Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kujulisha Tumaini la Kikristo Nchini Senegal

Kujulisha Tumaini la Kikristo Nchini Senegal

Sisi Ni Aina Iliyo na Imani

Kujulisha Tumaini la Kikristo Nchini Senegal

SAMAKI ni chakula kikuu tangu nyakati za kale. Kwa maelfu ya miaka watu wamevua samaki katika bahari, maziwa, na mito ya dunia. Baadhi ya mitume wa Yesu Kristo walikuwa wavuvi katika Bahari ya Galilaya. Lakini Yesu aliwaanzishia aina nyingine ya uvuvi. Huo ulikuwa uvuvi wa kiroho ambao ungewanufaisha wavuvi na samaki pia.

Kuhusu hilo, Yesu alimwambia hivi mvuvi Petro: “Tangu sasa na kuendelea utakuwa ukivua watu wakiwa hai.” (Luka 5:10) Aina hiyo ya uvuvi inaendelea kufanywa leo katika nchi zaidi ya 230, kutia ndani Senegal. (Mathayo 24:14) Katika nchi hiyo “wavuvi [wa kisasa] wa watu” wanajulisha kwa ujasiri tumaini lao la Kikristo.—Mathayo 4:19.

Senegal iko kwenye ncha ya magharibi zaidi ya Afrika. Nchi hiyo inaanzia sehemu za jangwa la mchanga zinazopakana na Sahara upande wa kaskazini hadi misitu yenye mvua ya Casamance upande wa kusini. Senegal ni nchi ambayo hupata pepo kavu kutoka jangwani na vilevile pepo baridi na zenye kuburudisha kutoka Atlantiki. Nchi hiyo ina wakazi zaidi ya milioni tisa. Wakazi wa Senegal wanasifika kwa ukaribishaji-wageni. Wengi wao hawadai kuwa Wakristo. Wengi hufuga kondoo, huku wengine wakifuga ng’ombe, ngamia, na mbuzi. Pia kuna wakulima wanaokuza njugu, pamba, na mpunga. Naam, na kuna wavuvi, wanaoleta samaki wengi kutoka Bahari ya Atlantiki na kutoka mito mikubwa kadhaa inayopinda-pinda katika nchi hiyo. Biashara ya uvuvi huchangia sana uchumi wa Senegal. Kwa kweli, chakula maarufu cha taifa ni ceebu jën, mlo mtamu wa wali, samaki, na mboga.

“Wavuvi wa Watu”

Kuna wahubiri 863 wenye bidii wa Ufalme wa Mungu nchini Senegal. Uvuvi wa kiroho ulianza humo mwanzoni mwa miaka ya 1950. Ofisi ya tawi ya Watch Tower Society ilifunguliwa Dakar, jiji kuu, mwaka wa 1965. Mishonari waliokuwa “wavuvi” walianza kuwasili kutoka nchi nyingi za mbali. Kazi ya “kuvua” ikaanza, na kujulishwa kwa tumaini la Kikristo nchini Senegal kukaendelea hatua kwa hatua. Hatimaye, ofisi mpya ya tawi ilijengwa huko Almadies, viungani mwa jiji la Dakar, na kuwekwa wakfu kwa Yehova mnamo Juni 1999. Huo ulikuwa wakati wenye shangwe iliyoje!

Ugumu wa Kukubali Kweli

Watu wa malezi tofauti-tofauti sana wanahubiriwa kwa ukawaida, na baadhi yao wameitikia ifaavyo ujumbe wa tumaini unaopatikana katika Neno la Mungu. Japo wengi hawaijui Biblia, wanafurahi kujua kwamba ahadi ambazo Yehova Mungu aliwatolea manabii waaminifu wa kale zitatimizwa karibuni.

Mara nyingi inahitaji ujasiri kuchukua msimamo thabiti kwa ajili ya kanuni za Kikristo, hasa wakati mapokeo na desturi za familia zinapohusika. Kwa mfano, watu wengi Senegal huoa wake wengi. Fikiria kisa cha mtu ambaye alikuwa na wake wawili alipoanza kujifunza Biblia. Je, angekuwa na ujasiri wa kukubali kweli ya Kikristo na kuishi kulingana na takwa la Maandiko la kuwa mume wa mke mmoja? (1 Timotheo 3:2) Na je, angebaki tu na mke wa ujana wake, mwanamke aliyeoa kwanza? Hivyo ndivyo alivyofanya, na sasa anatumikia akiwa mzee mwenye bidii katika mojawapo ya makutaniko makubwa katika eneo la Dakar. Pia mke wake wa kwanza na watoto wote 12 wamekubali kweli, watoto 10 wa mke wa kwanza na watoto 2 wa aliyekuwa mke wake wa pili.

