Mtu Unayempenda Anapougua
“Baba yangu alipokuwa anakaribia kutolewa hospitalini, tulimwomba daktari achunguze tena vipimo vya damu ya Baba. Daktari alituhakikishia kwamba vipimo vilikuwa sawa, lakini alikubali kuvichunguza tena. Alishangaa alipogundua kwamba vipimo viwili vilionyesha hali isiyo ya kawaida! Alituomba msamaha na kisha akamwita daktari bingwa. Baba anaendelea vizuri. Tunashukuru sana kwamba tuliuliza maswali.”—Maribel.
Wengi wetu hatufurahii kwenda hospitali. Kama mfano wa Maribel unavyoonyesha, msaada tunaopata kutoka kwa rafiki au mtu wa ukoo unaweza kutusaidia sana—huenda hata ukaokoa maisha yetu. Unawezaje kumsaidia mtu unayempenda?
Kabla ya kwenda hospitali. Msaidie kuandika dalili na dawa anazotumia mgonjwa. Pia, andika maswali yoyote mtakayohitaji kumuuliza daktari. Msaidie rafiki yako kukumbuka habari zozote kuhusu ugonjwa wake au ikiwa ugonjwa huo umewahi kumpata mtu mwingine katika familia yao. Usifikiri kwamba daktari anajua habari hizo au ataziulizia.
Mnapokuwa kwa daktari. Hakikisha kwamba wewe na mgonjwa mnaelewa maelezo ya daktari. Uliza maswali lakini usisisitize maoni yako. Mruhusu mgonjwa aulize maswali na ajieleze. Sikiliza kwa makini na andika mambo muhimu. Uliza kuhusu njia mbalimbali za matibabu. Katika hali fulani, huenda ikawa jambo la hekima kumwambia mgonjwa atafute maoni ya daktari mwingine.
Baada ya kumwona daktari. Pitieni habari zote mlizozungumzia na daktari. Hakikisha kwamba anatumia dawa sahihi. Mtie moyo atumie dawa kulingana na maelekezo na kutoa taarifa mara moja kwa daktari ikiwa atapata madhara yoyote yanayotokana na dawa hizo. Msihi mgonjwa awe na mtazamo mzuri na mtie moyo afuate maagizo yoyote ya ziada aliyopewa kama vile kurudi tena hospitali ili kutibiwa. Msaidie aelewe mengi zaidi kuhusu ugonjwa wake.
Hospitalini
Uwe mtulivu na chonjo. Huenda mgonjwa anapofika hospitali akawa na wasiwasi na kukata tamaa. Ukiwa mtulivu na msikivu, unaweza kumsaidia pia kutulia na kuepuka kukosea. Hakikisha kwamba mgonjwa wako amejaza kwa usahihi fomu zote za hospitali anazopaswa kujaza. Heshimu haki ya mgonjwa ya kuamua aina ya matibabu anayopenda. Ikiwa ni mgonjwa sana na hawezi kufanya hivyo, heshimu maamuzi yake aliyoandika awali na mamlaka aliyompa ndugu yake wa karibu au mwakilishi wake. *
Chukua hatua ya kwanza. Usiogope kuzungumza. Heshima na adabu yako inaweza kuwafanya madaktari na wauguzi kumtendea vizuri mgonjwa na kumpa huduma bora. Katika hospitali nyingi, wagonjwa hutibiwa na madaktari mbalimbali. Unaweza kuwarahisishia kazi yao kwa kuwaeleza yale ambayo madaktari wengine wamesema. Kwa kuwa unamjua mgonjwa, waeleze ikiwa umeona mabadiliko yoyote ya mwili au akili yake.
Onyesha heshima na shukrani. Mara nyingi wafanyakazi wa hospitali hufanya kazi chini ya hali ngumu. Hivyo, watendee kama ambavyo ungependa kutendewa. (Mathayo 7:12) Heshimu kazi yao, onyesha kwamba una uhakika wanaweza kufanya kazi yao, na uwashukuru kwa jitihada zao. Kuwathamini kunaweza kuwachochea wafanye vizuri zaidi.
Hatuwezi kuepuka kuugua. Hata hivyo, unaweza kumsaidia rafiki yako au mtu wa familia yako anayeugua kwa kujitayarisha na kutoa msaada unaohitajika.—Methali 17:17.
^ fu. 8 Utaratibu na sheria zinazohusu haki na wajibu wa mgonjwa zinatofautiana kati ya nchi moja na nyingine. Hakikisha kwamba habari zinazohusu maamuzi ya mgonjwa wako ni sahihi na za karibuni.