Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Gospeli—Mjadala Wake Waendelea

Gospeli—Mjadala Wake Waendelea

Gospeli—Mjadala Wake Waendelea

Je, yale masimulizi ya Gospeli yanayohusu kuzaliwa kwa Yesu Kristo ni ya kweli?

Je, alitoa yale Mahubiri ya Mlimani?

Je, kweli Yesu alifufuliwa?

Je, kweli alisema:“Mimi ndiyo njia na kweli na uhai”?—YOHANA 14:6.

MASUALA kama hayo yamejadiliwa na wasomi wapatao 80 kwenye Semina Juu ya Yesu, ambayo imekuwa ikifanywa mara mbili kwa mwaka tangu mwaka wa 1985. Kikundi hicho cha wasomi kimejibu maswali kama hayo kwa njia isiyo ya kawaida. Washiriki wa semina hiyo wamepigia kura kila jambo linalosemekana kwamba lilitajwa na Yesu katika Gospeli. Kura nyekundu inaonyesha kwamba kwa kweli Yesu alisema jambo hilo. Kura ya pinki inamaanisha kwamba usemi unaotajwa wafanana na jambo ambalo huenda Yesu alisema. Kura ya kijivu yaonyesha kwamba huenda mambo yaliyotajwa yakakaribia kufanana na maneno ya Yesu, lakini si yeye aliyeyasema. Kura nyeusi ni ya kupinga kabisa, ikionyesha kwamba usemi huo ulitokana na mapokeo ya baadaye.

Wakifuata utaratibu huo, washiriki wa hiyo Semina Juu ya Yesu wamepinga yale mambo manne ambayo yametajwa kwa njia ya maswali mwanzoni mwa makala hii. Hata wamepiga kura nyeusi ya kupinga asilimia 82 ya maneno yanayosemekana kuwa yalisemwa na Yesu katika Gospeli. Kwa maoni yao, asilimia 16 tu ya matukio yaliyosimuliwa kuhusu Yesu katika Gospeli na maandishi mengine ndiyo yanayoonekana kuwa asilia.

Kuchambua Gospeli kwa njia hiyo si jambo jipya. Mwaka wa 1774 Gospeli zilishambuliwa wakati hati yenye kurasa 1,400 ya Hermann Reimarus, aliyekuwa profesa wa lugha za Mashariki kule Hamburg, Ujerumani, ilipochapishwa baada ya kifo chake. Katika hati hiyo, Reimarus alitilia shaka sana usahihi wa Gospeli. Uamuzi wake ulitegemea uchunguzi aliofanyia lugha iliyotumiwa katika Gospeli na pia mambo yanayoonekana kana kwamba yanapingana katika masimulizi manne ya Gospeli juu ya maisha ya Yesu. Tangu wakati huo, mara nyingi wachambuzi wametilia shaka uasilia wa Gospeli, na kwa kadiri fulani wamedhoofisha imani ya watu katika maandishi hayo.

Wasomi hao wanakubaliana kwa ujumla kwamba masimulizi ya Gospeli ni hekaya za kidini ambazo zimewasilishwa na watu tofauti-tofauti. Maswali ambayo kwa kawaida huulizwa na hao wasomi wenye kutilia shaka ni kama yafuatayo: Je, yawezekana kwamba itikadi za watu hao ziliwafanya waandikaji wa zile Gospeli nne watilie chumvi mambo ya hakika? Je, ushindani uliokuwapo miongoni mwa Wakristo wa mapema uliwafanya warekebishe masimulizi ya Yesu au kuyatilia chumvi? Ni sehemu zipi za Gospeli ambazo yaelekea zimeripotiwa kwa usahihi na ambazo si hekaya?

Watu waliolelewa katika jamii ambayo haiamini kuwapo kwa Mungu au katika jamii inayofuatia mambo ya ulimwengu wanaamini kwamba Biblia—kutia ndani zile Gospeli—ni kitabu kilichojaa hekaya tu. Wengine nao wamechukizwa sana na umwagikaji wa damu, uonevu, migawanyiko, na mwenendo mpotovu, mambo ambayo yamefanyika katika historia ya Jumuiya ya Wakristo. Watu hao hawaoni sababu yoyote kamwe ya kusikiliza yale maandishi yaonwayo kuwa matakatifu katika Jumuiya ya Wakristo. Wanahisi kwamba vitabu ambavyo vimetokeza dini yenye unafiki ni hekaya tupu.

Wewe unaonaje? Je, uwaache wasomi fulani wanaotilia shaka usahihi wa Gospeli wakuzushie shaka kama hizo akilini mwako? Unaposikia taarifa zinazodai eti waandikaji wa Gospeli walitunga hekaya, je, uache jambo hilo livunje imani yako katika maandishi hayo? Je, rekodi mbaya ya Jumuiya ya Wakristo ikufanye utilie shaka usahihi wa zile Gospeli? Twakuomba uchunguze baadhi ya mambo ya hakika.

[Picha katika ukurasa wa 4]

Je, Gospeli ni hekaya tu au mambo ya hakika?

[Hisani]

Jesus Walking on the Sea/The Doré Bible Illustrations/Dover Publications

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Mandhari ya nyuma, ukurasa wa 3-5 na 8: Courtesy of the Freer Gallery of Art, Smithsonian Institution, Washington, D.C.