Huenda kizuizi kingine cha kukubali tumaini la Kikristo kikawa kutojua kusoma na kuandika. Je, hilo lamaanisha kwamba mtu asiyejua kusoma na kuandika hawezi kukubali kweli na kuishi kulingana nayo? Sivyo kamwe. Fikiria mfano wa Marie mwenye bidii ambaye ana watoto wanane. Aliona mara moja umuhimu wa kuzungumzia andiko la Biblia kila siku pamoja na watoto wake kabla hawajaondoka kwenda shuleni naye kwenda kazini. Lakini angefanyaje hivyo na hawezi kusoma? Mapema kila asubuhi, alichukua kijitabu Kuyachunguza Maandiko Kila Siku na kusimama kwenye barabara yenye mchanga mbele ya nyumba yake. Aliuliza watu waliokuwa wakipita kama wanaweza kusoma. Alipopata mtu awezaye kusoma, alimpa kijitabu hicho na kusema kwa unyofu: “Tafadhali unaweza kunisomea sehemu hii leo kwa kuwa sijui kusoma?” Alisikiliza kwa makini yaliyosomwa. Kisha alimshukuru mpita-njia huyo, akaingia upesi katika nyumba yake na kuzungumzia andiko hilo kwa uchangamfu pamoja na watoto wake kabla hawajaondoka kwenda shuleni!

Watu wa Namna Zote Waitikia

Nchini Senegal, watu wanaweza kupatikana wameketi barabarani wakiuza samaki, mboga, au wakiuza matunda sokoni au wameegama chini ya mbuyu mkubwa wakinywa ataya, chai ya kijani-kibichi iliyo chungu kidogo. Wakiwa wameazimia kuhubiria habari njema wote waliokutana nao, ndugu wawili walizungumza na mlemavu mmoja aliyekuwa akiombaomba barabarani. Baada ya kumsalimu, walisema: “Watu wengi hukupa fedha lakini hawasimami kuzungumza nawe. Sisi tumekuja kuzungumza nawe juu ya jambo muhimu sana linalohusu wakati wako ujao.” Mwombaji huyo akashangaa. “Tungependa kukuuliza swali,” ndugu huyo akaendelea kusema. “Unafikiri ni kwa nini kuna mateseko mengi hivi ulimwenguni?” “Ni mapenzi ya Mungu,” mwombaji huyo akajibu.

Kisha ndugu hao wakasababu naye kwa kutumia Maandiko na kufafanua Ufunuo 21:4. Mwombaji huyo aliguswa moyo sana na ujumbe huo wa tumaini na pia akaguswa moyo kwamba mtu fulani alipendezwa naye vya kutosha kuweza kusimama na kuzungumzia Biblia. Machozi yakamlengalenga. Badala ya kuomba fedha, akawasihi ndugu hao wachukue sarafu zote zilizokuwa katika mkebe wake wa kuombea fedha! Aliwasihi sana hivi kwamba jambo hilo lilivuta uangalifu wa watu waliokuwa wakipita. Japo ilikuwa vigumu sana, ndugu hao walimsadikisha asiwape fedha hizo. Hatimaye akakubali lakini akasisitiza kwamba wamtembelee tena.

Chuo kikuu kikubwa kilichoko Dakar pia kinaongezea samaki katika wavu wa kiroho wa kuvulia. Mwanafunzi mmoja humo aitwaye Jean-Louis aliyekuwa akisomea udaktari alianza kujifunza Biblia. Alikubali kweli upesi, akajiweka wakfu kwa Yehova, na kubatizwa. Alitamani kumtumikia Mungu wakati wote akiwa painia, lakini alipenda pia masomo yake ya udaktari. Kwa sababu ya mkataba aliokuwa amefanya na nchi yao, alilazimika kumaliza masomo yake. Lakini wakati huohuo akaanza kutumikia akiwa painia-msaidizi. Punde baada ya kupata diploma yake akiwa tabibu aliyehitimu, alialikwa kutumikia katika makao fulani makubwa ya Betheli barani Afrika akiwa daktari. Mwanamume mwingine kijana aliyehubiriwa kwenye Chuo Kikuu cha Dakar anatumikia pia pamoja na familia ya Betheli katika nchi yao.

Kwa kweli uvuvi wa kiroho nchini Senegal una matokeo. Vichapo vya Biblia vya Mashahidi wa Yehova vinathaminiwa sana na sasa vinatolewa katika lugha yao ya Kiwolof. Kusikia habari njema katika lugha yao wenyewe kumewatia moyo watu wengi wenye mioyo minyofu waitikie kwa shukrani. Kwa baraka za Yehova, yaelekea samaki wengi sana wa mfano watavuliwa, wakati “wavuvi [wenye bidii] wa watu” nchini Senegal wanapoendelea kujulisha tumaini la Kikristo kwa imani na ujasiri.

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 31]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

SENEGAL

[Picha]

Kujulisha tumaini la Kikristo nchini Senegal

[Picha zimeandalilwa na]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.