Mnara wa Ukumbusho Unaothibitisha Usahihi wa Unabii
KATIKATI YA JIJI LA ROMA NCHINI ITALIA, KUNA MNARA WA USHINDI AMBAO HUWAVUTIA WATU WENGI ULIMWENGUNI POTE. MNARA HUO ULIJENGWA ILI KUMUENZI TITO, MMOJA WA MALIKI WALIOPENDWA SANA KATIKA MILKI YA ROMA.
Mnara wa ukumbusho wa Tito una michoro miwili mikubwa inayohusu tukio la kihistoria linalojulikana sana. Hata hivyo, jambo moja ambalo halifahamiki sana ni uhusiano kati ya mnara huo na Biblia—Mnara wa ukumbusho wa Tito unathibitisha usahihi wa hali ya juu wa unabii wa Biblia.
JIJI LILILOLAANIWA
Mwanzoni mwa karne ya kwanza W.K., Milki ya Roma ilianzia Uingereza na Gaul (ambayo sasa ni Ufaransa) hadi kufikia Misri, na eneo lote hilo lilikuwa na utulivu na ufanisi wa pekee. Lakini kulikuwa na eneo moja katika milki hiyo ambalo lilisababisha vurugu mara kwa mara—eneo la Yudea.
Kitabu kimoja (Encyclopedia of Ancient Rome) kinasema: “Ni maeneo machache katika milki ya Roma ambayo yalisitawisha chuki kama iliyokuwepo kati ya Waroma na watu wa Yudea. Wayahudi waliwachukia watawala wa kigeni ambao hawakujali tamaduni zao, na Waroma waliona ukaidi wa Wayahudi kuwa ndio chanzo cha wao kuwakandamiza.” Wayahudi wengi walitarajia kwamba Masihi angekuja na kuwa kiongozi ambaye angewafukuza Waroma na kulirudishia taifa la Israeli utukufu wake wa awali. Lakini katika mwaka wa 33 W.K., Yesu Kristo alitangaza kwamba jiji la Yerusalemu litaharibiwa.
Yesu alisema: “Siku zitakuja, adui zako watakapojenga ngome yenye miti iliyochongoka kukuzunguka, nao watakuzingira kila upande. Watakuangusha chini wewe na watoto wako walio ndani yako, nao hawataacha jiwe juu ya jiwe lingine.”—Luka 19:43, 44.
Ni wazi kwamba maneno ya Yesu yaliwashangaza wanafunzi wake. Siku mbili baadaye, mmoja wao alisema hivi alipoliona hekalu la Yerusalemu: “Mwalimu, ona! jinsi mawe na majengo haya yalivyo maridadi!” Inasemekana kwamba baadhi ya mawe ya hekalu yalikuwa na urefu wa meta 11, upana wa meta 5, na kimo cha meta 3! Hata hivyo, Yesu aliwajibu hivi: “Vitu hivi mnavyoona, siku zitakuja ambapo hakuna jiwe litakaloachwa juu ya jiwe lingine bila kuangushwa chini.”—Marko 13:1; Luka 21:6
Yesu aliongezea kusema: “Mtakapoona Yerusalemu limezingirwa na majeshi yaliyopiga kambi, jueni kwamba linakaribia kuharibiwa. Ndipo wale walio Yudea waanze kukimbilia milimani, na wale walio Yerusalemu waondoke, nao wale walio mashambani wasiingie ndani yake.” (Luka 21:20, 21) Je, maneno ya Yesu yalitimia?
JIJI LAANGUKA
Miaka thelathini na tatu ilipita na bado Wayahudi walichukia kutawaliwa na Waroma. Lakini katika mwaka wa 66 W.K. gavana Mroma aliyetawala Yudea, Gessius Florus, alichukua pesa kutoka kwenye hazina ya hekalu. Wayahudi, ambao tayari walikuwa na hasira, hawakuweza kuvumilia kukandamizwa zaidi. Baada ya muda, kikundi cha wapiganaji Wayahudi kilivamia Yerusalemu, na kuwaua wanajeshi wa kikosi cha Roma waliokuwa jijini humo, kisha wakajitangaza kuwa huru kutokana na utawala wa Waroma.
