Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mchukua-Nuru kwa Mataifa Mengi

Mchukua-Nuru kwa Mataifa Mengi

Simulizi la Maisha

Mchukua-Nuru kwa Mataifa Mengi

SIMULIZI JUU YA GEORGE YOUNG KAMA ILIVYOSIMULIWA NA RUTH YOUNG NICHOLSON

“Mbona makasisi wako kimya jinsi hii? . . . Tunapaswa kuwa watu wa aina gani ikiwa baada ya kuthibitisha kwamba mambo ninayoandika ni ya kweli tunakaa kimya? Tusiwaache watu gizani, badala yake tuwatangazie kweli bila radhi wala kuficha.”

MANENO hayo ni sehemu ya barua yenye kurasa 33 iliyoandikwa na Baba yangu akiomba jina lake liondolewe kwenye orodha ya wafuasi wa kanisa. Hilo lilitukia mwaka wa 1913. Tokea wakati huo na kuendelea alianza maisha yenye shughuli nyingi akitumikia akiwa mchukua-nuru kwa mataifa mengi. (Wafilipi 2:15) Tangu nilipokuwa msichana mdogo, nilikuwa nikikusanya habari kuhusu maisha ya Baba yangu kutoka kwa watu wa ukoo na katika mambo yaliyoandikwa juu yake, na rafiki wakanisaidia kuunganisha habari yote ya maisha yake. Maisha ya Baba yangu hunikumbusha sana maisha ya mtume Paulo. Kama huyo “mtume kwa mataifa,” Baba alikuwa tayari kwenda katika kila nchi na kisiwa kutangazia watu ujumbe wa Yehova. (Waroma 11:13; Zaburi 107:1-3) Ebu sasa niwaambie habari ya Baba yangu, George Young.

Miaka ya Mapema

Baba alikuwa mwana wa mwisho wa John na Margaret Young, nao walikuwa wafuasi wa kanisa la Presbiteri la Scotland. Alizaliwa Septemba 8, 1886, punde tu baada ya familia hiyo kuhama kutoka Edinburgh, Scotland na kwenda British Columbia, magharibi mwa Kanada. Ndugu zake wakubwa watatu —Alexander, John, na Malcom —walizaliwa huko Scotland miaka michache awali. Marion, dada yao mdogo, ambaye walizoea kumwita Nellie, alizaliwa miaka miwili baada ya Baba yangu.

Watoto hao walikuwa wenye furaha walipokuwa wakikua katika shamba moja katika Saanich, karibu na mji wa Victoria ulio katika jimbo la British Columbia. Kwa wakati uo huo walizoezwa kuwa wenye bidii katika mambo yote. Hivyo wazazi wao waliporejea kutoka safari zao za mjini Victoria, wangepata kazi zote za nje zimefanywa na nyumba ni safi.

Baadaye, Baba na ndugu zake walianza biashara ya migodi na mbao. Vijana hao walijulikana sana kwa ustadi wao wa kukagua eneo linaloweza kutokeza mbao na pia walikuwa wafanyabiashara wa mbao. Baba alishughulikia mambo ya fedha.

Hatimaye, upendo wake Baba kwa mambo ya kiroho ulimfanya aamue kuwa mhudumu wa kanisa la Presbiteri. Hata hivyo, karibu na wakati huo, hotuba zilizochapishwa magazetini za aliyekuwa msimamizi wa kwanza wa Zion’s Watch Tower Tract Society, Charles Taze Russell, ziliathiri sana maisha yake. Aliyojifunza kutokana na hotuba hizo ilimsukuma Baba kuandika barua iliyotajwa hapo mwanzoni.

Kwa fadhili lakini kwa njia ya wazi sana, Baba alitumia mistari ya Biblia kukanusha mafundisho ya kanisa kwamba nafsi za binadamu hazifi na kwamba Mungu atazitesa nafsi milele na milele katika moto wa helo. Pia, alilifunua fundisho la utatu kuwa la uwongo na kuthibitisha kuwa halitokani na Ukristo na halina msingi wowote wa Kimaandiko. Kutoka wakati huo na kuendelea Baba akimwiga Yesu, alifuatia huduma ya Kikristo akitumia uwezo wake na nguvu zake zote kumtukuza Yehova.

