Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Je, Wakristo waliofunga ndoa wanaweza kuiona njia ya kupanga uzazi kwa kutumia kitanzi (IUD) kuwa njia inayopatana na Maandiko?

Wenzi wa ndoa wanaweza kuchanganua mambo hakika kuhusu jambo hilo na kanuni za Biblia zinazohusika. Kisha wanapaswa kufanya uamuzi utakaowasaidia kudumisha dhamiri safi mbele za Mungu.

Mwanzoni wakati ambapo kulikuwa na wanadamu wawili tu (na baada ya Gharika wanadamu wanane), Yehova aliamuru hivi: “Zaeni, muwe wengi.” (Mwa. 1:28; 9:1) Biblia haisemi kwamba amri hiyo inawahusu Wakristo. Hivyo, ni jukumu la wenzi wa ndoa kuamua iwapo watatumia njia fulani ya kupanga uzazi na pia kuamua wakati wa kupata watoto. Wanapaswa kufikiria mambo gani?

Wakristo wanapaswa kuchunguza kanuni za Biblia zinazohusika wanapoamua ni njia gani ya kupanga uzazi watakayotumia. Hivyo, Wakristo hawatoi mimba kama njia ya kupanga uzazi. Kutoa mimba kimakusudi kunapingana na yale ambayo Biblia inasema kuhusu kuheshimu uhai. Wakristo hawakatizi uhai ambao mwishowe ungetokeza mtoto. (Kut. 20:13; 21:22, 23; Zab. 139:16; Yer. 1:5) Vipi kuhusu matumizi ya kitanzi?

Jambo hilo lilizungumziwa katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Oktoba 15, 1979 (ukurasa wa 22-23). Vitanzi vilivyotumika sana wakati huo vilitengenezwa kwa plastiki isiyosababisha madhara yoyote mwilini na viliingizwa kwenye tumbo la uzazi ili kuzuia mimba. Makala hiyo ilitaja kwamba haikujulikana kikamili jinsi ambavyo vitanzi hivyo vilifanya kazi. Wataalamu wengi walisema kwamba vitanzi hivyo hutokeza mazingira ambayo huzuia shahawa kufikia yai la mwanamke na kutunga mimba. Ikiwa mimba haikutungwa, basi uhai mpya haukutokezwa.

Hata hivyo, uthibitisho fulani ulionyesha kwamba nyakati nyingine mimba ilitungwa. Yai hilo lililotungishwa linaweza kubaki ndani ya mirija ya uzazi au Falopia (yaani, mimba iliyotungwa nje ya tumbo la uzazi) au linaweza kufika katika tumbo la uzazi. Ikiwa yai hilo litafika kwenye tumbo la uzazi, uwepo wa kitanzi utalizuia lisijipachike kwenye ukuta wa ndani wa tumbo la uzazi na hivyo kufanya mimba hiyo isiendelee kukua. Kukatiza uhai huo unaoendelea kukua ni sawa na kutoa mimba. Makala hiyo ilimalizia kwa kusema hivi: “Mkristo mnyofu anayefikiria sana juu ya kama inafaa kutumia . . . IUD anapaswa kufikiria habari hiyo kwa uzito kupatana na maoni ya Biblia ya kuheshimu utakatifu wa uhai.”—Zab. 36:9.

Je, kuna maendeleo yoyote ya kisayansi au ya kitiba tangu makala hiyo ilipochapishwa mwaka wa 1979?

Kwa sasa, kuna aina mbili za vitanzi. Aina moja ni kitanzi chenye madini ya shaba ambacho kilianza kutumika sana nchini Marekani mwaka wa 1988. Pia, aina nyingine ni kitanzi kinachotoa homoni ambacho kilianza kupatikana mwaka wa 2001. Tunajua nini kuhusu jinsi vitanzi hivyo hufanya kazi?

