Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

TUNAYOJIFUNZA KUTOKANA NA HISTORIA

Al-Khwarizmi

Al-Khwarizmi

WATU wengi hutumia tarakimu za Kihindu na Kiarabu wanapopima uzito au wanapopiga hesabu ya matumizi yao. Kwa nini wanatumia tarakimu hizo za “Kihindu na Kiarabu”? Inaonekana kwamba msingi wa utaratibu wa sasa wa kuhesabu unaotumia tarakimu sifuri mpaka tisa, ulianzia India na kufika katika nchi za Magharibi kupitia wasomi wa enzi za kati walioandika kwa Kiarabu. Muhammad ibn-Musa al-Khwarizmi alikuwa mmojawapo wa wasomi hao wa kwanza. Huenda alizaliwa katika eneo ambalo leo ni nchi ya Uzbekistan, mwaka wa 780 W.K. hivi. Al-Khwarizmi anaitwa “shujaa wa hesabu za Kiarabu.” Kwa nini alipewa sifa hiyo?

“SHUJAA WA HESABU ZA KIARABU”

Al-Khwarizmi aliandika kuhusu matumizi bora ya desimali na alifafanua na kueneza njia za kufanya hesabu. Alizungumzia njia hizo katika kitabu chake kinachoitwa The Book of Restoring and Balancing. Neno al-jabr lililotumiwa katika kichwa cha kitabu hicho, Kitab al-jabr wa’l-muqabala katika Kiarabu, ndilo chanzo cha neno la Kiswahili aljebra. Mwandishi wa mambo ya sayansi, Ehsan Masood, alisema kwamba aljebra inaonekana kuwa mojawapo ya “njia muhimu sana ya hesabu iliyowahi kubuniwa na inayounga mkono kila sehemu katika sayansi.” *

Mwandishi mmoja alisema hivi: “Wanafunzi wengi wa sekondari wanasema haikuwa lazima kwa [al-Khwarizmi] kuvumbua kanuni hiyo.” Hata ikiwa madai yao ni ya kweli, al-Khwarizmi alisema kwamba lengo la kufafanua kanuni hizo ni ili kurahisisha kupiga hesabu katika biashara, kugawa urithi, kufanya ukaguzi na mambo mengine.

Karne nyingi baadaye, Galileo na Fibonacci, wanahisabati kutoka nchi za Magharibi, walimheshimu sana al-Khwarizmi kwa sababu ya ufafanuzi wake ulio wazi wa jinsi ya kutumia mlinganyo. Ufafanuzi wa al-Khwarizmi ulikuwa chanzo cha kufanywa kwa utafiti mwingi zaidi wa hesabu za aljebra, namba, na pembe au trigonometria. Hesabu za trigonometria ziliwawezesha wasomi wa Mashariki ya Kati kujua thamani ya pembe na upande wa pembetatu na kuboresha elimu ya nyota. *

Aljebra: “Njia muhimu sana ya hesabu iliyowahi kubuniwa”

Wale waliotumia uvumbuzi wa al-Khwarizmi, walianzisha njia mpya za kutumia desimali na kuanzisha mbinu mpya za kujua eneo na ujazo. Wachoraji ramani za ujenzi na wajenzi wa Mashariki ya Kati walitumia mbinu hizo za kisasa muda mrefu kabla ya nchi za Magharibi kuanza kutumia wakati wa vita vya dini vya kutetea kanisa. Baadaye, walianza kutumia ujuzi huo katika nchi zao wakisaidiwa na wasomi Waislamu waliokuwa mateka na wahamiaji.

HESABU ZA KIARABU ZASAMBAA

Baada ya muda, kazi za al-Khwarizmi zilitafsiriwa katika Kilatini. Mwanahisabati Mwitaliano, Fibonacci (1170-1250), anayejulikana pia kwa jina la Leonardo wa Pisa, anasifiwa sana kwa sababu ya kuhamasisha matumizi ya tarakimu za Kihindu na Kiarabu katika nchi za Magharibi. Alijifunza tarakimu hizo alipotembelea nchi za Mediterania na kisha akaandika kitabu kinachoitwa Book of Calculation.

Ufafanuzi wa al-Khwarizmi ulianza kujulikana baada ya karne kadhaa kupita. Hata hivyo, sasa kanuni na hesabu zake ni msingi wa sayansi na teknolojia, biashara na viwanda.

^ fu. 5 Katika mfumo wa kisasa wa aljebra, namba zisizojulikana zinawakilishwa na herufi kama vile x au y. Kwa mfano x + 4 = 6. Ukitoa kwa 4 katika pande zote za mlinganyo huu, utaona kwamba x ni 2. 

^ fu. 7 Wataalamu wa nyota wa Ugiriki walianzisha utaratibu wa kupiga hesabu ili kujua thamani ya pembe na pande za pembetatu. Wasomi Waislamu walitumia hesabu za pembe au trigonometria kujua upande wa Mecca. Waislamu wanapenda kusali wakitazama upande wa Mecca. Pia, hufuata utaratibu wao kwa kuchimba makaburi na kuzika wafu kuelekea upande wa Mecca na wauzaji wa nyama ambao ni waumini wa dini ya Kiislamu, hupenda kuangalia upande wa Mecca wanapochinja wanyama.