Katika mwaka wa 1917, chini ya mwelekezo wa Watch Tower Society, Baba alianza kutumikia akiwa pilgrimu, kama walivyojulikana wawakilishi wasafirio wa Mashahidi wa Yehova wa wakati huo. Alitembelea miji na majiji kotekote Kanada akitoa hotuba na kuonyesha sinema inayoitwa “Photo-Drama of Creation.” Majumba yalikuwa yakifurika na watu wakati wa ziara zake. Ratiba ya ziara zake ilichapishwa katika Mnara wa Mlinzi hadi mwaka wa 1921.

Gazeti moja la habari la huko Winnipeg liliripoti kwamba Mweneza-evanjeli Young alihutubia watu 2,500 na wengine wengi walishindwa kuingia kwa sababu jumba lilijaa pomoni. Katika Ottawa, alitoa hotuba yenye kichwa “Kwenda Helo na Kurudi.” Kuhusu pindi hiyo mtu mmoja mzee alitoa ripoti ifuatayo: “Baada ya kumaliza hotuba yake, George Young aliwaalika kwenye jukwaa makasisi walioketi kwenye safu ili wajadili habari hiyo pamoja naye, lakini hakuna hata mmoja wao aliyethubutu kufanya hivyo. Ndipo nikafahamu nimeipata kweli.”

Baba alijaribu kutimiza mambo mengi ya kiroho kwa kadiri alivyoweza katika ziara zake za pilgrimi. Baadaye ilimbidi akimbilie gari-moshi asafiri nalo hadi eneo linalofuata katika ratiba yake. Alipotumia gari kwenda kwa mgawo unaofuata, mara nyingi alianza safari yake asubuhi na mapema kabla ya wakati wa kiamsha kinywa. Mbali na kuwa mtu mwenye bidii, Baba alijulikana kuwa mtu mwenye huruma, mwenye matendo mema ya Kikristo na mkarimu.

Miongoni mwa mikusanyiko mingi ya mapema aliyohudhuria, wenye kukumbukwa sana ni ule wa mwaka wa 1918 uliofanyika katika mji wa Edmonton, Alberta. Washiriki wote wa familia yake walikuwepo kushuhudia kubatizwa kwa Nellie. Hii ilikuwa mara ya mwisho kwa Baba na ndugu zake kuwa pamoja. Miaka miwili baadaye, Malcolm aliugua nimonia kisha akafa. Malcolm alikuwa na tumaini la kwenda mbinguni, tumaini walilokuwa nalo ndugu zake watatu na baba yao, na wote walidumu wakiwa waaminifu hadi kifo chao.—Wafilipi 3:14.

Kwenda Kwenye Maeneo ya Kigeni

Baada ya Baba kumaliza kuhubiri katika Kanada Septemba 1921, aliagizwa na aliyekuwa msimamizi wa Watch Tower Society, Joseph F. Rutherford, azuru visiwa vya Karibea. Baba alionyesha ile sinema ya “Photo-Drama of Creation,” na kila mahali watu walipendezwa sana nayo. Akiwa Trinidad aliandika hivi: “Ukumbi ulijaa sana, na wengi walizuiliwa wasiingie. Usiku uliofuata jengo lilisongamana watu.”

Kisha, mwaka wa 1923 baba alipewa mgawo kwenda Brazili. Huko alikuwa akihutubia wasikilizaji wengi, na nyakati nyingine aliwatumia wafasiri wa kulipwa. Mnara wa Mlinzi la Desemba 15, 1923, lilisema hivi: “Kuanzia Juni 1 hadi Septemba 30 Ndugu Young alifanya mikutano 21 ya hadhara iliyohudhuriwa na watu 3,600; na mikutano 48 ya kutaniko iliyohudhuriwa na watu 1,100; akatoa vichapo vya lugha ya Kireno vipatavyo 5,000 bila malipo.” Watu wengi walionyesha kupendezwa Baba alipowatolea habari yenye kichwa “Mamilioni Wanaoishi Sasa Hawatakufa Kamwe.”

Majengo mapya yalipowekwa wakfu nchini Brazili mnamo Machi 8, 1997, broshua iliyotayarishwa kwa ajili ya wakfu huo ilitoa ripoti hii: “1923: George Young awasili Brazili. Afungua ofisi ya tawi katikati ya mji wa Rio de Janeiro.” Ijapokuwa vichapo vya Biblia vilipatikana katika Kihispania, kulikuwepo uhitaji wa vichapo hivyo katika Kireno, ambayo ndiyo lugha inayosemwa na wengi Brazili. Hivyo, kuanzia Oktoba 1, 1923, Mnara wa Mlinzi lilianza kuchapishwa katika Kireno.

