Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Unajimu na Kubashiri​—Je, Ni Njia Sahihi za Kujua Kuhusu Wakati Ujao?

Unajimu na Kubashiri​—Je, Ni Njia Sahihi za Kujua Kuhusu Wakati Ujao?

UNAJIMU

Unajimu ni aina ya uaguzi inayotegemea imani ya kwamba nyota, mwezi, na sayari huathiri maisha ya wanadamu duniani kwa kiwango kikubwa. Wanajimu wanaamini kwamba utu na maisha ya wakati ujao ya mtu hutegemea mahali ambapo nyota, mwezi, na sayari zilikuwa wakati anazaliwa.

Ingawa unajimu ulianzia Babiloni ya kale, bado aina hii ya uaguzi ni maarufu leo. Kulingana na utafiti uliofanywa Marekani mwaka wa 2012, asilimia 33 hivi ya watu waliohojiwa walisema kwamba unajimu “unaonekana kuwa mbinu ya kisayansi,” na asilimia 10 walisema “unajimu ni mbinu ya kisayansi kabisa.” Je, ni kweli? Hapana. Kwa sababu:

  • Sayari na nyota hazina uwezo wowote wa kuathiri maisha ya wanadamu kama ambavyo wanajimu wanaamini.

  • Mara nyingi utabiri wa wanajimu ni wa ujumla kiasi kwamba unaweza kumhusu mtu yeyote yule.

  • Utabiri wa wanajimu leo unategemea imani ya kale kwamba sayari huzunguka dunia. Ukweli ni kuwa, sayari huzunguka jua na si dunia.

  • Utabiri unaotolewa na wanajimu tofauti kumhusu mtu yuleyule huwa unatofautiana.

  • Wanajimu huwagawanya watu katika makundi 12, au alama za unajimu, kwa kutegemea tarehe ambayo mtu amezaliwa. Kadiri miaka inavyopita, dunia imekuwa ikihama kutoka pale ilipokuwa, hivyo kwa sasa jua linapita kwenye makundi ya nyota yanayowakilisha zile alama 12 katika tarehe tofauti na zile zilizotambuliwa awali.

Inasemekana kuwa alama za unajimu husaidia kujua utu wa mtu. Ukweli ni kwamba watu ambao wamezaliwa tarehe ileile huwa na utu tofauti; tarehe ya mtu ya kuzaliwa haiwezi kufunua utu wake. Badala ya kuwaona wengine kama tu walivyo, wanajimu huelezea utu na tabia za watu kwa kutegemea habari za kukisia. Je, hii si aina ya ubaguzi?

KUBASHIRI

Tangu nyakati za kale, watu wamekuwa wakiwaendea wabashiri. Baadhi ya wabashiri hao walitafuta habari za mtu kwa kutumia viungo vya ndani ya miili ya wanadamu na wanyama au kwa kuangalia jinsi jogoo anavyodonoa chakula chake. Wengine walitoa utabiri wao kwa kuangalia michoro iliyo kwenye majani ya chai au kwa kutumia mbegu za kahawa. Leo, wabashiri hutumia kadi, mipira ya kioo, dadu, na njia nyingine za “kusoma” wakati ujao wa mtu. Je, ubashiri ni njia sahihi ya kujua kuhusu wakati ujao? Hapana. Acheni tuchunguze sababu.

Kwanza kabisa, utabiri unaofanywa kwa kutumia njia mbili tofauti za kubashiri mara nyingi hutofautiana. Hata ikiwa mbinu ileile inatumika, matokeo hutofautiana. Kwa mfano, tunatarajia kwamba wabashiri wawili wakiulizwa swali lilelile kuhusu wakati ujao na wakatumia kadi zilezile kutoa utabiri wao, jibu lao litakuwa moja. Lakini mara nyingi haiwi hivyo.

Mbinu au nia za wabashiri zinatiliwa shaka. Wachambuzi wanasema kwamba kadi au mipira ya kioo ni mbinu za kijanja tu. Wabashiri huchunguza hasa jinsi mhusika anavyotenda na si vifaa wanavyodai kutumia. Kwa mfano, mbashiri stadi anaweza kuuliza maswali ya kawaida tu, halafu anamsikiliza na kumtazama kwa makini mteja wake ili aone ishara zozote zitakazomfunulia habari za mtu huyo. Kisha mbashiri huyo ataonekana kuwa na uwezo wa kujua habari za mteja wake, ambazo kwa kweli mteja huyo amemfunulia bila yeye kujua. Baada ya kuhakikisha kwamba wateja wao wanawaamini, baadhi ya wabashiri wamefanikiwa kuchuma pesa nyingi sana kutoka kwao.

BIBLIA INASEMA NINI?

Kutafuta habari kutoka kwa wanajimu na wabashiri kunabeba wazo la kwamba maisha yetu yamepangwa. Lakini je, hilo ni kweli? Biblia inasema kwamba tuna uwezo wa kuamua mambo tutakayoamini au tutakayofanya, na maamuzi yetu huathiri maisha yetu ya wakati ujao.—Yoshua 24:15.

Mungu anakataza aina zote za uaguzi, na hiyo ni sababu nyingine inayowafanya waabudu wake wasijihusishe na unajimu au kubashiri. Biblia inasema hivi: “Asipatikane miongoni mwenu mtu yeyote . . . anayefanya uaguzi, mtu yeyote anayefanya uchawi, mtu yeyote anayetafuta ishara za ubashiri, mlozi, mtu yeyote anayewafunga wenzake kwa uchawi, mtu yeyote anayetafuta ushauri kutoka kwa watu wanaowasiliana na roho, mpiga ramli, au mtu yeyote anayetafuta habari kuhusu wafu. Kwa maana mtu yeyote anayefanya mambo haya ni chukizo kwa Yehova.” *Kumbukumbu la Torati 18:10-12.

^ Jina la yule ‘Aliye Juu Zaidi, juu ya dunia yote.’—Zaburi 83:18.