Mfalme wa Ufalme wa Mungu Ni Nani?
Mungu aliwaongoza baadhi ya waandishi wa Biblia kuandika habari zinazomtambulisha Yule atakayekuwa Mfalme wa Ufalme wa Mungu. Mtawala huyo
-
Angechaguliwa na Mungu. “Mimi mwenyewe nimemweka mfalme wangu . . . Nitakupa mataifa kuwa urithi wako na miisho ya dunia kuwa miliki yako.”—Zaburi 2:6, 8.
-
Angekuwa mrithi wa Mfalme Daudi. “Mtoto amezaliwa kwetu, tumepewa mwana . . . Kwa wingi wa utawala wake na amani, hakutakuwa na mwisho, kwenye kiti cha ufalme cha Daudi na juu ya ufalme wake ili kuuimarisha kabisa.”—Isaya 9:6, 7.
-
Angezaliwa Bethlehemu. “Ee Bethlehemu . . . , kutoka kwako atatoka kwa ajili yangu yule atakayekuwa mtawala . . . Ukuu wake utafika kwenye miisho ya dunia.” —Mika 5:2, 4.
-
Angekataliwa na watu na kuuawa. “Alidharauliwa, nasi tulimwona kuwa asiye na maana. . . . Alichomwa kwa sababu ya makosa yetu; alipondwa kwa sababu ya dhambi zetu.”—Isaya 53:3, 5.
-
Angefufuliwa na kutukuzwa. “Hutaniacha Kaburini. Hutamruhusu mshikamanifu wako aone shimo. . . . Kuna furaha kwenye mkono wako wa kuume milele.”—Zaburi 16:10, 11.
Yesu Kristo—Mtawala Anayefaa
Katika historia ya wanadamu, ni mtu mmoja tu aliyetimiza kikamili sifa za kuwa mtawala anayefaa. Mtu huyo ni Yesu Kristo. Malaika alimwambia hivi Maria, mama ya Yesu: “Mungu atampa kiti cha ufalme cha Daudi baba yake, . . . na Ufalme wake hautakuwa na mwisho.”—Luka 1:31-33.
Yesu hakuwahi kamwe kuwa mtawala alipokuwa duniani. Badala yake, atawatawala wanadamu kutoka mbinguni akiwa Mfalme wa Ufalme wa Mungu. Kwa nini Yesu ndiye Mtawala anayefaa? Hebu tuchunguze mambo ambayo Yesu alifanya alipokuwa duniani.
-
Mathayo 9:36; Marko 10:16) Mtu mwenye ukoma alipomwomba Yesu: “Ikiwa tu unataka, unaweza kunitakasa,” Yesu alimhurumia na kumponya.—Marko 1:40-42.
Yesu aliwajali watu. Yesu aliwasaidia wanaume na wanawake, vijana kwa wazee, licha ya malezi au hadhi yao katika jamii. ( -
Yesu alitufundisha jinsi ya kumpendeza Mungu. Alisema hivi: “Hamwezi kutumikia Mungu na Utajiri.” Pia, Yesu alifundisha kanuni muhimu aliposema kwamba mambo yote tunayotaka watu watutendee, ni lazima sisi pia tuwatendee vivyo hivyo. Kanuni hiyo inaitwa Kanuni Bora. Isitoshe, Yesu alitufundisha kwamba Mungu anapendezwa na mambo tunayofanya na pia yale tunayofikiri na kuhisi. Hivyo, ili tumpendeze Mungu, tunahitaji kudhibiti hisia zetu. (Mathayo 5:28; 6:24; 7:12) Yesu alikazia kwamba ili tuwe na furaha ya kweli, tunapaswa kujifunza mambo yanayompendeza Mungu na kuishi kulingana nayo.—Luka 11:28.
-
Yesu alifundisha jinsi ya kuwapenda wengine. Maneno na matendo ya Yesu yalikuwa na nguvu sana na yaligusa mioyo ya wasikilizaji wake. “Umati ukashangazwa na njia yake ya kufundisha, kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye mamlaka.” (Mathayo 7:28, 29) Aliwafundisha “kuwapenda adui [zao].” Yesu hata alisali kwa ajili ya baadhi ya watu waliohusika kumuua. Alisali hivi: “Baba, wasamehe, kwa maana hawajui wanachofanya.”—Mathayo 5:44; Luka 23:34.
Yesu anafaa kabisa kuwa Mtawala wa ulimwengu kwa sababu ni mwenye fadhili na yuko tayari kuwasaidia watu. Hata hivyo, ataanza kutawala lini?