Miezi mitatu hivi baadaye, zaidi ya wanajeshi Waroma 30,000 walioongozwa na Sesho Galo, walienda Yerusalemu ili kukomesha uasi uliotokea. Mathayo 24:15, 16.
Waroma waliingia jijini mara moja na kuuangusha ukuta uliozunguka eneo la hekalu. Halafu, bila sababu yoyote ya msingi, waliondoka. Vikosi vya waasi vya Wayahudi vilishangilia na vikaanza kuwakimbiza. Kwa kuwa vikosi vilivyopigana vilikuwa vimeondoka jijini, Wakristo walitii onyo la Yesu na kuondoka Yerusalemu, wakakimbilia milimani ng’ambo ya Mto Yordani.—Mwaka uliofuata, jeshi la Roma lilirudi tena Yudea likiongozwa na Jenerali Vespasian na mwanaye aliyeitwa Tito. Hata hivyo, mara baada ya Maliki Nero kufa katika mwaka wa 68 W.K., Vespasian alirudi Roma ili achukue utawala, na kumwachia Tito jukumu la kuwaongoza wanajeshi 60,000 hivi waliopaswa kuishambulia Yerusalemu.
Mnamo Juni mwaka wa 70 W.K., Tito aliwaagiza wanajeshi wake wakate miti ya eneo la mashambani la Yudea, na kuitumia kujenga ukuta wa miti iliyochongoka uliozunguka jiji la Yerusalemu kwa urefu wa kilometa 7. Kufikia mwezi wa Septemba, Waroma walikuwa wameingia jijini, wamepora mali, wakalichoma jiji na hekalu lake, na kuangusha jiwe moja baada ya jingine kama Yesu alivyokuwa ametabiri. (Luka 19:43, 44) Inakadiriwa kwamba, “kati ya watu 250,000 hadi 500,000 walikufa jijini Yerusalemu na katika maeneo mengine ya nchi.”
USHINDI MKUBWA KWELIKWELI
Mwaka wa 71 W.K., Tito alirudi nchini Italia na kukaribishwa kwa shamrashamra na wakazi wa jiji la Roma. Watu wote jijini walitoka ili kushangilia msafara ambao ulikuwa ndio mkubwa zaidi kuwahi kuonekana katika jiji la Roma.
Umati huo wa watu ulistaajabu kuona mali nyingi sana zikipitishwa katika mitaa ya jiji. Kulikuwa na meli zilizotekwa, majukwaa yenye magurudumu na yaliyokuwa na picha za matukio mbalimbali ya vita, na vyombo vilivyoporwa kwenye hekalu la Yerusalemu.
Katika mwaka wa 79 W.K., Tito alichukua nafasi ya baba yake, Vespasian, na kuwa maliki. Lakini, miaka miwili baadaye, Tito alikufa ghafla. Kaka yake aliyeitwa Domitiani, alianza kutawala na mara moja akajenga mnara wa ukumbusho ili kumuenzi Tito.
WATU WANAUONAJE MNARA HUO LEO?
Leo, mamia ya maelfu ya watu ambao hutembelea Roma kila mwaka, huvutiwa sana na mnara wa ukumbusho wa Tito. Baadhi yao huuona kama kazi nzuri sana ya sanaa, wengine kama kitu kinachowakilisha uwezo wa milki ya Roma, na bado wengine kama kumbukumbu ya anguko la Yerusalemu na hekalu lake.
Hata hivyo, kwa watu wanaosoma Biblia kwa makini, Mnara wa Ukumbusho wa Tito ni wenye umaana mkubwa hata zaidi. Unathibitisha kwamba unabii wa Biblia ni sahihi na wenye kutegemeka, jambo linaloonyesha kwamba Mungu ndiye aliyeongoza uandikwe.—2 Petro 1:19-21.