Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Maswali Kutoka kwa Wasomaji

Baada ya Yesu kuzaliwa, kwa nini Yosefu na Maria waliendelea kukaa Bethlehemu badala ya kurudi nyumbani kwao huko Nazareti?

Biblia haitoi sababu. Lakini inataja mambo yenye kupendeza ambayo huenda yalichangia uamuzi huo.

Malaika alimwambia Maria kwamba angepata mimba na kuzaa mtoto. Malaika alipoleta ujumbe huo, Maria na Yosefu walikuwa wakiishi Nazareti, mji wa nyumbani wa Yosefu huko Galilaya. (Luka 1:26-31; 2:4) Baadaye, waliporudi kutoka Misri, walirudi Nazareti. Yesu alilelewa huko na akawa Mnazareti. (Mt. 2:19-23) Ndiyo maana tunawahusianisha wote watatu—Yesu, Yosefu, na Maria—na mji wa Nazareti.

Maria alikuwa na mtu wa ukoo aliyeitwa Elisabeti, ambaye aliishi huko Yuda. Elisabeti alikuwa mke wa kuhani Zekaria na baadaye akawa mama ya Yohana Mbatizaji. (Luka 1:5, 9, 13, 36) Maria alikuwa amemtembelea Elisabeti na kukaa naye kwa miezi mitatu huko Yuda. Kisha Maria akarudi Nazareti. (Luka 1:39, 40, 56) Kwa hiyo, Maria alilifahamu eneo la Yuda.

Baada ya muda, Yosefu alitii agizo la “kuandikishwa.” Hivyo, Yosefu akasafiri kutoka Nazareti kwenda Bethlehemu, ambalo liliitwa “jiji la Daudi” na ilikuwa imetabiriwa kwamba Masihi angezaliwa huko. (Luka 2:3, 4; 1 Sam. 17:15; 20:6; Mika 5:2) Baada ya Maria kumzaa Yesu akiwa huko, Yosefu hakutarajia Maria afunge safari ndefu ya kurudi Nazareti akiwa na mtoto mchanga. Walikaa huko Bethlehemu, mji uliokuwa kilomita tisa kutoka Yerusalemu. Hivyo, ilikuwa rahisi kwao kwenda na mtoto wao hekaluni ili kutoa dhabihu iliyohitajika.​—Law. 12:2, 6-8; Luka 2:22-24.

Hapo awali, malaika wa Mungu alikuwa amemwambia Maria kwamba mwana wake angepokea “kiti cha ufalme cha Daudi” naye ‘angetawala akiwa Mfalme.’ Je, inawezekana Maria na Yosefu walihisi lilikuwa jambo muhimu kwamba Yesu alizaliwa katika jiji la Daudi? (Luka 1:32, 33; 2:11, 17) Huenda walifikiri ni jambo la hekima kuendelea kukaa huko na kusubiri kuona jambo ambalo Mungu alitaka wafanye.

Hatujui walikuwa wamekaa kwa muda gani huko Bethlehemu wale wanajimu walipofika. Hata hivyo, wakati huo familia yao ilikuwa ikiishi ndani ya nyumba, na mwana wao alikuwa “mtoto” na si mtoto mchanga. (Mt. 2:11) Inaonekana kwamba badala ya kurudi huko Nazareti, walikaa muda mrefu vya kutosha huko Bethlehemu hivi kwamba walikuwa na nyumba yao.

Herode aliagiza kwamba “wavulana wote huko Bethlehemu . . . kuanzia umri wa miaka miwili kwenda chini” wauawe. (Mt. 2:16) Baada ya kuonywa na Mungu kuhusu agizo hilo, Yosefu na Maria walikimbilia huko Misri pamoja na Yesu na wakakaa huko mpaka Herode alipokufa. Baadaye, Yosefu aliipeleka familia yake huko Nazareti. Kwa nini hawakurudi Bethlehemu? Ili kumwepuka Arkelao, mwana mkatili wa Herode, aliyekuwa huko Yudea, na ili kutii onyo la Mungu. Huko Nazareti, ilikuwa salama kwa Yosefu kumlea Yesu akiwa mwabudu wa kweli wa Mungu.​—Mt. 2:19-22; 13:55; Luka 2:39, 52.

Inaonekana Yosefu alikufa kabla Yesu hajafungua njia ya kwenda mbinguni. Hivyo, Yosefu atafufuliwa hapa duniani. Watu wengi watakutana naye na kujifunza habari zaidi kutoka kwake kuhusu sababu zilizomfanya yeye na Maria waendelee kukaa Bethlehemu baada ya Yesu kuzaliwa.