Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 NCHI NA WATU

Kutembelea Indonesia

Kutembelea Indonesia

INDONESIA imefanyizwa na visiwa vipatavyo 17,000. Waindonesia wanajulikana kuwa watu wenye urafiki sana, wenye subira, adabu, na ukarimu.

Chakula nchini Indonesia kinatia ndani wali, vyakula vingine, na matunda. Mara nyingi wali na vyakula vingine hutiwa vikolezo. Katika maeneo fulani, familia huketi kwenye mkeka, na kula kwa kutumia vidole kuchovya vyakula vingine kwenye wali. Waindonesia wengi hudai kwamba chakula huwa kitamu sana kinapoliwa kwa njia hiyo.

Tunda la duriani lina nyama yenye rangi ya malai na linapendwa na wengi licha ya harufu yake mbaya

Waindonesia wanapenda sanaa, dansi, na muziki. Anklong ni aina fulani ya ala ya muziki ya Indonesia; inatengenezwa kwa vipande vya mirija ya mianzi iliyoning’inizwa kwenye kiunzi. Mirija hiyo hupangwa katika njia ambayo itatokeza sauti mbalimbali inapotikiswa. Ili kucheza muziki, ni lazima wapiga ala washirikiane, kila mmoja akitikisa anklong yake kwa wakati barabara.

Orangutangu—wanaopatikana katika misitu ya mvua ya Sumatra na Borneo—ndio wanyama wakubwa zaidi wanaoishi kwenye miti. Dume aliyekomaa anaweza kuwa na uzito wa kilogramu 90.7 na mikono yenye urefu wa mita 2.4 kutoka upande mmoja hadi ule mwingine

Mpaka karne ya 15 W.K., Indonesia iliathiriwa sana na Uhindu na Ubudha. Kufikia karne ya 16, Uislamu ukawa umeathiri utamaduni wa Indonesia. Wazungu walipoenda huko katika karne ya 16 kutafuta vikolezo, waliingiza dini zilizodai kuwa za Kikristo nchini humo.

 Mashahidi wa Yehova wanaojulikana ulimwenguni pote kwa sababu ya kazi yao ya kufundisha watu Biblia, wamekuwa wakifanya kazi hiyo nchini Indonesia tangu mwaka wa 1931. Kwa sasa, kuna Mashahidi wa Yehova zaidi ya 22,000 nchini Indonesia na wanajitahidi sana kuwafikia viziwi nchini humo. Hivi karibuni, zaidi ya viziwi 500 walihudhuria mkutano wa pekee wa lugha ya ishara uliofanywa na Mashahidi wa Yehova ili kuadhimisha kifo cha Yesu Kristo.

Amkeni! huchapishwa katika lugha 98, kutia ndani Kiindonesia (lugha hiyo pia inaitwa Kibahasa cha Indonesia)