Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

SIMULIZI LA MAISHA

Nimefanya Kile Nilichopaswa Kufanya

Nimefanya Kile Nilichopaswa Kufanya

KWA ZAIDI ya miaka 30, Donald Ridley aliwatetea kisheria Mashahidi wa Yehova. Alitimiza jukumu muhimu katika kuwasaidia madaktari waelewe haki za wagonjwa za kukataa kutiwa damu mishipani. Kazi yake ilisaidia tengenezo kushinda kesi nyingi mahakamani. Rafiki zake walizoea kumwita Don, na alikuwa mwenye bidii, mnyenyekevu, na mwenye kujidhabihu.

Mwaka wa 2019, Don aligunduliwa na ugonjwa wa mfumo wa neva usio wa kawaida na usio na tiba. Ugonjwa huo ulimdhoofisha haraka, naye akafa Agosti 16, 2019. Lifuatalo ni simulizi lake.

Nilizaliwa huko St. Paul, Minnesota, nchini Marekani mwaka wa 1954 katika familia ya Kikatoliki yenye kipato cha kati. Mimi ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto watano. Nilisoma shule ya msingi ya Kikatoliki, na nilikuwa mvulana anayetumikia madhabahuni. Lakini bado, nilikuwa na ujuzi mdogo sana wa Biblia. Ingawa niliamini kwamba lazima kuwe kuna Mungu ambaye aliumba vitu vyote, nilipoteza imani katika kanisa.

NAJIFUNZA KWELI

Mwaka wangu wa kwanza katika Chuo cha Sheria cha William Mitchell, Mashahidi wa Yehova walinitembelea nyumbani kwangu. Nilikuwa nikifua, na kwa fadhili wenzi walionitembelea walikubali kurudi wakati mwingine. Waliporudi, niliwauliza maswali mawili: “Kwa nini watu wema hawafanikiwi sana katika ulimwengu?” na “Mtu anaweza kufanya nini ili awe na furaha?” Nilikubali kitabu Kweli Iongozayo Kwenye Uzima wa Milele na Biblia Takatifu—Tafsiri ya Ulimwengu Mpya, iliyokuwa na jalada la kijani lenye kuvutia. Pia, nilikubali kujifunza Biblia. Kwa kweli jambo hilo lilinifungua macho. Nilivutiwa na wazo la kwamba Ufalme wa Mungu ndiyo serikali tunayohitaji sana ambayo itasimamia masuala ya wanadamu duniani. Niliona kwamba utawala wa wanadamu ulikuwa umeshindwa kabisa na kwamba ulisababisha ulimwengu ujae maumivu, mateso, ukosefu wa haki, na misiba.

Nilijiweka wakfu kwa Yehova mwanzoni mwa mwaka wa 1982 na nikabatizwa baadaye mwaka huo kwenye Kusanyiko la “Kweli ya Ufalme” lililofanyika katika kituo cha jamii cha St. Paul. Nilirudi katika kituo hicho juma lililofuata ili kufanya mtihani wa uwakili wa jimbo la Minnesota. Mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba, nilipata habari kwamba nilifaulu mtihani huo, ambao ulinistahilisha kufanya kazi ya uwakili.

Katika Kusanyiko la “Kweli ya Ufalme,” nilikutana na Mike Richardson, Mwanabetheli kutoka Brooklyn, ambaye alinieleza kwamba idara ya sheria ilikuwa imeanzishwa katika makao makuu. Nilikumbuka maneno ya towashi Mwethiopia kwenye Matendo 8:36 nami nikajiuliza, ‘Ni nini kinachonizuia kuomba kufanya kazi katika Idara ya Sheria?’ Hivyo, nilijaza ombi la kutumikia Betheli.

Wazazi wangu hawakufurahi kwamba nilikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Baba yangu alitaka kujua jinsi ambavyo ningenufaika kwa kufanya kazi nikiwa wakili wa Watchtower. Nilimweleza kwamba ningefanya kazi nikiwa mjitoleaji. Nilimwambia kwamba ningepokea dola 75 za Marekani kila mwezi, kiasi ambacho Wanabetheli walipokea kama rudishio la kila mwezi.

