu ya kusukumwa na upepo anaporuka, “sehemu ya katikati ya haltere itageuka pia,” kinasema kitabu hicho. “Kugeuka huko hutambuliwa na neva za fahamu zilizo kwenye miisho ya haltere, na taarifa hizo hufika kwenye ubongo ili nzi achukue hatua inayofaa . . . ili asibadili upande aliokuwa akielekea.” Kwa sababu hiyo, nzi husonga kwa wepesi sana na ni vigumu sana kuwakamata.
Wahandisi wanaona kwamba wataweza kutengeneza vitu kama vile roboti, vitu vidogo sana vinavyoruka vyenye umbo kama la wadudu, na vyombo vya angani kwa kutegemea utendaji wa haltere. “Nani angedhani kwamba kiumbe mdogo, asiyevutia kama nzi angetufundisha mambo mengi kiasi hiki?” akaandika mtafiti wa mambo ya angani Rafal Zbikowski.
Una maoni gani? Je, haltere za nzi zinazotenda kama magurudumu yaliyokingamana zilitokana na mageuzi? Au zilibuniwa?
^ fu. 3 Haltere zinapatikana pia katika wadudu wenye mabawa mawili, kama vile aina nyingine za nzi na mbu.
^ fu. 4 Magurudumu hayo (gyroscope) hufanyizwa kwa kiunzi kilichoshikilia sehemu iliyo kama kisahani ambacho huzunguka kwa kasi kwenye mhimili wake. Mhimili wa kisahani hicho haubadiliki licha ya msukumo wowote unaosababishwa na kitu kingine au na nguvu za sumaku au za uvutano. Kwa hiyo, magurudumu hayo yanaweza kutumiwa kutengeneza dira yenye uwezo mkubwa.