Je, Maisha Yako Yanaweza Kuwa na Maana Zaidi?
Je, Maisha Yako Yanaweza Kuwa na Maana Zaidi?
THAMANI ya kweli haiamuliwi kwa macho tu. Noti yenye thamani kubwa zaidi katika Marekani ilikuwa ya dola 10,000. Lakini karatasi ya noti hiyo ni yenye thamani ndogo.
Je, umewahi kujiuliza kama karatasi hizo ambazo hazina thamani zinaweza kufanya maisha yako yawe na maana ya kweli? Watu wengi hufikiri hivyo. Mamilioni ya watu hufanya kazi mchana na usiku ili kuchuma fedha nyingi kadiri wawezavyo. Nyakati nyingine kufuatia fedha huwalazimu wadhabihu afya yao, rafiki zao, na hata familia zao. Kwa mafanikio gani? Je, fedha—au vitu vinavyonunuliwa na fedha—vinaweza kutupa uradhi wa kweli na wa kudumu?
Kulingana na wachunguzi, kadiri tutafutavyo uradhi unaoletwa na mali, ndivyo inavyoonekana kuwa vigumu kuupata. Mwandishi mmoja wa habari, Alfie Kohn atoa kauli ya kwamba “kwa wazi uradhi haununuliwi. . . . Watu ambao utajiri ndio jambo kuu maishani mwao huelekea kupatwa na mahangaiko kupita kiasi na mshuko wa moyo pamoja na kukosa afya kwa ujumla.”
—International Herald Tribune.Ingawa huenda wachunguzi wakang’amua kwamba maisha yenye maana huhitaji jambo jingine mbali na fedha, watu wengi wana maoni tofauti. Hilo halishangazi hata kidogo, kwa kuwa watu wanaoishi katika mataifa ya Magharibi husikiliza matangazo ya biashara zaidi ya 3,000 kwa siku. Matangazo hayo yawe yanatangaza magari au peremende, wazo la msingi ni: ‘Nunua kitu hiki na utakuwa mwenye furaha zaidi.’
Matangazo hayo ya daima ya vitu vya kimwili yana matokeo gani? Mambo ya kiroho hupuuzwa mara nyingi! Kulingana na ripoti moja katika gazeti la habari la Newsweek, hivi karibuni askofu mkuu wa Cologne, Ujerumani, alijulisha kuwa “katika jamii yetu ya sasa, Mungu si wa maana.”
Labda umetumia karibu uwezo wako wote katika kutafuta riziki. Na huenda ukahisi kwamba huna wakati wa kufanya mambo mengine. Hata hivyo, mara kwa mara huenda ukahisi kwamba lazima maisha yana maana zaidi kuliko kujishughulisha tu hadi afya au uzee ukomeshe utendaji wako.
Je, kuzingatia mambo ya kiroho kutakutokezea uradhi zaidi? Ni nini kinachoweza kufanya maisha yako yawe na maana zaidi?