Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

 NCHI NA WATU

Kutembelea Italia

Kutembelea Italia

ITALIA ni nchi yenye mandhari tofauti-tofauti—upande mmoja una pwani ndefu, na mwingine una milima yenye miamba; upande wa kusini una majira ya kiangazi yenye joto kali na upande wa kaskazini una majira ya baridi kali. Pia, nchi hiyo ina milima mingi ya volkano, lakini ni michache tu—kama vile Stromboli na Mlima Etna —ambayo bado hulipuka.

Italia ni mojawapo ya nchi zilizo na watu wengi zaidi barani Ulaya. Watu wengi wamezuru nchi hiyo, kutia ndani Waarabu, watu wa Byzantium, Wagiriki, Wanormani, na Wafoinike.

Watalii wakiwa kwenye mashua inayoitwa gondola kwenye mifereji ya Venice

Nchi hiyo ina hazina nyingi za kihistoria na sanaa. Magofu ya kale ya Wagiriki na Waroma au majengo ya karne ya 17 na 18 yanapatikana katika miji na majiji mengi ya Italia. Kuna michoro, sanamu za marumaru, na chemchemi zilizotengenezwa na wasanii kama Bernini, Michelangelo, na Raphael.

Chakula ni muhimu sana kwa Waitaliano, na desturi nyingi zinahusiana na vyakula vya kienyeji. Kwa kawaida wakati wa mlo, tambi huliwa kwanza, kisha nyama au samaki na mboga. Mafuta ya zeituni hutumiwa sana, kwa kuwa zeituni hukuzwa kwa wingi huko.  Pizza na risotto ni vyakula vya Kiitaliano vinavyojulikana sana.

Tambi ndicho chakula kikuu cha Waitaliano

Waitaliano wanajulikana kuwa watu wachangamfu, wakarimu, na wenye urafiki. Pia, wanapenda kuzungumza, hivyo ni kawaida kuona watu wakiongea katika sehemu za umma au wakitembea huku wakizungumza kwa furaha.

Waitaliano wengi hudai kuwa Wakatoliki, lakini ni wachache ambao huenda kanisani kwa ukawaida. Uvutano wa kanisa umefifia katika miaka ya hivi karibuni, kwa kuwa watu wengi wanapuuza sheria za kanisa kuhusu utoaji-mimba na talaka.

Idadi ya Mashahidi wa Yehova inazidi kuongezeka nchini Italia. Wanajulikana sana kwa kuwafundisha watu Biblia na pia kwa kuishi kulingana na viwango vya Biblia. Kuna zaidi ya makutaniko 3,000 ya Mashahidi wa Yehova nchini Italia, na mengi ya makutaniko hayo yanajitahidi kuwafikia watu wanaozungumza lugha nyingine mbali na Kiitaliano. Kumekuwa na uhitaji wa kuwafundisha watu Biblia katika lugha nyingine kwa sababu idadi ya wageni nchini Italia imeongezeka mara tatu katika kipindi cha miaka kumi iliyopita.

JE, WAJUA?

Ingawa Vatican City iko katika jiji la Rome, imekuwa nchi huru tangu mwaka wa 1929 na hivyo wenyeji wa Italia huiona kuwa nchi ya kigeni.

Safu ya milima ya Dolomites, iliyo kaskazini-mashariki mwa Italia