Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

KUUTAZAMA ULIMWENGU

Kuchunguza Afya

Kuchunguza Afya

Licha ya maendeleo ya kitiba, bado magonjwa yanaendelea kuwakumba wanadamu. Hata hivyo, uthibitisho unaonyesha kwamba magonjwa mengi yanaweza kuzuiwa.

Ulimwenguni

Shirika la Afya Ulimwenguni linatabiri kwamba kufikia mwaka wa 2035 kutakuwa na watu milioni 24 watakaogunduliwa kuwa na ugonjwa wa kansa kila mwaka. Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 70 ya watu wanaogunduliwa kuwa na ugonjwa huo kwa sasa. Kulingana na makadirio ya wakati huu, watu zaidi ya milioni 14 hugunduliwa kuwa na kansa kila mwaka. Karibu nusu ya watu watakaogundulika kuwa na ugonjwa wa kansa wakati huo watakuwa wamepatwa na ugonjwa huo kwa sababu ya mambo yafuatayo: ulevi, kutofanya mazoezi, kunenepa kupita kiasi, kupigwa na mionzi, na kuvuta sigara.

Uingereza

Serikali ya Uingereza ilianzisha uchunguzi kuhusu uwezekano wa kuenezwa kwa aina ya kichaa cha ng’ombe kinachoathiri wanadamu kupitia kutiwa damu mishipani. Andrew Miller, mbunge nchini Uingereza alisema hivi: “Tulipata wasiwasi sana tuliposikia kwamba ugonjwa huo usiotibika unahatarisha afya ya wananchi. Tuliambiwa kwamba ugonjwa huo ungeweza kuenea kupitia damu yenye maambukizo au kupewa figo au viungo vingine vya mwili vilivyoathiriwa.”

Norway

Uchunguzi uliofanywa kwa miaka 11 uliohusisha wenyeji 63,000 hivi nchini Norway ulionyesha kwamba, kushuka moyo kunaweza kuongeza kwa asilimia 40 hatari ya kupatwa na magonjwa ya moyo. Shirika la Ulaya Linaloshughulika na Magonjwa ya Moyo (The European Society of Cardiology) lilimnukuu mmoja wa waandishi wa uchunguzi huo aliyesema kwamba kushuka moyo hufanya mwili utokeze homoni zinazosababisha mkazo, ambazo zinaweza kumfanya mtu apatwe na magonjwa ya moyo na hata kuzuia uwezo wa mtu kufuata mashauri yatakayomsaidia kuboresha afya yake.

Marekani

Wanasayansi wanachunguza madhara ya afya yanayosababishwa na mabaki ya moshi wa sigara, yanayoachwa kwenye sehemu mbalimbali katika nyumba, vyumba vya hoteli, na kwenye magari. Madhara ya mabaki hayo yanayoendelea kujikusanya, huongezeka kadiri muda unavyopita.