Mbona Kuna Ufisadi Mwingi Mno?
Mbona Kuna Ufisadi Mwingi Mno?
“Nawe usipokee rushwa; kwani hiyo rushwa huwapofusha macho hao waonao, na kuyapotoa maneno ya wenye haki.”—Kutoka 23:8.
MIAKA 3,500 iliyopita, Sheria ya Musa ililaani rushwa. Kwa karne nyingi tangu wakati huo, sheria nyingi za kupambana na ufisadi zimetungwa. Hata hivyo, sheria hazijafaulu kukomesha ufisadi. Mamilioni hupokea na kutoa rushwa kila siku, na hali hiyo husababisha mateso kwa mabilioni ya watu.
Ufisadi umeenea na kuwa tata sana hivi kwamba unatisha kuharibu misingi ya jamii. Katika nchi fulani haiwezekani kufanyiwa lolote bila kutoa rushwa. Wengine hutoa rushwa kwa watu wenye mamlaka ili kupita mtihani, kupata leseni ya kuendesha gari, kupata kandarasi, au kushinda kesi. “Ufisadi ni kama uchafuzi mkubwa unaovunja mioyo ya watu,” alalamika Arnaud Montebourg, mwanasheria mjini Paris.
Rushwa hasa imejaa katika biashara. Kampuni fulani hutenga theluthi moja ya faida zake ili kuwapa rushwa maofisa fisadi serikalini. Gazeti la Uingereza liitwalo The Economist lasema kwamba kufikia asilimia 10 ya dola bilioni 25 za Marekani zinazotumiwa kila mwaka katika mauzo ya silaha ulimwenguni hutumiwa kuwapa rushwa wale wanaotazamiwa kuzinunua. Kadiri ufisadi huu unavyoongezeka, ndivyo matokeo yake yanavyozidi kuwa mabaya. Katika kipindi cha miaka kumi iliyopita, yasemekana kuwa ubepari wenye ubaguzi, ambao ni shughuli za kibiashara zenye ufisadi zinazowapendelea matajiri wachache walio na mahusiano bora ya kibiashara, umeangamiza uchumi wa nchi mbalimbali.
Bila shaka maskini—ambao mara nyingi hawana uwezo wa kumpa yeyote rushwa—ndio wanaoteseka zaidi kutokana na ufisadi na kuharibika kwa uchumi kunakoletwa na ufisadi. Kama gazeti la The Economist lilivyosema waziwazi, “ufisadi ni aina moja tu ya uonevu.” Je, uonevu wa aina hiyo waweza kushindwa, au ufisadi hauwezi kuepukwa? Ili kujibu swali hilo, lazima kwanza tutambue baadhi ya visababishi vikuu vya ufisadi.
Ni Nini Kinachosababisha Ufisadi?
Kwa nini watu huamua kuwa mafisadi badala ya kufuata haki? Kwa wengine, huenda ikawa kwamba ufisadi ndio njia rahisi zaidi—au njia pekee kabisa—ya kupata wanachotaka. Wakati mwingine, huenda rushwa ikawa njia rahisi ya kuepuka adhabu. Wengi wanapoona kuwa wanasiasa, polisi, na mahakimu wanapuuza ufisadi au hata wao wenyewe ni mafisadi, hufuata tu mfano wao.
Ufisadi hupata kukubaliwa zaidi na hatimaye kuwa jambo la kawaida maishani kadiri uongezekavyo. Watu wanaolipwa mshahara Mhubiri 8:11.
mdogo sana huona kwamba ni lazima wakubali rushwa. Inawabidi wadai rushwa ili waishi maisha bora. Na itukiapo kwamba wale wanaotoza rushwa au wanaoitoa ili kupata mapendeleo isivyo haki hawaadhibiwi, basi watu wachache huwa na nia ya kupambana na ufisadi. “Kwa sababu hukumu juu ya tendo baya haitekelezwi upesi, mioyo ya wanadamu huthibitishwa ndani yao ili kutenda mabaya,” akasema Mfalme Solomoni.—Kuna mambo makuu mawili ambayo huendeleza ufisadi: ubinafsi na pupa. Kwa sababu ya ubinafsi, mafisadi hupuuza mateso ambayo ufisadi wao huletea wengine, nao hutetea rushwa kwa sababu tu inawanufaisha. Kadiri mafisadi hao wanavyokusanya mali, ndivyo wanavyozidi kuwa wenye pupa. “Apendaye fedha hatashiba fedha,” akasema Solomoni, “wala apendaye wingi hatashiba nyongeza.” (Mhubiri 5:10) Ni kweli huenda pupa ikamwezesha mtu kuchuma pesa, lakini sikuzote pupa huchochea ufisadi na uvunjaji wa sheria.
Jambo jingine lisilopasa kusahauliwa ni fungu la mtawala asiyeonekana wa ulimwengu huu, ambaye Biblia humtambulisha kuwa Shetani Ibilisi. (1 Yohana 5:19; Ufunuo 12:9) Shetani huchochea sana ufisadi. Rushwa kubwa zaidi kupita zote ni ile ambayo Shetani alitaka kumpa Kristo. ‘Nitakupa falme zote za ulimwengu ukianguka chini na kunifanyia tendo la ibada.’—Mathayo 4:8, 9.
Hata hivyo, Yesu hakuwa fisadi kamwe, naye aliwafundisha wafuasi wake wamwige. Je, mafundisho ya Yesu yaweza kuwa chombo bora cha kupambana na ufisadi leo? Makala yafuatayo yatachunguza swali hilo.