Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 WANYAMA WA PORINI

Moose—Kongoni Mkubwa Aliye na Sura ya Ajabu

Moose—Kongoni Mkubwa Aliye na Sura ya Ajabu

“SURA ya moose (kongoni wa kaskazini) ni ya ajabu na haivutii. Kwa nini awe mrefu sana? Kwa nini awe na kichwa kirefu sana?” Watu wengi wana maoni kama ya Henry David Thoreau, mwandishi wa karne ya 19 aliyeandika maneno hayo kumhusu kongoni huyo. Kwa sababu ana sura ya ajabu-ajabu na ni watu wachache tu ambao wamemwona porini mnyama huyo ambaye hupenda kuwa peke yake, baadhi ya watu hudhani kwamba kongoni huyo ni mzembe na hana akili. Je, madai hayo ni ya kweli? Watafiti katika mabara ya Amerika Kaskazini, Ulaya, na Asia wamegundua mambo mengi kuhusu mnyama huyo asiye wa kawaida.

Hakuna mtu anayekana kwamba kongoni huyo ni jitu. Ingawa miguu yake ni mirefu na inamfanya asivutie, anaweza kuitumia kujilinda dhidi ya kundi zima la mbwa-mwitu. Kongoni hao hujifunza kuogelea siku chache tu baada ya kuzaliwa, na wameonekana wakiogelea umbali wa kilomita nyingi na kupiga mbizi kwenye maji yenye kina cha karibu mita sita ili kula mimea ya baharini!

Kongoni huyo anaweza kuzungusha macho yake na kutambua kitu kinaposonga nyuma yake bila ya kugeuza kichwa chake. Pia pua yake humsaidia sana. Watafiti wanasema kwamba kwa sababu matundu ya pua yake hayako karibu-karibu, yanamfanya awe na uwezo wa pekee wa kutambua mahali vitu vilipo kwa usahihi kabisa. Masikio ya kongoni huyo humsaidia sana katika kutambua mambo. Masikio yake yana uwezo wa kuzunguka pande zote, na yanaweza kunasa sauti za kongoni wengine walio umbali wa kilomita tatu hivi!

 Ndama wa kongoni huyo, ambao walifafanuliwa na mwandishi mmoja kuwa “wenye sura yenye kuchekesha,” ni wadadisi na wanapenda kucheza. Mama zao huwalinda kwa kuwatunza kwa wororo na uaminifu. Kongoni hao wa kike wenye watoto watamshambulia yeyote ambaye angetaka kuwawinda ndama wao, kutia ndani mbwa-mwitu, dubu, na hata wanadamu. Lakini ndama anapokuwa na umri wa mwaka mmoja hivi na mama yake awe ameshika mimba tena, mama humfukuza bila huruma ili mtoto huyo aanze kujitunza mwenyewe.

JINSI ANAVYOSTAHIMILI BARIDI KALI

Kwa kuwa kongoni hao hula mimea tu, wao hustahimili jinsi gani majira ya baridi kali? Njia moja ni kwa kula sana wakati wa majira ya kiangazi. Kongoni hao hula kilogramu 23 hivi za chakula kila siku, iwe mimea hiyo iko mita tatu juu ya ardhi au ndani ya maji. Chakula kingi anachokula humeng’enywa katika tumbo lake lenye sehemu nne, na kumpatia virutubisho anavyohitaji na pia kutokeza mafuta. Hata hivyo, kongoni hao hukabili hatari nyingine katika majira ya baridi kali.

Kongoni hao hukabili hali ngumu hata zaidi wakati wa baridi kali na theluji nyingi. Wakati huo hatembei sana ili asipoteze joto analopata kutoka kwenye ngozi yake yenye manyoya. Pia inakuwa vigumu kwake kuwakimbia mbwa-mwitu kunapokuwa na theluji nyingi, lakini mara nyingi, hatari kubwa zaidi kwa kongoni huyo hutoka kwa wawindaji na madereva wa magari.

Kongoni hao wanapenda sana kula chumvi inayomwagwa barabarani ili kuyeyusha theluji. Hata hivyo, kwa kuwa kongoni wana ngozi nyeusi na wana mazoea ya kuvuka barabara usiku, ni vigumu kwa madereva wa magari kuwaona na kuepuka kuwagonga. Jambo hilo limesababisha wanadamu na kongoni kupoteza maisha yao.

NI MNYAMA ANAYEPENDA KUCHEZA

Kongoni hao wameonekana wakicheza kana kwamba wanashambulia mawimbi ya bahari na wakioga kwa furaha katika chemchemi za maji moto. Kongoni wa kike na wa kiume huonekana kana kwamba wanaonyeshana upendo wanapojamiiana, na watu huguswa sana na jinsi kongoni wa kike humtunza kwa uaminifu ndama wake. Ndama wanaotunzwa na wanadamu hata wamejenga uhusiano wa karibu sana na watunzaji wao. Dakt. Valerius Geist anafikia mkataa huu: “Mnyama huyo wa ajabu mwenye sura isiyovutia, anaweza kuwa mwerevu, mwenye upendo, na mwaminifu sana.”

Ndama wa kongoni wa kaskazini ni wadadisi na wanapenda kucheza

Hata hivyo, uwe na tahadhari: Moose ni mnyama mkubwa mwenye nguvu sana. Ukimwona porini, uwe mwangalifu na usimkaribie sana. Ni vizuri kusimama mbali hasa ikiwa kuna ndama karibu. Hata hivyo, uwe na hakika kwamba hata ukiwa mbali, utastaajabu kumwona kongoni huyo mkubwa aliye na sura ya ajabu.