Kutoa Ujumbe wa Faraja Nchini Italia
Sisi Ni Namna ya Watu Walio na Imani
Kutoa Ujumbe wa Faraja Nchini Italia
YEHOVA ndiye “Mungu wa faraja yote.” Watumishi wake wanapojifunza kumwiga, ‘waweza kufariji wale walio katika namna yoyote ya dhiki.’ (2 Wakorintho 1:3, 4; Waefeso 5:1) Hilo ni mojawapo ya malengo mengi ya kazi ya kuhubiri ambayo Mashahidi wa Yehova wanafanya.
Kumsaidia Mwanamke Mwenye Uhitaji
Hasa katika miaka ya hivi majuzi umaskini, vita, na tamaa ya kupata maisha bora zaidi vimewafanya watu wengi wahamie katika nchi zenye utajiri zaidi. Licha ya hayo, si jambo rahisi kuzoea makao mapya. Manjola alikuwa anaishi na Waalbania wenzake katika Borgomanero. Kwa kuwa alikuwa akiishi nchini Italia kinyume cha sheria, alisita kuongea na Wanda, ambaye ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Ijapokuwa hivyo, hatimaye Wanda aliahidi kukutana na Manjola, ambaye alionyesha upendezi mkubwa mara moja wa kujifunza Neno la Mungu, hata ingawa kizuizi cha lugha kilifanya hilo kuwa gumu. Hata hivyo, baada ya ziara kadhaa, Wanda hakuweza kumkuta yeyote nyumbani. Kwani kulitokea nini? Wanda alijulishwa kwamba wakazi wote wa nyumba hiyo wametoroka kwa sababu mmoja wao—rafiki wa kiume wa Manjola—anatafutwa kwa kuua kimakusudi!
Miezi minne baadaye, Wanda alikutana tena na Manjola. “Huku akiwa dhaifu na amekonda, alifanana na mtu aliyekabili magumu kwelikweli,” asema Wanda. Manjola alieleza kwamba rafiki yake wa kiume wa awali alikuwa gerezani, na kwamba rafiki ambao Manjola aliwaendea wampe msaada walimvunja moyo sana. Huku akiwa amekata tamaa, Manjola alisali kwa Mungu ampe msaada. Kisha akamkumbuka Wanda, aliyesema naye habari za Biblia. Manjola alifurahi kama nini kumwona tena!
Funzo la Biblia lilianzishwa tena, na punde si punde Manjola akaanza kuhudhuria mikutano ya Kikristo. Alifaulu kupata kibali halali cha kuishi nchini Italia. Baada ya mwaka mmoja, Manjola akawa Shahidi aliyebatizwa. Akiwa amefarijika na ahadi za Mungu, amerudi nchini Albania ili kuushiriki ujumbe wa Biblia unaofariji na wananchi wenzake.
Kutoa Ushahidi Kwenye Kambi ya Wahamiaji
Makutaniko mengi nchini Italia yamefanya mipango ya kuwatolea ushahidi wahamiaji kama Manjola.
Kwa kielelezo, kutaniko moja huko Florence lilifanya mipango ya kutembelea kambi moja ya wahamiaji kwa ukawaida. Wakazi kambini humo—wengi wao kutoka Ulaya Mashariki, Makedonia, na Kosovo—walikuwa wakikabili magumu mbalimbali. Baadhi yao walikabili matatizo ya dawa za kulevya na kileo. Wengi walijiruzuku kwa kuiba vitu vidogo-vidogo.Ilikuwa kazi ngumu kuhubiri katika jumuiya hiyo. Hata hivyo, hatimaye mweneza-evanjeli wa wakati wote aitwaye Paola akamtembelea Jaklina, bibi wa Makedonia. Baada ya mazungumzo machache, Jaklina alimtia moyo Susanna rafiki yake aichunguze Biblia. Susanna naye akazungumza na jamaa wengine. Muda si muda, washiriki watano wa familia wakaanza kujifunza Biblia kwa ukawaida, kuhudhuria mikutano ya Kikristo, na kutumia maishani mambo waliyokuwa wakijifunza. Licha ya matatizo ambayo hawana budi kukabili, wanapata faraja kutoka kwa Yehova na Neno lake.
Mtawa Akubali Faraja Kutoka kwa Yehova
Mjini Formia, mweneza-evanjeli wa wakati wote aitwaye Assunta alisema na mwanamke aliyekuwa akitembea kwa shida. Mwanamke huyo alikuwa mtawa, mshiriki wa jamii ya kidini inayotoa misaada kwa wagonjwa na walemavu hospitalini na pia nyumbani.
Assunta akamwambia mtawa huyo: “Wewe pia unateseka, sivyo? Yasikitisha kwamba sote tuna matatizo tunayopambana nayo.” Mara mtawa huyo akaangua kilio na kueleza kwamba ana matatizo mabaya sana ya afya. Assunta alimtia moyo, na kumwambia kwamba Mungu wa Biblia aweza kumfariji. Mtawa akakubali magazeti yenye msingi wa Biblia ambayo Assunta alimpa.
Kwenye mazungumzo yao yaliyofuata, mtawa huyo, aitwaye Palmira, alikiri kwamba anateseka sana. Alikuwa ameishi kwa muda mrefu katika taasisi moja inayosimamiwa na watawa. Ilipombidi kuondoka humo kwa muda mfupi kwa sababu za afya, hakuruhusiwa kurudi. Hata hivyo, Palmira aliona kwamba amefungamanishwa na Mungu kupitia nadhiri alizoweka akiwa mtawa. Aliwaendea waponyaji ili “kutibiwa,” lakini aliteseka sana kutokana na matibabu hayo. Palmira alikubali kujifunza Biblia, naye akahudhuria mikutano ya Kikristo kwa mwaka mmoja. Kisha akahamia eneo jingine, na Shahidi hakuweza kuwasiliana naye. Miaka miwili ikapita kabla ya Assunta kumpata tena. Palmira alipata upinzani mkali kutoka kwa familia yake na makasisi. Ijapokuwa hivyo, alianza kujifunza Biblia tena, akafanya maendeleo ya kiroho, na kubatizwa akiwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova.
Naam, wengi hufarijiwa na ujumbe wa ‘Mungu apaye faraja.’ (Waroma 15:4, 5) Basi, Mashahidi wa Yehova nchini Italia wameazimia kuendelea kumwiga Mungu kwa kuwapa wengine ujumbe wake mzuri ajabu wa faraja.