Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

JE, NI KAZI YA UBUNI?

Kazi ya Sharubu za Paka

Kazi ya Sharubu za Paka

MARA nyingi paka wa nyumbani huwinda usiku. Inaonekana kwamba sharubu huwasaidia kutambua vitu na kukamata windo hasa baada ya giza kuingia.

Fikiria hili: Sharubu za paka zimeunganishwa na tishu zenye neva nyingi za fahamu. Neva hizo zina uwezo mkubwa wa kutambua hata msukumo mdogo wa hewa. Hivyo, paka wana uwezo wa kutambua vitu vilivyo karibu nao bila kuviona, jambo linalowafaa kunapokuwa na giza.

Kwa kuwa sharubu zina uwezo wa kutambua shinikizo la hewa, paka huzitumia kujua mahali na mwendo wa windo au kitu fulani. Pia, sharubu husaidia paka kupima upana wa sehemu fulani kabla ya kuingia. Kitabu Encyclopædia Britannica, kinasema kwamba “kazi ya sharubu (vibrissae) inajulikana kwa kiwango kidogo tu; hata hivyo, paka hulemaa kwa kipindi fulani cha wakati sharubu hizo zikinyolewa.”

Wanasayansi wanabuni roboti zitakazokuwa na vipokezi vinavyofanya kazi sawa na sharubu za paka ili kusaidia roboti hizo kutembea katika maeneo yenye vitu vingi bila kukwazwa. Ali Javey, mwanasayansi katika Chuo Kikuu cha California, Berkeley anasema hivi kuhusu vipokezi hivyo vinavyoitwa e-whiskers: “Vitatumia programu mbalimbali za kompyuta kwa ajili ya roboti za kisasa, zilizo rahisi kutumiwa na watu na zitakuwa pia na programu za kibiolojia.”

Una maoni gani? Uwezo wa sharubu za paka ulijitokeza wenyewe? Au ulibuniwa?