Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuna Uhitaji Mkubwa wa Faraja!

Kuna Uhitaji Mkubwa wa Faraja!

Kuna Uhitaji Mkubwa wa Faraja!

“Tazama, machozi yao waliodhulumiwa, ambao walikuwa hawana mfariji; na upande wa wale waliowadhulumu kulikuwa na uwezo, walakini wale walikuwa hawana mfariji.”—MHUBIRI 4:1.

JE, UNAHITAJI faraja? Je, unatamani sana kuliwazwa kidogo tu ili uondolewe huzuni nyingi? Je, unatamani sana kupata kitulizo kidogo tu cha kuboresha maisha yako yenye taabu nyingi na matukio mabaya?

Pindi moja au nyingine, sisi sote huhitaji sana faraja na kitia-moyo. Hii ni kwa sababu kuna mambo mengi sana maishani ambayo hutuhuzunisha. Sisi sote huhitaji makao, mavazi, na upendo. Wengine wetu wamezeeka na hawafurahii mambo hayo. Wengine wamevunjika moyo sana kwa sababu maisha hayajawa kama walivyotarajia. Wengine nao wameshtuliwa na ripoti wanayopata juu ya magonjwa yao.

Na zaidi, si watu wengi wawezao kudai kwamba matukio ya wakati wetu hayajatokeza uhitaji mkubwa wa faraja na tumaini. Katika karne iliyopita peke yake, vita vimesababisha vifo vya zaidi ya watu milioni mia moja. * Karibu wote waliacha familia zenye huzuni—mama na baba, dada na ndugu, wajane na mayatima—wakihitaji sana kitulizo. Leo, zaidi ya watu bilioni moja ni maskini hohehahe. Nusu ya watu ulimwenguni hawapati matibabu na dawa muhimu kwa ukawaida. Katika barabara za majiji makubwa, mamilioni ya watoto waliotupwa wanarandaranda, wengi wao wakitumia dawa za kulevya na kufanya ukahaba. Mamilioni ya wakimbizi wananyong’onyea katika kambi zenye kusikitisha sana.

Hata hivyo, idadi hizo—hata ziwe zenye kuhuzunisha namna gani—hazionyeshi uchungu na taabu ambazo watu wamepata maishani. Kwa mfano, ebu mfikirie Svetlana, msichana mmoja wa nchi za Balkan aliyezaliwa katika familia fukara. * “Ili tupate pesa,” yeye asema, “nilikuwa nikitumwa na wazazi wangu kuomba-omba au kuiba. Maisha ya familia yetu yaliharibika sana kiasi cha kwamba nilishikwa kinguvu na mtu wa jamaa yetu. Nilipata kazi ya kuhudumu katika hoteli, na mama yangu, ambaye alikuwa akipokea mshahara wangu, alisema kwamba atajiua nikipoteza kazi hiyo. Hayo yote yakanitumbukiza katika maisha ya ukahaba. Nilikuwa na umri wa miaka 13 tu wakati huo. Nikashika mimba na kuitoa. Nilipokuwa na umri wa miaka 15, ungalidhani nina umri wa miaka 30.”

Laimonis, kijana mmoja wa Latvia, ataja jinsi alivyohitaji faraja na ataja pia kumbukumbu mbaya zilizomhuzunisha sana. Akiwa na umri wa miaka 29, alipata aksidenti ya gari iliyofanya apooze tokea kiunoni hadi chini. Akakosa tumaini kabisa na kuingilia vileo. Miaka mitano baadaye akawa mlevi wa kupindukia—kiwete mlevi asiye na tumaini. Angepata faraja wapi?

Au mfikirie Angie. Mume wake alifanyiwa upasuaji wa ubongo mara tatu na mwanzoni upasuaji huo ulisababisha sehemu ya mwili wake ipooze kwa muda. Kisha, miaka mitano baada ya upasuaji wa mwisho kufanywa, akahusika katika aksidenti mbaya sana, akanusurika kifo. Mke wake alipoingia katika chumba cha wagonjwa mahututi na kumwona akiwa amelala bila fahamu kutokana na majeraha mabaya sana ya kichwa, akajua tu atapata msiba. Wakati wake ujao na wa familia yake ungekuwa mgumu. Angepataje utegemezo na kitia-moyo?

Siku moja ya kipupwe ilianza kama kawaida kwa Pat miaka kadhaa iliyopita. Hata hivyo, hawezi kukumbuka mambo yaliyotokea siku tatu zilizofuata. Baadaye mumewe alimwambia kwamba baada ya kushikwa na maumivu makali ya kifua, moyo wake uliacha kabisa kupiga. Moyo ulianza kupiga haraka-haraka sana na bila utaratibu, kisha ukaacha kabisa kupiga. Akaacha kupumua. “Moyo wangu na mapafu yangu vilikuwa vimeacha kufanya kazi,” asema Pat. Lakini kwa njia fulani akapona. Alisema hivi kuhusu muda mrefu aliokaa hospitalini: “Niliogopa sana kule kupimwa-pimwa mara nyingi, hasa walipojaribu kufanya moyo wangu upige-pige na kuacha, kama ulivyokuwa umefanya hapo awali.” Angepataje liwazo na kitulizo alizohitaji katika wakati huo mgumu?

Joe na Rebecca walifiwa na mwana wao mwenye umri wa miaka 19 katika aksidenti ya gari. “Hatujawahi kupata kihoro kama hicho,” wao wasema. “Ingawa katika nyakati zilizopita tumeomboleza pamoja na wengine wanapofiwa, hatukuhisi uchungu mwingi wa moyoni kama sasa.” Ni nini kiwezacho kutuliza “uchungu mwingi wa moyoni”—huzuni kubwa ya kufiwa na mtu umpendaye?

Watu hao wote, pamoja na mamilioni wengine, kwa kweli wamepata chanzo kikuu cha faraja na kitulizo. Ili uone jinsi wewe pia uwezavyo kunufaika na chanzo hicho, tafadhali endelea kusoma.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Idadi kamili ya wanajeshi na raia ambao wamekufa haijulikani vizuri. Kwa mfano, kitabu Facts About the American Wars cha 1998 chasema hivi kuhusu Vita ya Ulimwengu ya Pili pekee: “Habari nyingi zinataja kwamba jumla ya watu waliokufa kwa sababu ya Vita ya Ulimwengu ya Pili (wanajeshi na raia) ni milioni 50 lakini wengi ambao wamechunguza suala hilo vizuri wanaamini kwamba waliokufa ni wengi zaidi—maradufu ya idadi inayotajwa.”

^ fu. 6 Jina limebadilishwa.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

UNITED NATIONS/PHOTO BY J. K. ISAAC

UN PHOTO 146150 BY O. MONSEN