Baba alikutana na watu muhimu katika Brazili. Mmoja wao ni Mreno mmoja tajiri aitwaye Jacintho Pimentel Cabral, ambaye alitoa makao yake yatumiwe kwa ajili ya mikutano. Punde si punde Jacintho alikubali kweli ya Biblia na baadaye akawa mshiriki wa ofisi ya tawi. Mwingine alikuwa kijana Mreno aitwaye Manuel da Silva Jordão, aliyekuwa mtunza-bustani. Alisikiliza hotuba moja iliyotolewa na Baba, akachochewa kurudi kwao Ureno akatumikie akiwa kolpota, kama wahudumu wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo.

Baba alisafiri kotekote Brazili kwa gari-moshi na aliweza kupata watu wenye kupendezwa. Kwenye mojawapo ya safari zake alikutana na Bony Green na mkewe Catarina, akakaa kwao kwa majuma mawili hivi akiwafundisha Maandiko. Angalau watu saba wa familia hiyo walionyesha kujitoa kwao kwa Yehova kwa ubatizo wa maji.

Mwingine aliyepatikana ni Sarah Bellona Ferguson katika mwaka wa 1923. Akiwa msichana mdogo mwaka wa 1867, yeye, ndugu yake Erasmus Fulton Smith, pamoja na washiriki wengine wa familia yao walihamia Brazili kutoka Marekani. Tangu mwaka wa 1899 alikuwa akiyapokea kwa ukawaida magazeti ya Mnara wa Mlinzi kwa njia ya posta. Kuwasili kwa Baba kuliwapa Sarah, watoto wake wanne, na mwingine ambaye Baba alimwita Shangazi Sallie fursa waliyongojea kwa muda mrefu ya kubatizwa. Walibatizwa Machi 11, 1924.

Muda mfupi baadaye, Baba alikuwa akihubiri katika nchi nyinginezo katika Amerika Kusini. Mnamo Novemba 8, 1924, aliandika hivi akiwa Peru: “Ndipo tu nimemaliza kugawanya trakti 17,000 katika miji ya Lima na Callao.” Halafu akaondoka kwenda Bolivia ili aweze kugawanya trakti huko pia. Kuhusu ziara hiyo, aliandika hivi: “Baba yetu anabariki jitihada. Mtu mwenye asili ya Kihindi amenisaidia. Yeye anaishi kwenye chanzo cha Mto Amazon. Anarudi kwao akiwa na trakti 1,000 na pamoja na vitabu fulani.”

Kupitia jitihada za Baba yangu, mbegu za kweli ya Biblia zilienea katika nchi nyingi za Amerika Kusini na Kati. Mnara wa Mlinzi la Desemba 1, 1924 lilitoa ripoti hii: “George Young amekuwa sasa Amerika Kusini kwa muda unaozidi miaka miwili. . . . Limekuwa pendeleo kwa Ndugu huyu mpendwa kupeleka kweli hadi Punta Arenas, katika Mlango-Bahari wa Magellan.” Baba pia aliongoza kazi ya kuhubiri katika nchi za Kosta Rika, Panama, na Venezuela. Alisonga mbele tu na kazi ingawa alikuwa akiugua malaria na afya yake kudhoofika.

Kisha Ulaya

Katika Machi 1925, Baba aliondoka kwa meli kwenda Ulaya, na alitumaini kugawanya trakti 300,000 za Biblia katika Hispania na Ureno na pia kufanya mpango huko ili Ndugu Rutherford atoe hotuba kwa umma. Lakini, alipowasili Hispania, Baba alishuku uwezekano wa Ndugu Rutherford kuja kuhutubu huko kwa sababu ya hali iliyokuwapo ya kutovumilia dini.

Katika jibu lake, Ndugu Rutherford, akinukuu Isaya 51:16 aliandika hivi: “Nami nimetia maneno yangu kinywani mwako, nami nimekusitiri katika kivuli cha mkono wangu, ili nizipande mbingu, na kuiweka misingi ya dunia, na kuuambia Sayuni, Ninyi ni watu wangu.” Baada ya kusoma hayo Baba akafikia mkataa huu: “Hakika ni mapenzi ya Bwana niendelee na kuacha mambo mikononi mwake.”

Katika Mei 10, 1925, Ndugu Rutherford alihutubia watu akitumia mfasiri katika ukumbi wa Novedades Theater mjini Barcelona. Zaidi ya watu 2,000 walihudhuria, kutia ndani ofisa mmoja wa serikali na mlinzi maalumu kwenye jukwaa. Utaratibu uo huo ulifuatwa huko Madrid kukiwa na wahudhuriaji 1,200. Upendezi uliotokezwa na hotuba hizo ulifanya ofisi ya tawi ifunguliwe nchini Hispania na kama 1978 Yearbook of Jehovah’s Witnesses kinavyotaja ofisi hiyo “ilisimamiwa na George Young.”