Baada ya kukamilisha mkataba wangu wa kikazi katika mahakama fulani, nilianza utumishi wangu wa Betheli huko Brooklyn, New York, mwaka wa 1984. Nilipata mgawo katika Idara ya Sheria. Huo ulikuwa wakati mwafaka kabisa kwangu.

UKARABATI WA JUMBA LA SINEMA LA STANLEY

Jumba la Sinema la Stanley lilivyokuwa kabla ya kununuliwa

Jumba la Sinema la Stanley huko Jersey City, New Jersey, lilinunuliwa Novemba 1983. Akina ndugu waliomba vibali vya kukarabati mifumo ya umeme na mabomba ya jengo hilo. Walipokutana na maofisa wa eneo hilo, akina ndugu walieleza kwamba walikusudia kutumia jumba hilo la sinema kama ukumbi wa kufanyia makusanyiko ya Mashahidi wa Yehova. Jambo hilo lilitokeza mgogoro. Sheria za jiji hilo kuhusu matumizi ya majengo ziliruhusu majengo ya ibada yawepo tu kwenye maeneo ya makazi. Jumba la Sinema la Stanley lilikuwa katika eneo la biashara, hivyo maofisa wa jiji walikataa kutoa vibali. Akina ndugu walikata rufaa, lakini rufaa yao ilikataliwa.

Katika juma langu la kwanza Betheli, tengenezo lilifungua kesi ya mashtaka kwenye mahakama ya wilaya ili kupinga uamuzi wa kunyimwa vibali. Kwa sababu nilikuwa nimetoka tu kukamilisha miaka miwili ya kufanya kazi katika mahakama ya wilaya huko St. Paul, Minnesota, nilizifahamu vizuri kesi za namna hiyo. Mmoja wa wanasheria wetu alitoa hoja kwamba Jumba la Sinema la Stanley lilikuwa limetumiwa kwa ajili ya matukio kadhaa ya umma, kama vile maonyesho ya sinema na matamasha ya muziki wa roki. Hivyo basi, kwa nini iwe kinyume cha sheria kuwa na tukio la kidini kwenye jumba hilo? Mahakama ya wilaya ilichunguza jambo hilo na kufikia uamuzi kwamba jiji la Jersey City lilikuwa limeingilia uhuru wetu wa kidini. Mahakama iliamuru jiji hilo litoe vibali tulivyohitaji, nami nilianza kuona jinsi Yehova alivyobariki tengenezo lake kuhusiana na matumizi ya njia za kisheria ili kuendeleza kazi yake. Nilifurahi sana kwamba nilitimiza fungu fulani katika kazi hiyo.

Akina ndugu walianzisha mradi mkubwa wa ukarabati, na programu ya kuhitimu ya darasa la 79 la Shule ya Gileadi ikafanyika katika Jumba la Kusanyiko la Jersey City Septemba 8, 1985, chini ya mwaka mmoja tangu ukarabati ulipoanza. Nilihisi nimependelewa sana kuendeleza masilahi ya Ufalme katika Idara ya Sheria, na hisia za kuridhika nilizokuwa nazo zilizidi kwa mbali sana hisia zozote nilizowahi kuwa nazo nilipokuwa nikifanya kazi za kisheria kabla ya kuja Betheli. Sikuwahi kuwazia kwamba Yehova angenipa mapendeleo mengi zaidi kama hayo wakati ujao.

KUTETEA HAKI ZA MATIBABU YASIYOHUSISHA DAMU

Katika miaka ya 1980, lilikuwa jambo la kawaida kwa madaktari na hospitali kupuuza ombi la Shahidi aliye mtu mzima la kutotiwa damu mishipani. Wanawake wajawazito walikabili changamoto kubwa hata zaidi kwa sababu kwa kawaida mahakimu walihisi kwamba wanawake hao hawakuwa na haki ya kisheria ya kukataa kutiwa damu mishipani. Mahakimu walitoa hoja kwamba ikiwa mwanamke mjamzito angekosa kutiwa damu mishipani, huenda angekufa na mtoto angebaki bila mama.

