Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Umeathiriwa na Wabeuzi?

Je, Umeathiriwa na Wabeuzi?

Je, Umeathiriwa na Wabeuzi?

“MBEUZI ni mtu ambaye kamwe haoni sifa nzuri ya mwingine, naye hakosi kamwe kuona sifa mbaya. Yeye ni kama bundi, makini katika giza, lakini haoni nuruni, awindaye wadudu wala haoni wanyama wanaostahili kuwa chakula.” Yasemekana kwamba kasisi Mwamerika Henry Ward Beecher aliyeishi katika miaka ya 1800 ndiye aliyesema maneno hayo. Huenda watu wengi wakaona kwamba maneno hayo yamfafanua mbeuzi wa siku hizi. Lakini, neno la Kiingereza “cynic” linalotafsiriwa “mbeuzi” lilianzia Ugiriki ya kale ambapo halikurejezea tu mtu wa aina hiyo. Kwa karne nyingi, lilirejezea kikundi fulani cha wanafalsafa.

Falsafa ya Wabeuzi ilianzaje? Walifundisha nini? Je, inafaa Mkristo awe na tabia za Mbeuzi?

Wabeuzi wa Kale—Mwanzo na Itikadi Zao

Katika Ugiriki ya kale majadiliano yalikuwa jambo kuu. Katika karne zilizotangulia Wakati Wetu wa Kawaida, wanaume kama Socrates, Plato, na Aristotle walitoa falsafa zilizowaletea umaarufu. Mafundisho yao yaliwaathiri watu sana na mawazo yao yanapatikana bado katika utamaduni wa nchi za Magharibi.

Socrates (470-399 K.W.K.) alidai kwamba furaha haipatikani kwa kufuatia mambo ya kimwili au raha. Alisisitiza kwamba furaha ya kweli yatokana na kutafuta maadili. Socrates aliyaona maadili kuwa upeo wa wema. Ili kufikia mradi wake, alikataa anasa na jitihada zisizo za lazima kwa kuwa aliona kwamba zingemvuruga. Aliishi maisha yake kwa uangalifu asitumie chochote vibaya, huku akiunga mkono sifa za kujinyima na kiasi.

Socrates alitokeza mtindo wa kufundisha unaojulikana kama utaratibu wa Socrates. Kwa kawaida wanafalsafa walitoa mawazo mapya kwanza, na kuonyesha kwa nini jambo hilo lilikuwa kweli, lakini Socrates alifanya kinyume. Alisikiliza nadharia za wanafalsafa wengine, kisha akajaribu kuonyesha hitilafu zao. Njia hiyo ilisababisha mtazamo wa kuchambua na kutoheshimu watu wengine.

Miongoni mwa wafuasi wa Socrates kulikuwa mwanafalsafa aliyeitwa Antisthenes (445-365 K.W.K. hivi). Yeye na watu wengine kadhaa walibadili fundisho la Socrates, nao walisema kwamba maadili ndiyo wema pekee. Kwa maoni yao, ufuatiaji wa raha haukuwa kikengeusha-fikira tu bali namna ya uovu. Waliwadharau sana watu wenzao, wakajitenga kabisa na watu wengine. Walikuja kujulikana kama Wabeuzi. Huenda jina la Kiingereza, Cynic (Ubeuzi), lilitokana na neno la Kigiriki (ky·ni·kosʹ) linaloeleza jinsi walivyokuwa watu wenye kununa na wagomvi. Neno hilo lamaanisha “wanaofanana na mbwa.” *

Jinsi Maisha Yao Yalivyoathiriwa

Ingawa baadhi ya mawazo ya falsafa ya Wabeuzi kama vile kukataa tamaa ya mali na kujipendeza wenyewe tu, yameonwa kuwa mazuri, Wabeuzi walipita kiasi. Maisha ya Mbeuzi anayejulikana zaidi, mwanafalsafa Diogenes, yathibitisha jambo hilo.

Diogenes alizaliwa mwaka wa 412 K.W.K. mjini Sinope, karibu na Bahari Nyeusi. Alihamia Athene pamoja na baba yake, mahali alipokuja kujulia mafundisho ya Wabeuzi. Diogenes alifundishwa na Antisthenes, naye alijishughulisha sana na falsafa ya Wabeuzi. Socrates aliishi maisha sahili, na Antisthenes aliishi maisha yasiyo na raha. Naye Diogenes aliishi maisha ya kujinyima kabisa. Yasemekana kwamba kwa muda Diogenes aliishi katika pipa kubwa ili kuonyesha kwamba alikataa kabisa anasa.

Alipotafuta upeo wa wema, yasemekana kwamba Diogenes alitembea kutoka upande mmoja hadi upande mwingine wa mji wa Athene, akitafuta mtu mwema, akiwa na taa iliyokuwa imewashwa ijapokuwa kulikuwa na nuru ya mchana! Mwenendo wa aina hiyo ulivuta fikira za watu, naye Diogenes na Wabeuzi wengine walitumia njia hiyo ili kufundisha. Inasemekana kwamba pindi moja Aleksanda Mkuu alimwuliza Diogenes alitamani nini hasa. Jibu la Diogenes lilikuwa kwamba hakutaka lingine isipokuwa Aleksanda atoke njiani asiuzuie mwangaza wa jua!

