Kukabiliana na Matatizo ya Kukoma kwa Hedhi
“Ghafula nilihisi nimelemewa na huzuni bila kujua sababu. Nililia na kuanza kujiuliza ikiwa ninarukwa na akili.”
—Rondro, * mwenye umri wa miaka 50.
“Unaamka asubuhi na kupata nyumba yako ikiwa shaghalabaghala. Huwezi kupata kitu chochote unachotafuta. Mambo ambayo ulikuwa ukifanya kwa urahisi, sasa yanaonekana kuwa magumu sana, na hujui ni kwa nini hali iko hivyo.”—Hanta, mwenye umri wa miaka 55.
WANAWAKE hao si wagonjwa. Wanapitia tu kipindi cha kukoma kwa hedhi, ambacho ni badiliko la kiasili katika maisha ya mwanamke anapoacha kuwa na uwezo wa kupata watoto. Ikiwa wewe ni mwanamke, je, unakaribia kipindi hicho? Au je, unapitia kipindi hicho sasa hivi? Vyovyote vile, kadiri ambavyo wewe na wapendwa wako mnajifunza kuhusu kipindi hiki cha mabadiliko, ndivyo mtakavyoweza kukabiliana kwa njia inayofaa na matatizo yanayohusiana nacho.
Kipindi cha Kukoma Hedhi
Wanawake wengi huanza kipindi hicho wakiwa na umri wa miaka 40 na kitu, lakini wengine huanza wakiwa wamechelewa wakiwa na miaka 60 na kitu. * Kwa wanawake wengi, hedhi hukoma hatua kwa hatua. Kwa sababu ya kubadilika-badilika kwa kiwango cha homoni kinachotokezwa, huenda mwanamke akakosa kupata hedhi pindi kwa pindi, akapata hedhi wakati ambao hakutarajia, au akavuja damu nyingi isivyo kawaida wakati wa hedhi. Wanawake wachache hukoma kupata hedhi ghafula, yaani, wanakosa hedhi mwezi mmoja na huo unakuwa mwisho wa kuipata.
Kitabu kuhusu kukoma kwa hedhi (Menopause Guidebook) kinasema: “Kipindi hicho huwa tofauti kwa kila mwanamke.” Kitabu hicho kinaendelea kusema hivi: “Matatizo ya kawaida yanayohusiana na kipindi hicho ni kupata joto la ghafula mwilini,” ambalo huenda likafuatwa na kuhisi baridi. Dalili hizo zinaweza kumfanya mtu akose usingizi na kuishiwa na nguvu. Matatizo hayo huendelea kwa muda gani? Kulingana na kitabu hicho, “wanawake fulani hupatwa na joto la ghafula mwilini kwa mwaka mmoja au miwili wakati wa kipindi hicho cha kukoma kwa hedhi. Wengine hupatwa na hali hiyo kwa miaka mingi, na wachache sana husema kwamba wao hupatwa na joto la ghafula mara kwa mara maisha yao yote.” *
Kwa sababu ya kubadilika-badilika kwa kiwango cha homoni, huenda mwanamke akashuka moyo, hisia zake zikabadilika-badilika na hilo linaweza kumfanya alielie bila sababu, na pia asiwe makini sana na asahau mambo. Licha ya hayo, kitabu The Menopause Book kinasema kwamba “kuna uwezekano mkubwa kwamba mwanamke hatapatwa na mambo hayo yote.” Kwa kweli, wanawake fulani hupata matatizo machache sana na wengine hawapati matatizo yoyote wakati wa kipindi hicho.
Jinsi ya Kukabiliana na Kipindi Hicho
Kubadili mtindo wa maisha kunaweza kupunguza baadhi ya matatizo hayo. Kwa mfano, wanawake wanaovuta sigara wanaweza kupunguza mara ambazo wanapatwa na joto la ghafula kwa kuacha kuvuta sigara. Wanawake wengi hunufaika kwa kubadili mazoea yao ya kula kama vile kupunguza au hata kuacha kunywa kileo, vinywaji vyenye kafeini, na vyakula vyenye sukari au vikolezo ambavyo vinaweza kusababisha joto la ghafula mwilini. Bila shaka, ni muhimu kula vyakula mbalimbali na vyenye lishe.
Kufanya mazoezi husaidia sana kupunguza matatizo yanayohusianishwa na kukoma kwa hedhi. Kwa mfano, mazoezi yanaweza kupunguza kukosa usingizi na kusaidia kuboresha hali ya kihisia na pia kuimarisha mifupa na afya ya mtu kwa ujumla. *
Eleza Mambo Waziwazi
Rondro aliyenukuliwa mwanzoni mwa makala hii anasema hivi: “Usiteseke kimyakimya. Ukiwaeleza wapendwa wako mambo waziwazi, hawatakuwa na wasiwasi kuhusu hali yako.” Jambo hilo linaweza kuwafanya hata wakuonyeshe subira na huruma zaidi. “Upendo ni wenye ustahimilivu na wenye fadhili,” linasema andiko la 1 Wakorintho 13:4.
Wanawake wengi hunufaika kwa kusali, kutia ndani wale ambao wanahuzunika kwa sababu kipindi hicho kinawafanya wapoteze uwezo wao wa kupata watoto. Biblia inatuhakikishia hivi: “[Mungu] hutufariji sisi katika taabu zetu zote.” (2 Wakorintho 1:4, Biblia Habari Njema) Pia inafariji kujua kwamba kipindi hicho cha kukoma kwa hedhi ni cha muda tu. Kipindi hicho kinapokwisha, wanawake ambao hutunza afya yao, wanapata tena nguvu na kuendelea kufurahia maisha.
^ fu. 2 Majina yamebadilishwa.
^ fu. 6 Madaktari wanasema kwamba mwanamke amekoma hedhi anapokosa kupata hedhi kwa miezi 12 mfululizo.
^ fu. 7 Matatizo mengine ya afya, kutia ndani ugonjwa wa dundumio, maambukizo, na pia dawa fulani zinaweza kumfanya mtu apatwe na joto la ghafula mwilini. Ni jambo la hekima mtu afanyiwe uchunguzi kabla ya kuamua kwamba joto la ghafula linasababishwa na kukoma kwa hedhi.
^ fu. 11 Ili kumsaidia mwanamke kukabiliana vizuri na kipindi hicho cha kukoma kwa hedhi, huenda madaktari wakampa homoni, vitamini na madini, na dawa za kutibu kushuka moyo. Amkeni! halipendekezi dawa au matibabu yoyote.