Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kazi ya Kuokoa Kisiwani Robinson Crusoe

Kazi ya Kuokoa Kisiwani Robinson Crusoe

Kazi ya Kuokoa Kisiwani Robinson Crusoe

ROBINSON CRUSOE ni kimojawapo cha visiwa vitatu katika Bahari ya Pasifiki vinavyoitwa Juan Fernández, vilivyo kilometa 640 kutoka pwani ya Chile. * Kisiwa hicho chenye mraba wa kilometa 93 kilipewa jina hilo kutokana na riwaya inayojulikana sana iitwayo Robinson Crusoe iliyoandikwa na Mwingereza Daniel Defoe katika karne ya 18. Kwa ujumla riwaya hiyo ni matukio ya maisha ya Mskoti aitwaye Alexander Selkirk, aliyeishi katika kisiwa hicho kwa muda wa miaka minne hivi.

Sehemu ya maandishi kwenye ubao kisiwani yasema: “Hapa ndipo, siku baada ya siku kwa muda wa miaka minne, baharia Mskoti aitwaye Alexander Selkirk, alitazama upeo wa macho akiwa na wasiwasi, akiingojea meli ambayo ingemwokoa.” Hatimaye, Selkirk alipookolewa na kurudishwa kwao, alirudia ulimwengu usiomridhisha tena baada ya kuishi katika paradiso yake ndogo. Inasemekana kwamba alisema hivi baadaye: “Kisiwa changu kipenzi! Ninajuta kwamba nilikuacha!”

Baadaye, kisiwa hicho kikawa mahali pa kuadhibia watu, kikikaliwa na baadhi ya wale ambao walikuwa “wameasi imani” ya Kanisa Katoliki. Hali kisiwani ikawa tofauti sana na hali ya kiparadiso ambayo Selkirk alikuwa amezoea! Hata hivyo, wakazi wa siku hizi wa kisiwa hicho wanafurahia amani na utulivu zisizo za kawaida sehemu nyingine ulimwenguni. Maisha kisiwani, sawa na desturi za visiwa vingi, ni yenye utulivu na ni rahisi kuanzisha mazungumzo na karibu kila mtu.

Idadi rasmi ya wakazi wa kisiwa cha Robinson Crusoe ni 500 hivi, hata hivyo, ni watu 400 pekee wakaao humo mwaka mzima. Sababu moja ni kwamba baadhi ya akina mama na watoto wao hukaa barani Chile shule zinapofunguliwa, huku wakirudi tu kisiwani shule zinapofungwa ili wawe pamoja na familia nzima.

Ijapokuwa kuna mazingira mazuri ya kibustani katika kisiwa cha Robinson Crusoe, baadhi ya wakazi hawajaridhishwa kiroho nao watafuta majibu kwa maswali yao. Wengine wamehisi kana kwamba wanahitaji kuokolewa kiroho.

Kazi ya Kuokoa ya Kiroho

Kazi ya kuokoa ya kiroho ilianza mnamo 1979. Mwanamke mmoja aliyekuwa anajifunza Biblia pamoja na Mashahidi wa Yehova kule Santiago, Chile, alihamia kisiwani, akaanza kufundisha wengine juu ya yale aliyokuwa amejifunza. Baada ya muda, mzee wa kutaniko moja aliyetembelea kisiwa hicho kwa sababu ya kazi alishangaa kupata kikundi kidogo cha wanafunzi wa Biblia waliokuwa wakisaidiwa na mwanamke huyo kufanya maendeleo ya kiroho. Aliporudi tena baada ya miezi mitatu, yule mwalimu wa Biblia na wanafunzi wake wawili walistahili kubatizwa. Basi, mzee huyo alisimamia ubatizo wao. Hatimaye, Mkristo mmoja wa wale wapya waliobatizwa akaolewa, naye pamoja na mume wake, wakaendelea kutafuta wengine waliohitaji kuokolewa kiroho. Mume wake alisimamia ujenzi wa Jumba la Ufalme dogo ambalo bado latumiwa na kile kikundi kidogo katika kisiwa hicho. Hatimaye, kwa sababu ya hali za kiuchumi wakahama Robinson Crusoe na kuhamia kutaniko lililoko katikati ya Chile, ambako wanaendelea kumtumikia Yehova kwa bidii.

