Kukosa Subira Kunaweza Kuleta Madhara
FIKIRIA mfano huu: Mwanamume fulani anaendesha gari lake kwenye barabara ambayo ni kinyume cha sheria kulipita gari lililo mbele yako. Mwanamke aliye mbele yake anaendesha gari kwa mwendo wa chini kidogo kuliko ule uliowekwa. Mwanamume huyo asiye na subira anaona kwamba mwanamke huyo anaendesha gari polepole sana. Baada ya kumfuata kwa ukaribu sana kwa dakika chache, anakosa subira kabisa na kuendesha gari kwa mwendo wa kasi na kumpita. Kwa kufanya hivyo anavunja sheria na pia anaweza kusababisha aksidenti.
Namna gani mwanamke ambaye hana subira anapofanya kazi na watu ambao hawafanyi kazi haraka na si werevu kama yeye? Au mwanamume asiye na subira ambaye kila wakati anabonyeza kidude cha kufanya lifti ije? Je, mara nyingi wewe hushindwa kuwa na subira unaposhughulika na wazazi wako waliozeeka? Au je, wewe ni mzazi ambaye hukosa subira haraka unaposhughulika na watoto wako wachanga? Je, wewe hukasirishwa haraka na makosa ya wengine?
Yaelekea kila mtu atakosa kuwa na subira pindi fulani. Lakini huenda kukawa na matokeo mabaya ikiwa ni jambo la kawaida kwa mtu kukosa subira.
Madhara kwa afya:
Imesemekana kwamba kukosa subira humfanya mtu akate tamaa, audhike, na hata apandwe na hasira. Hisia hizo zinaweza kutufanya tuwe na mkazo zaidi, na hilo linaweza kudhuru afya yetu. Uchunguzi wa hivi karibuni uliochapishwa na Chama cha Kitiba cha Marekani ulitaja kihususa kwamba kukosa subira huongeza hatari ya kupanda kwa shinikizo la damu, hata miongoni mwa vijana.
Kuna matatizo mengine ya afya yanayohusianishwa na kukosa subira. Uchunguzi wa hivi karibuni unaonyesha kwamba kukosa subira kunaweza kutokeza tatizo la kunenepa kupita kiasi. “Watafiti waligundua kwamba watu ambao hawana subira wana uwezekano mkubwa wa kuwa wanene kupita kiasi kuliko watu wenye subira,” linaripoti gazeti Washington Post. Katika maeneo fulani, vyakula visivyo na lishe ambavyo hupikwa haraka vinapatikana kwa urahisi na kwa bei nafuu wakati wote, jambo ambalo huwavutia watu wasio na subira.
Kuahirisha mambo:
Utafiti uliofanywa na Kituo cha Utafiti wa Sera za Kiuchumi huko London ulionyesha kwamba watu wasio na subira wana mazoea ya kuahirisha mambo yanayopaswa kufanywa. Je, inawezekana kwamba wao huahirisha kazi ambazo zitachukua wakati mwingi kwa sababu hawana subira ya kufanya kazi hizo hadi wazikamilishe? Vyovyote vile, mazoea ya kuahirisha mambo yanaweza kuwa na matokeo mabaya kwa mwenye kuahirisha na kwa uchumi. Kulingana na gazeti The Telegraph, linalochapishwa huko Uingereza, mtafiti Ernesto Reuben alisema kwamba “kuahirisha mambo huathiri sana kazi na kuwagharimu watu pesa nyingi [watu wasio na subira] wanapoahirisha kufanya kazi kwa muda mrefu.”
Kutumia vibaya kileo na matendo ya jeuri:
Gazeti la Uingereza, South Wales Echo linasema kwamba “watu wasio na subira wana uwezekano mkubwa wa kujihusisha katika jeuri baada ya kunywa kileo hadi usiku wa manane.” Watafiti katika Chuo Kikuu cha Cardiff walithibitisha hilo baada ya kuwachunguza mamia ya wanaume na wanawake.