Mei 13, 1925, Ndugu Rutherford alihutubu mjini Lisbon, Ureno. Ziara hiyo ilifanikiwa sana ijapokuwa makasisi walijaribu kuvuruga mkutano kwa kupiga kelele na kuharibu viti. Baada ya hotuba za Ndugu Rutherford huko Hispania na Ureno, Baba aliendelea kuonyesha ile sinema ya “Photo-Drama of Creation” na kufanya mpango wa kuchapishwa na kutolewa kwa vichapo vya Biblia katika sehemu hizo. Mwaka wa 1927 aliripoti kwamba habari njema “imetangazwa katika majiji yote na miji yote nchini Hispania.”

Kuhubiri Katika Muungano wa Sovieti

Muungano wa Sovieti ukawa mgawo mpya wa mishonari wa Baba na alifika huko Agosti 28, 1928. Barua yake ya Oktoba 10, 1928 inasema hivi kwa sehemu:

“Tangu nifike Urusi, kwa kweli naweza kusali hivi kwa moyo wangu wote, ‘Ufalme wako uje.’ Najifunza lugha yao, lakini nafanya maendeleo polepole. Mfasiri wangu ni mtu wa pekee sana na ingawa yeye ni Myahudi, amwamini Yesu na anaipenda Biblia. Nimeona mambo mengi yenye kupendeza lakini sijui nitaruhusiwa kukaa hapa kwa muda gani. Juma lililopita niliagizwa niondoke hapa kabla ya muda wa saa 24, lakini jambo hilo lilitatuliwa na hivyo naweza kukaa muda zaidi.”

Niliwasiliana na Wanafunzi wa Biblia walioishi Kharkov, ambalo sasa ni jiji kubwa katika Ukrainia, na kuamkiana huku kulifanya wadondoke machozi kwa furaha. Mkusanyiko mdogo ulifanywa kila usiku na kumalizika usiku wa manane. Akiandika baadaye juu ya kukutana kwake na hao ndugu, Baba alisema hivi: “Maskini ndugu zetu, vitabu vyao vichache vimetwaliwa kinguvu, na wenye mamlaka ni wenye uhasama kuwaelekea, na bado wao ni wenye furaha.”

Huduma ya Baba katika Muungano wa Sovieti ilielezwa katika broshua maalumu ambayo waliopewa wahudhuriaji wa kuwekwa wakfu kwa ofisi mpya ya tawi katika Juni 21, 1997, huko St. Petersburg, Urusi. Broshua hiyo inaeleza kwamba Baba alitumwa Moscow na alipata idhini ya “kuchapa na kugawanya nakala 15,000 za vijitabu Freedom for the Peoples na Where Are the Dead? huko Urusi.”

Aliporejea kutoka Urusi, Baba alipewa mgawo wa kuwa pilgrimu kule Marekani. Akiwa South Dakota alizuru makao ya dada wawili wa kimwili, Nellena na Verda Pool, ambao miaka ya baadaye walitumikia wakiwa mishonari katika Peru. Kwa shauku nyingi, walieleza uthamini wao kwa huduma ya Baba yenye bidii na kusema hivi: “Siku hizo za mapema kwa hakika akina ndugu walikuwa na roho ya upainia na walikwenda katika maeneo hayo yote ya kigeni bila vitu vya kimwili vya ulimwengu huu, lakini walikuwa na mioyo iliyojawa na upendo kwa Yehova. Huo uliwachochea kutimiza yote hayo.”

Ndoa na Safari ya Pili

Kwa muda wote huo Baba alikuwa akiwasiliana kwa barua na Clara Hubbert wa kisiwa cha Manitoulin kilichoko Ontario. Wote wawili walihudhuria mkusanyiko huko Columbus, Ohio, mnamo Julai 26, 1931, wakati ambapo Wanafunzi wa Biblia walikubali rasmi jina Mashahidi wa Yehova. (Isaya 43:10-12) Juma moja baada ya mkusanyiko huo walifunga ndoa. Punde tu baadaye, Baba aliondoka kwa safari yake ya pili ya mishonari kuelekea visiwa vya Karibea. Huko, alipanga kuwe na mikutano na akazoeza wengine kazi ya nyumba hadi nyumba.

