Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, kurekebisha utendaji wa chembe za urithi za wanadamu kumerefusha maisha?

Jitihada za Kurefusha Maisha

Jitihada za Kurefusha Maisha

“Nimeona kazi ambayo Mungu amewapa wanadamu wajishughulishe nayo. Amefanya kila kitu kipendeze kwa wakati wake. Hata ameweka umilele katika moyo wao.”​Mhubiri 3:10, 11.

MANENO hayo yaliyosemwa zamani na Mfalme mwenye hekima, Sulemani, yanafafanua kwa usahihi kabisa hisia za wanadamu kuhusu uhai. Huenda kwa sababu ya ufupi wa maisha na kwamba kifo hakiepukiki, kwa muda mrefu wanadamu wamekuwa wakijaribu kurefusha maisha yao. Kuna masimulizi mengi ya watu ambao wamekuwa wakitafuta mbinu za kuongeza urefu wa maisha yao.

Kwa mfano, fikiria Gilgamesh mfalme wa Sumeria. Watu wamesimulia hadithi nyingi za kubuni kuhusu maisha yake. Mojawapo wa hadithi hizo (Epic of Gilgamesh) inasimulia kwamba alifunga safari ndefu iliyokuwa hatari ili kutafuta njia za kuepuka kifo. Jitihada zake ziligonga mwamba.

Mkemia akiwa kwenye maabara yake (500 W.K.-1500 W.K.)

Miaka 2,400 hivi iliyopita, wakemia nchini China walitengeneza kinywaji walichoamini kwamba kingerefusha maisha. Kinywaji hicho kilikuwa na mchanganyiko wa kiwango fulani cha zebaki na aseniki. Inasemekana kwamba maliki kadhaa wa China walikufa kwa kunywa kinywaji hicho. Huko Ulaya, kati ya miaka ya 500 W.K. hadi 1500 W.K., baadhi ya wakemia walijaribu kutengeneza dhahabu kwa njia ambayo mwili wa mwanadamu ungeweza kuimeng’enya, kwa kuwa waliamini kwamba uwezo wa dhahabu wa kutoharibika ungeweza kurefusha maisha.

Leo, baadhi ya wanabiolojia na wataalamu wa chembe za urithi wanachunguza ili waelewe sababu hasa inayofanya tuzeeke. Kama wakemia waliotengeneza kinywaji cha kuongeza urefu wa maisha, utafiti huu unathibitisha kwamba wanadamu bado wana tumaini la kupata njia ya kuzuia uzee na kifo. Lakini matokeo yamekuwaje?

MUNGU “AMEWEKA UMILELE KATIKA MOYO WAO.”​—MHUBIRI 3:10, 11

JITIHADA ZINAZOFANYWA ILI KUBAINI CHANZO CHA UZEE

Wanasayansi wanaochunguza chembe za wanadamu wametoa sababu tofauti-tofauti zaidi ya 300 ambazo wanadhani ndizo chanzo cha kuzeeka na kufa. Katika miaka ya karibuni, wanasayansi wamefanikiwa kuongeza urefu wa maisha ya chembe za wanadamu na za wanyama wanaofanyiwa uchunguzi kwenye maabara kwa kuboresha utendaji wa chembe za urithi na protini. Maendeleo kama hayo yamewachochea baadhi ya watu wenye uwezo kufadhili utafiti unaofanywa ili kubaini chanzo cha kifo. Ni nini kilichotimizwa kufikia sasa?

Kupunguza kasi ya kuzeeka. Baadhi ya wanasayansi wanaamini kwamba uzee husababishwa na kufupika kwa kisehemu kilicho mwishoni mwa kila kromosomu, kinachoitwa telomeres. Kisehemu hicho hulinda taarifa za chembe za urithi, chembe hizo zinapokuwa zikijigawanya. Lakini kila mara chembe inapojigawanya, urefu wa kisehemu hicho hupungua. Hatimaye, chembe huacha kujigawanya, na kusababisha mtu aanze kuzeeka.

Mshindi wa Tuzo ya Nobeli mwaka wa 2009, Elizabeth Blackburn na wenzake, waligundua kimeng’enya kinachopunguza kasi ya kufupika kwa telomeres, na kwa njia hiyo kupunguza kasi ya kuzeeka kwa chembe. Hata hivyo, katika ripoti yao wanakiri kwamba telomeres “hazina uwezo wa kufanya tuishi muda mrefu zaidi ya tunaoishi sasa.”

Kurekebisha utendaji wa chembe za uhai ni njia nyingine ya kuzuia uzee. Chembe zinapozeeka sana na kushindwa kujigawanya, zinaweza kutuma taarifa zisizo sahihi kwenye chembe jirani zinazokinga mwili, na hivyo kusababisha uvimbe, maumivu sugu, na ugonjwa. Hivi majuzi, wanasayansi nchini Ufaransa walirekebisha utendaji wa chembe za watu wenye umri mkubwa, ambao baadhi yao walikuwa na miaka zaidi ya 100. Kiongozi wa utafiti huo, Profesa Jean-Marc Lemaître alisema, kazi yao imefunua kwamba inawezekana ‘kurudisha ubora’ kwenye chembe zilizozeeka.

JE, WANASAYANSI WANAWEZA KUONGEZA UREFU WA MAISHA YETU?

Wanasayansi wengi wanasema kuwa mbinu zinazotumiwa haziwezi kuongeza urefu wa maisha yetu kuliko tunavyoishi sasa. Ni kweli kwamba kuanzia karne ya 19, wanadamu wanaishi muda mrefu kuliko ilivyokuwa awali. Lakini hilo limewezekana kwa sababu ya kuzingatia zaidi usafi, kudhibitiwa kwa magonjwa ya kuambukiza, na kupatikana kwa chanjo na dawa za kuua bakteria. Baadhi ya wataalamu wa chembe za urithi wanaamini kwamba urefu wa maisha ya wanadamu ni kama umefikia kikomo chake.

Miaka 3,500 hivi iliyopita, mwandikaji mmoja wa Biblia, Musa, alikiri hivi: “Urefu wa maisha yetu ni miaka 70, au miaka 80 ikiwa mtu ana nguvu za pekee. Lakini imejaa taabu na huzuni; nayo hupita haraka, nasi hutokomea.” (Zaburi 90:10) Licha ya jitihada nyingi za wanadamu za kurefusha maisha, kimsingi maisha yetu yapo kama tu Musa alivyofafanua.

Kwa upande mwingine, baadhi ya wanyama wanaweza kuishi kwa mamia ya miaka, na miti kama vile mibuyu inaweza kuishi kwa maelfu ya miaka. Tunapolinganisha urefu wa maisha yetu na ya viumbe hawa na wengine pia, swali linalokuja akilini ni: ‘Je, kweli tulikusudiwa tuishi miaka 70 au 80 tu?’