Kufanya maamuzi yasiyofaa:
Kikundi cha wachanganuzi katika Kituo cha Utafiti cha Pew huko Washington, D.C., kiligundua kwamba kwa sababu ya kukosa subira watu “mara nyingi hufanya haraka maamuzi yasiyo na hekima.” Dakt. Ilango Ponnuswami, ambaye ni profesa na msimamizi wa Idara ya Huduma za Jamii katika Chuo Kikuu cha Bharathidasan, India, alifikia mkataa huohuo. Anaeleza hivi: “Kukosa subira kutakugharimu. Kutakugharimu pesa na marafiki, kutakuletea maumivu na kuteseka au madhara mengine, kwa kuwa mara nyingi watu wasio na subira hufanya maamuzi mabaya.”
Matatizo ya kifedha:
Gazeti Research Review, linalochapishwa na Benki ya Federal Reserve ya Boston linasema kwamba kukosa subira kumehusianishwa na “kuwa na madeni mengi.” Kwa mfano, huenda wenzi wa ndoa ambao wameoana hivi karibuni wakakosa subira na kutaka kuwa na vitu vyote vya nyumba mara tu baada ya kufanya harusi licha ya kwamba hawana pesa za kuvinunua. Kwa hiyo, wananunua nyumba, fanicha, gari, na vitu vingine kwa mkopo. Jambo hilo linaweza kuleta mzozo katika ndoa. Watafiti katika Chuo Kikuu cha Arkansas, Marekani wanasema kwamba “wenzi wa ndoa ambao wameoana hivi karibuni wanaoanza maisha yao kwa madeni hawana furaha kama wenzi ambao huwa na madeni machache sana au hawana madeni yoyote wanapoanza maisha ya ndoa.”
Watu fulani wanasema kwamba kukosa subira ndiko kulikosababisha kuporomoka kwa uchumi wa Marekani hivi karibuni. Gazeti Forbes ambalo huzungumzia mambo ya kiuchumi linadai kwamba “hali iliyopo sasa katika soko la ulimwengu ilisababishwa na kukosa subira na pupa. Ukosefu wa subira uliwafanya watu wengi sana wa kawaida wanunue nyumba kwa bei ya juu zaidi kuliko pesa walizokuwa nazo katika benki. Kwa hiyo, waliamua kukopa pesa nyingi sana ambazo ingewachukua miaka mingi kuzilipa—na hata katika visa fulani, hawangeweza kuzilipa maisha yao yote.”
Kupoteza marafiki:
Kukosa subira kunaweza kutufanya tupoteze uwezo wetu wa kuwasiliana. Ikiwa mtu hana subira ya kujihusisha katika mazungumzo yanayojenga, yaelekea atazungumza bila kufikiri. Huenda pia akakasirika watu wengine wanapozungumza. Mtu wa aina hiyo hana subira ya kungoja hadi mtu aseme anachotaka kusema. Kwa hiyo, msikilizaji asiye na subira anaweza kuwaharakisha wengine wamalize wanachosema kwa kuwamalizia sentensi zao au kujaribu kutumia njia nyingine kuharakisha mazungumzo.
Ukosefu huo wa subira unaweza kumfanya mtu apoteze marafiki. Dakt. Jennifer Hartstein, mtaalamu wa magonjwa ya akili aliyenukuliwa katika makala iliyotangulia anaeleza hivi: “Ni nani anayetaka kuwa na mtu ambaye kila mara anagongesha-gongesha miguu yake chini kwa kukosa subira [au] anatazama saa yake kila mara?” Kwa kweli kukosa subira si sifa nzuri. Kutafanya usiwe na marafiki.
Hayo ni baadhi tu ya mambo ambayo huenda yakatokea kwa sababu ya kukosa subira. Makala inayofuata itazungumzia jinsi ya kusitawisha sifa ya subira na kuidumisha.