Pole pole, kikundi hicho kidogo kisiwani kiliongezeka wengine walipookolewa kutoka dini za uwongo. Hata hivyo, kwa kuwa ni lazima wanafunzi wahamie barani kwa ajili ya shule ya sekondari, kikundi hicho kilipunguka na wakabaki kisiwani dada wawili waliobatizwa kutia ndani msichana mmoja mchanga. Kikundi hicho huongezeka shule zinapofungwa wakati ambapo baadhi ya akina mama hurudi kisiwani. Jambo hilo latia nguvu wale Wakristo watatu wanaobaki humo mwaka mzima. Kwa sababu ya kazi ya bidii ya dada hao, Mashahidi wa Yehova wajulikana sana Robinson Crusoe. Baadhi ya wakazi wa kisiwa hicho wamepinga kazi yao na kujaribu kuwashurutisha wengine wasikubali habari za Ufalme. Hata hivyo, mbegu za kweli ya Biblia ambazo zimepandwa katika mioyo minyofu zaendelea kumea.

Kuwaimarisha Wale Waliookolewa

Mara moja kwa mwaka mwangalizi asafiriye hutembelea kisiwa hicho. Vipi kutembelea Mashahidi wachache katika kisiwa cha mbali? Mwangalizi mmoja wa mzunguko anaeleza hivi juu ya ziara yake ya kwanza kisiwani Robinson Crusoe:

“Safari hiyo ilikuwa nzuri ajabu. Safari ilianza saa moja asubuhi tulipotoka Valparaiso kwenda Uwanja wa Ndege wa Santiago uitwao Cerrillos. Tulipanda ndege ndogo inayoweza kubeba watu saba. Baada ya kusafiri kwa muda wa saa 2 na dakika 45, tulikiona kwa mbali kilele cha mlima kilichotokeza juu ya mawingu. Tulipokaribia tukakiona kisiwa—mwamba mkubwa katikati ya bahari. Ilionekana kana kwamba kinaelea juu ya maji, kama meli iliyopotea baharini.

“Baada ya kutua, mashua ilitusafirisha kijijini. Huku na huku, miamba itokezayo kutoka baharini yafanyiza visiwa vidogo-vidogo watuapo sili waitwao Juan Fernández fur seal. Hairuhusiwi kuwavua sili hao wenye manyoya kwa kuwa ni wachache sana wanaobaki. Ghafula, kitu fulani kiliruka kando ya mashua na kupotea tena baharini. Kumbe ni samaki arukaye aliye na mapezi yenye mikunjo yanayofanana na mabawa. Ni kana kwamba alifurahia kuruka kutoka majini na kula wadudu. Bila shaka, mara kwa mara alaye wengine pia huliwa; huenda kuruka kwake kwaweza kuwavutia wawindaji wengine walio tayari kummeza anapoanguka majini.

“Hatimaye, tukawasili kijiji cha San Juan Bautista (Mtakatifu Yohana Mbatizaji). Wakazi wengi waliokuwapo gatini ama waliwangojea wageni wao ama walitaka tu kujua ni nani waliokuja wakati huo. Tulivutiwa na mandhari nzuri ajabu—tuliuona mlima mkubwa wenye kilele cha mawemawe uitwao El Yunque (Fuawe), uliotandazwa kana kwamba kwa mahameli ya rangi nzito ya kijani, na nyuma ya mlima kulikuwa na anga ya buluu na mawingu meupe mengi.

“Mara tuliwatambua dada zetu Wakristo na watoto wao waliotungojea gatini. Shule zilikuwa zimefungwa, kwa hivyo kikundi hicho kilikuwa kikubwa kuliko kawaida. Baada ya kusalimiana kwa uchangamfu, tukapelekwa kwenye nyumba ndogo nzuri sana ambamo tulikaa kwa juma moja.