Mama alikuwa akipokea picha, kadi, na barua kutoka Suriname, St. Kitts, na sehemu nyinginezo nyingi. Barua hizo zilitoa ripoti juu ya kazi ya kuhubiri na mara nyingine zilikuwa na habari kuhusu ndege, wanyama, na mimea iliyopatikana kwenye nchi aliyokuwa akizuru. Mnamo Juni mwaka wa 1932, Baba alimaliza mgawo wake huko Karibea na, kama kawaida yake alisafiri kwa gharama ya chini akirudi Kanada. Baada ya hapo, Baba na Mama walishiriki pamoja katika kazi ya kuhubiri wakati wote, wakipisha majira ya baridi kali ya mwaka wa 1932/1933 katika eneo la Ottawa wakiwa pamoja na kikundi kikubwa cha wahudumu wengine wa wakati wote.

Maisha Mafupi ya Familia

Ndugu yangu David alizaliwa mwaka wa 1934. Akiwa bado mtoto mchanga, alikuwa na tabia ya kusimama juu ya sanduku la mama la kuweka kofia na kufanyia mazoezi “hotuba zake.” Kama baba yake, amekuwa mwenye bidii kwa ajili ya Yehova muda wote wa maisha yake. Wote watatu walizuru makutaniko kutoka pwani ya mashariki ya Kanada hadi pwani ya magharibi kwa gari lenye kikuza-sauti ambacho kiliwekwa juu yake. Mimi nilizaliwa mwaka wa 1938, Baba akiwa kwenye mgawo wake huko British Columbia. David bado anakumbuka vile Baba aliniweka kitandani na Baba, Mama, na David wakiwa wamepiga magoti, Baba alitoa sala kumshukuru Yehova kwa ajili yangu.

Katika majira ya baridi kali ya mwaka wa 1939, tuliishi Vancouver, Baba alipokuwa akizuru makutaniko ya sehemu hiyo. Miongoni mwa barua ambazo tumehifadhi kwa miaka mingi ni ile ya Januari 14, 1939, aliyoandika akiwa Vernon, British Columbia. Baba alituandikia sisi watatu— Clara, David, na Ruth— barua hiyo akisema: “Busu ndogo tu na kumbatio.” Ndani ya barua ile mlikuwa na ujumbe kwa kila mmoja wetu. Kuhusu eneo lake, alisema kwamba mavuno ni mengi lakini wafanyakazi ni wachache.—Mathayo 9:37, 38.

Juma moja baada ya kurejea Vancouver kutoka kwenye mgawo wake, Baba alipoteza fahamu akiwa kwenye mkutano. Alipimwa na ikapatikana kwamba ana uvimbe wenye kansa kwenye ubongo wake. Mei 1, 1939, Baba alimaliza mwendo wake wa kidunia. Wakati huo nilikuwa na umri wa miezi tisa na David alikuwa amekaribia kuwa na umri wa miaka mitano. Mama yetu mpendwa, ambaye pia alikuwa na tumaini la mbinguni, alidumu akiwa mwaminifu kwa Mungu hadi kifo chake mnamo Juni 19, 1963.

Jinsi Baba alivyohisi juu ya pendeleo lake la kupeleka habari njema katika nchi nyingi inaonyeshwa na mojawapo ya barua zake kwa Mama. Alisema hivi kwa sehemu: “Kwa fadhili Yehova aliniruhusu nizuru nchi hizi nikiwa kama nuru ili nitangaze ujumbe wa Ufalme. Jina lake takatifu na litukuzwe. Kupitia udhaifu, kutojiweza na unyonge, utukufu wake waangaza.”

Sasa watoto, wajukuu, na vitukuu wa George na Clara Young pia wanamtumikia Mungu wetu mwenye upendo, Yehova. Niliambiwa kwamba Baba alinukuu kwa kawaida Waebrania 6:10 ambayo husema: “Mungu si asiye mwadilifu ili asahau kazi yenu na upendo mlioonyesha kwa ajili ya jina lake.” Sisi pia hatujasahau kazi ya Baba.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Baba yangu, aliye kulia, pamoja na ndugu zake watatu

[Picha katika ukurasa wa 25]

Baba (amesimama) akiwa na Ndugu Woodworth, Rutherford, na Macmillan

Chini: Baba (mbali kushoto) kwenye kikundi pamoja na Ndugu Russell

[Picha katika ukurasa wa 26]

Baba na Mama

Chini: Siku yao ya arusi

[Picha katika ukurasa wa 27]

Mimi, David na Mama miaka kadhaa baada ya kifo cha Baba