Shaba: Kama ilivyotajwa mapema, inaonekana kwamba vitanzi hufanya iwe vigumu kwa shahawa kupita kwenye tumbo la uzazi na kufikia yai. Zaidi ya hilo, shaba iliyo ndani ya vitanzi huua shahawa. * Isitoshe, inasemekana kwamba vitanzi vyenye shaba hubadili mazingira ya ukuta wa ndani wa tumbo la uzazi.

Homoni: Kuna aina mbalimbali za vitanzi vyenye homoni inayofanana na ile inayopatikana katika vidonge vya kuzuia mimba. Vitanzi hivyo humwaga homoni hizo ndani ya tumbo la uzazi. Inaonekana kwamba vitanzi hivyo huzuia upevushaji wa mayai (ovulation) kwa baadhi ya wanawake. Bila shaka, yai lisipopevushwa, mimba haiwezi kutungwa. Mbali na kuzuia kupevushwa kwa yai, inasemekana kwamba homoni zilizo katika vitanzi hivyo hufanya ukuta wa ndani wa tumbo la uzazi uwe dhaifu. * Pia, hufanya uteute ulio kwenye shingo ya kizazi uwe mzito na hivyo kuzuia shahawa zisitoke kwenye uke na kuingia kwenye tumbo la uzazi. Vitanzi vya homoni hufanya kazi kama vitanzi vya plastiki isiyosababisha madhara na pia hutimiza mambo hayo tuliyozungumzia.

Kama tulivyoona, inaonekana kwamba aina zote mbili za vitanzi hubadili mazingira ya ukuta wa ndani wa tumbo la uzazi. Hata hivyo, vipi ikiwa yai linapevushwa na mimba inatungwa? Yai hilo lililotungishwa linaweza kufika kwenye tumbo la uzazi lakini likashindwa kukua kwa sababu ukuta wa ndani wa tumbo la uzazi umekuwa dhaifu. Hilo lingesababisha mimba iharibike ikiwa bado changa. Hata hivyo, inasemekana kwamba visa kama hivyo ni nadra sana kama tu inavyodhaniwa kwamba nyakati nyingine vidonge vya kuzuia mimba husababisha mimba iharibike.

Hivyo, hakuna yeyote anayeweza kusema kwa uhakika kwamba vitanzi vyenye shaba au homoni huzuia kabisa mimba isitungwe. Hata hivyo, uthibitisho wa kisayansi unaonyesha kwamba kwa sababu ya jinsi ambavyo vitanzi hivyo hufanya kazi ni nadra sana kwa mimba kutungwa.

Wenzi wa ndoa Wakristo wanaofikiria kutumia kitanzi wanaweza kuzungumza na mtaalamu wa mambo ya kitiba kuhusu aina mbalimbali za vitanzi vinavyopatikana katika eneo lao na pia manufaa na madhara yanayoweza kumpata mke. Wenzi wa ndoa hawapaswi kutarajia au kumruhusu mtu mwingine, hata daktari mwenyewe, awafanyie uamuzi huo. (Rom. 14:12; Gal. 6:4, 5) Huo ni uamuzi wao binafsi. Wenzi wa ndoa wanapaswa kufanya uamuzi huo wakiwa na nia ya kumpendeza Mungu na kudumisha dhamiri safi mbele zake.—Linganisha 1 Timotheo 1:18, 19; 2 Timotheo 1:3.

^ fu. 4 Mwongozo kutoka Huduma ya Afya ya Kitaifa ya Uingereza unasema hivi: “Vitanzi vyenye shaba nyingi vinazuia mimba kwa zaidi ya asilimia 99. Hiyo inamaanisha kwamba ni wanawake wasiozidi asilimia moja wanaotumia vitanzi watakaopata mimba katika muda wa mwaka mmoja. Vitanzi vyenye shaba kidogo vina uwezo mdogo wa kuzuia mimba.”

^ fu. 5 Kwa sababu vitanzi vyenye homoni huufanya ukuta wa tumbo la uzazi uwe dhaifu, nyakati nyingine madaktari huvitumia kuwatibu wanawake walioolewa au waseja ambao hupoteza damu nyingi wakati wa hedhi.