“Juma hili lilikuwa la pekee sana, nasi tukatambua kwamba lingepita haraka. Tungehitaji kutumia wakati wetu vizuri. Siku iyo hiyo, baada tu ya chakula cha mchana, tukamtembelea mwanafunzi wa Biblia ambaye karibuni angekuwa dada yetu wa kiroho na mshiriki wa paradiso ya kiroho ya Mungu. Alitabasamu kwa furaha lakini alikuwa na wasiwasi pia. Hivi karibuni angefikia mradi wake wa ubatizo ambao alikuwa ametarajia kwa muda mrefu. Tulizungumzia habari ya lazima naye ili aweze kustahili kuwa mhubiri wa habari njema. Kesho yake, alishiriki katika kazi ya kuhubiri kwa mara ya kwanza. Siku ya tatu tukaanza kupitia matakwa ya ubatizo pamoja naye. Kabla ya juma kwisha akabatizwa.

“Wengi walihudhuria mikutano ya juma hilo, na kilele cha hudhurio kilikuwa watu 14. Kila siku kulikuwako mipango ya utumishi wa shambani, ziara za kurudia, mafunzo ya Biblia, na ziara za uchungaji. Hayo yote yaliwatia moyo kama nini dada hao wanaoendelea na utendaji wao peke yao mwaka mzima!”

Imekuwa vigumu sana kwa wanaume kisiwani kukubali ujumbe wa kweli, huenda ikawa kazi yao ngumu ndiyo inayowazuia wasiitikie. Kazi kuu kisiwani ni ya kuvua kamba-mti, nayo inahitaji mtu kujitolea kabisa. Wengi wanakataa ujumbe kwa sababu ya upendeleo. Hata hivyo, tunatumaini kwamba siku zijazo wakazi wengi zaidi wa kisiwani wataitikia, wanaume kwa wanawake.

Kufikia leo, watu kumi wameokolewa kiroho kisiwani kwa kujua kweli na makusudi ya Yehova Mungu. Kwa sababu mbalimbali, baadhi yao wamekihama kisiwa hicho. Lakini, ikiwa wabaki ama la, kuokolewa kwao kiroho kumekuwa muhimu zaidi kuliko kuokolewa kwa Alexander Selkirk. Kwa sasa, wanafurahia paradiso ya kiroho popote pale walipo. Dada na watoto wao ambao bado wanaishi kisiwani wanafurahia mazingira ya kibustani, lakini zaidi ya hiyo, wanalo tumaini la kuishi wakati dunia nzima itakapokuwa paradiso halisi.

Kazi ya Kuokoa Yaendelea

Kikundi hicho kidogo cha Mashahidi wa Yehova kisiwani Robinson Crusoe, kinakaa mbali na ndugu na dada zao Wakristo. Hata hivyo, hawaoni kuwa wameachwa kabisa, kama alivyoona yule Mskoti aitwaye Selkirk. Kupitia vitabu vingi vya kitheokrasi, vidio za mikusanyiko na makusanyiko wanazopokea kutoka kwenye ofisi ya tawi ya Chile ya Watch Tower Society mara tatu kila mwaka, nayo ziara ya mwangalizi wa mzunguko mara moja kwa mwaka, wao huendelea kudumisha uhusiano wa karibu na tengenezo la Yehova. Hivyo, wanaendelea kuwa washiriki wenye kutenda miongoni mwa ‘ushirika mzima wa ndugu katika ulimwengu.’—1 Petro 5:9.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Jina rasmi la kisiwa hicho ni Más a Tierra.

[Ramani/Picha katika ukurasa wa 9]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

CHILE

Santiago

KISIWA CHA ROBINSON CRUSOE

San Juan Bautista

El Yunque

BAHARI YA PASIFIKI

KISIWA CHA SANTA CLARA

[Picha]

El Yunque (Fuawe), mlima wenye fahari wenye kilele cha mawemawe

[Hisani]

Ramani ya Chile: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 8, 9]

Ukaribiapo kisiwa, waweza kuuona mwamba mkubwa katikati ya bahari

[Picha katika ukurasa wa 9]

Kijiji cha San Juan Bautista (Mtakatifu Yohana Mbatizaji)

[Picha katika ukurasa wa 9]

Visiwa vidogo watuliapo sili wenye manyoya na “sea lion”

[Picha katika ukurasa wa 10]

Tulisafiri kwa ndege ndogo kutoka Santiago, Chile

[Picha katika ukurasa wa 10]

Pwani yenye miamba ya Kisiwa cha Robinson Crusoe

[Picha katika ukurasa wa 10]

Jumba la Ufalme dogo kisiwani