Desemba 29, 1988, Dada Denise Nicoleau alipoteza damu nyingi baada ya kujifungua mwana wake. Kiwango chake cha hemoglobini kilishuka chini ya 5.0, na madaktari walimwomba awape idhini ya kumtia damu mishipani. Dada Nicoleau alikataa. Asubuhi iliyofuata, hospitali ilitafuta amri ya mahakama ambayo ingewapa wafanyakazi wa hospitali mamlaka ya kumtia mgonjwa damu ambayo walihisi ilikuwa lazima wampe. Hakimu huyo, bila kusikiliza kesi hiyo au hata kumtaarifu Dada Nicoleau au mume wake, aliipa hospitali mamlaka ya kumtia damu mishipani.

Ijumaa, Desemba 30, wafanyakazi wa hospitali walimtia damu Dada Nicoleau licha ya pingamizi kutoka kwa mume wake na watu wengine wa familia yake waliokuwa naye hospitalini. Jioni hiyo, watu kadhaa wa familia yake na mzee mmoja au wawili walikamatwa kwa madai ya kwamba walizunguka kitanda cha Dada Nicoleau kama ukuta ili kuzuia asitiwe damu mishipani. Jumamosi asubuhi, Desemba 31, vyombo vya habari vya jiji la New York City na Long Island vilikuwa vikiripoti kuhusu kukamatwa huko.

Nikiwa na Philip Brumley tulipokuwa vijana

Jumatatu asubuhi, nilizungumza na Milton Mollen, aliyekuwa hakimu katika mahakama ya juu zaidi. Nilimweleza habari kamili kuhusu kesi hiyo, nikisisitiza kwamba hakimu wa mahakama ya chini alikuwa ametia sahihi agizo la kumtia mgonjwa damu mishipani bila kusikiliza kesi. Hakimu Mollen aliniomba nifike ofisini kwake baadaye alasiri hiyo ili kuzungumzia habari kuhusu kesi hiyo na sheria zilizohusika. Msimamizi wangu wa idara, Philip Brumley, aliandamana pamoja nami kwenda kwa ofisi ya Hakimu Mollen jioni hiyo. Pia, hakimu alimwalika wakili wa hospitali hiyo ili ajiunge pamoja nasi. Mazungumzo yetu yalikuwa makali. Wakati fulani, Ndugu Brumley aliandika jambo fupi kwenye daftari lake akiniambia kwamba ninapaswa “kuzungumza kwa upole.” Ninapotafakari hilo, kwa kweli lilikuwa shauri zuri kwa sababu hasira zilikuwa zikinipanda upesi nilipokuwa nikipinga hoja za wakili wa hospitali.

Kutoka kushoto kwenda kulia: Richard Moake, Gregory Olds, Paul Polidoro, Philip Brumley, mimi, na Mario Moreno—waliokuwa mawakili wetu siku ambayo kesi ya Watchtower v. Village of Stratton iliposikilizwa katika Mahakama Kuu ya Marekani.​—Tazama gazeti Amkeni! la Januari 8, 2003

Baada ya saa moja hivi, Hakimu Mollen alisema kwamba kesi hiyo ingekuwa ya kwanza kusikilizwa kesho yake asubuhi. Tulipokuwa tukiondoka ofisini kwake, Hakimu Mollen alisema kwamba wakili wa hospitali angekuwa na “kazi ngumu kesho.” Alimaanisha kwamba isingekuwa rahisi kwa wakili huyo kutetea hoja zake. Nilihisi kwamba Yehova alikuwa akinihakikishia kuwa tulikuwa na uwezekano mkubwa wa kushinda. Nilistaajabu kuona jinsi Yehova alivyokuwa akitutumia sisi kutimiza mapenzi yake.

Tulifanya kazi hadi usiku sana tukiandaa hoja ambazo tungetumia asubuhi iliyofuata. Mahakama iko karibu na Betheli ya Brooklyn, hivyo ndugu na dada wengi katika Idara yetu ndogo ya Sheria walitembea ili kufika hapo. Baada ya jopo la mahakimu wanne kusikiliza hoja zetu, walifikia uamuzi kwamba agizo la kutia damu mishipani halikupaswa kutolewa. Mahakama hiyo ya juu ilimuunga mkono Dada Nicoleau na kusema kwamba desturi ya kutafuta kibali kwa mahakama bila kumtaarifu mhusika ilikuwa ukiukaji wa haki za msingi za kikatiba.

Muda mfupi baada ya hapo, mahakama ya juu zaidi ya New York iliunga mkono uamuzi wa kwamba Dada  Nicoleau alikuwa na haki ya kupata matibabu yasiyohusisha damu. Kesi hiyo ndiyo iliyokuwa ya kwanza kati ya kesi nne kuhusu damu zilizoamuliwa na mahakama za juu za majimbo mbalimbali ambayo nilipata pendeleo la kushiriki. (Tazama sanduku “ Ushindi Katika Mahakama Kuu za Majimbo.”) Pia, nimeshirikiana na mawakili wengine wa Betheli katika kesi zinazohusisha malezi ya watoto, talaka, na sheria zinazohusu matumizi ya ardhi na majengo.

NDOA NA MAISHA YA FAMILIA

Nikiwa na mke wangu, Dawn

Nilipokutana kwa mara ya kwanza na mke wangu, Dawn, alikuwa ametalikiwa na alikuwa akilea watoto watatu. Alikuwa akijiruzuku huku akiendelea na upainia. Alikuwa amepitia hali ngumu maishani, nami nilivutiwa sana na azimio lake la kumtumikia Yehova. Katika mwaka wa 1992, tulihudhuria Kusanyiko la Wilaya la “Wachukuaji Nuru” lililofanyika New York City, nami nikamwomba tuwe wachumba. Mwaka mmoja baadaye, tulifunga ndoa. Kuwa na mke wa kiroho na aliye mcheshi ni zawadi kutoka kwa Yehova. Kwa kweli, Dawn amenithawabisha kwa mema sikuzote za maisha yetu pamoja.—Met. 31:12.

Tulipofunga ndoa, watoto walikuwa na umri wa miaka 11, 13, na 16. Nilitaka kuwa baba mzuri kwao, hivyo nilisoma kwa makini na kutumia kila kitu nilichosoma katika machapisho yetu kuhusu kuwa mzazi wa kambo. Kulikuwa na changamoto kadiri miaka ilivyopita, lakini ninafurahi kwamba watoto walinikubali na kunitumaini kuwa rafiki na baba yao anayewapenda. Sikuzote rafiki za watoto wetu walikuwa huru kutembelea nyumba yetu, na tulifurahi kuwa pamoja na vijana hao wenye nguvu.

Mwaka wa 2013, mimi pamoja na Dawn tulihamia Wisconsin ili kuwatunza wazazi wetu waliozeeka. Ajabu ni kwamba utumishi wangu wa Betheli haukuisha. Nilialikwa kuendelea kusaidia katika mambo ya kisheria ya tengenezo letu nikiwa mjitoleaji wa muda.

BADILIKO LA GHAFLA

Septemba 2018, niligundua kwamba nilikuwa nikikohoa mara nyingi kabla ya kuzungumza. Daktari wetu alinichunguza lakini hakuweza kutambua tatizo. Baadaye, daktari mwingine alipendekeza nikamwone daktari wa mfumo wa neva. Januari 2019, daktari huyo aliniambia kwamba huenda nina ugonjwa usio wa kawaida unaoitwa progressive supranuclear palsy (PSP) unaoathiri mfumo wa neva.

Siku tatu baadaye, nilipokuwa nikicheza mchezo wa kuteleza kwenye barafu, nilivunjika kwenye fundo la mkono wangu wa kulia. Nimekuwa nikiteleza kwenye barafu maisha yangu yote; ni jambo nililozoea kufanya. Hivyo nilijua kwamba nilikuwa nikipoteza uwezo wangu wa kudhibiti misuli. Nimeshangaa kuona jinsi ugonjwa huo ulivyonidhoofisha kwa kasi sana na kuathiri sana uwezo wangu wa kuongea, kutembea, na kumeza.

Nimependelewa sana kutumia uzoefu wangu nikiwa mwanasheria kutimiza fungu dogo katika kuendeleza masilahi ya Ufalme. Nimepata pendeleo la kuandika makala nyingi katika majarida ya kitaaluma na vilevile kuhutubu katika semina za mambo ya kisheria kuhusu tiba kotekote ulimwenguni, nikitetea haki za watu wa Yehova za kuchagua matibabu na upasuaji usiohusisha damu. Lakini bado nitanukuu Luka 17:10: ‘Mimi ni mtumwa asiyefaa kitu. Nimefanya kile nilichopaswa kufanya.’