Diogenes na Wabeuzi wengine waliishi kama ombaomba wanavyoishi. Hawakuwa na wakati wa kuwa na uhusiano wa kawaida na wanadamu wenzao, nao walikataa kufanya kazi ya serikali. Labda kwa sababu waliathiriwa na majadiliano ya utaratibu wa Socrates wakakosa kabisa kuheshimu wengine. Diogenes alikuja kujulikana kuwa mtu mwenye kukejeli kwa njia yenye kuumiza sana. Wabeuzi ‘walifananishwa na mbwa’ naye Diogenes mwenyewe aliitwa Jibwa. Alikufa mnamo 320 K.W.K. alipokuwa na miaka 90. Sanamu ya ukumbusho ya marumaru yenye umbo la mbwa ilisimamishwa juu ya kaburi lake.

Baadhi ya mawazo ya Ubeuzi yaliingizwa katika mafundisho ya wanafalsafa wengine. Hata hivyo, tabia za kipekee za Diogenes na wafuasi wa baadaye zililetea Ubeuzi sifa mbaya. Hatimaye, ulitoweka kabisa.

Wabeuzi wa Siku Hizi—Je, Wewe Unapaswa Kuwa na Tabia Kama Yao?

Kamusi The Oxford English Dictionary yamfafanua mbeuzi wa leo kuwa “mtu mwenye mwelekeo wa kukosoa au kulaumu. . . . Mtu asiyeweza kuamini kwamba kuna watu walio wanyofu na wema, aliyezoea kuonyesha mtazamo wake kwa kutoa kejeli na dhihaka; mtu mdhihaki aliyezoea kukosoa.” Tabia hizo zaonekana wazi katika ulimwengu unaotuzunguka, hata hivyo, hazipatani na utu wa Kikristo. Hebu fikiria mafundisho na kanuni za Biblia zifuatazo.

“BWANA amejaa huruma na neema, haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Yeye hatateta sikuzote, wala hatashika hasira yake milele.” (Zaburi 103:8, 9) Wakristo wameambiwa wawe “waigaji wa Mungu.” (Waefeso 5:1) Ikiwa Mungu Mweza Yote anaonyesha huruma na fadhili na upendo badala ya kuwa na “mwelekeo wa kukosoa au kulaumu,” bila shaka Wakristo wapaswa kujaribu kufanya vivyo hivyo.

Yesu Kristo aliye mfano kamili wa Yehova, ‘alituachia kigezo ili tufuate hatua zake kwa ukaribu.’ (1 Petro 2:21; Waebrania 1:3) Mara kwa mara, Yesu alifunua uongo wa kidini na kutoa ushuhuda kuhusu matendo maovu ya ulimwengu. (Yohana 7:7) Hata hivyo, alisifu sifa nzuri za watu wanyofu. Kwa mfano alisema hivi kuhusu Nathanaeli: “Ona, Mwisraeli kwa uhakika, ambaye katika yeye hamna udanganyi.” (Yohana 1:47) Mara kwa mara, Yesu aliisifu imani ya yule aliyefanyiwa mwujiza. (Mathayo 9:22) Baadhi ya watu walimlaumu mwanamke mmoja kwa kuwa waliona kwamba alitoa zawadi kwa ukarimu mno, hata hivyo Yesu hakumbeua lakini alisema hivi: “Kokote ambako habari njema hii ihubiriwako katika ulimwengu wote, alilofanya mwanamke huyu hakika litasimuliwa pia kuwa ukumbuko juu yake.” (Mathayo 26:6-13) Yesu alikuwa rafiki na mwandamani mwenye upendo wa wafuasi wake, “aliwapenda hadi mwisho.”—Yohana 13:1.

Kwa kuwa Yesu alikuwa mtu mkamilifu, angaliweza kwa urahisi kuona makosa ya watu wasiokamilika. Hata hivyo, badala ya kuwa na mwelekeo wa kukosoa na kutoamini watu, alijitahidi kuwaburudisha.—Mathayo 11:29, 30.

“[Upendo] huamini mambo yote.” (1 Wakorintho 13:7) Taarifa hiyo ni kinyume kabisa na mwelekeo wa mbeuzi anayetilia shaka nia na matendo ya wengine. Bila shaka, ulimwengu umejaa watu wenye nia mbaya; kwa hiyo kuna sababu ya kutahadhari. (Mithali 14:15) Hata hivyo, upendo unataka kuamini, hautilii shaka mno.

Mungu anawapenda na kuwaamini watumishi wake. Anajua udhaifu wao vizuri zaidi kuliko hata wao wenyewe. Hata hivyo, Yehova hawashuku kamwe watu wake, wala hatarajii kile wasichoweza kufanya. (Zaburi 103:13, 14) Isitoshe, Mungu anazingatia sifa nzuri za wanadamu, naye kwa kuwa anawaamini anawapa watumishi wake waaminifu, wasiokamilika, pendeleo na mamlaka mbalimbali.—1 Wafalme 14:13; Zaburi 82:6.

“Mimi, BWANA, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.” (Yeremia 17:10) Yehova anajua kilichomo moyoni mwa mtu. Sisi hatuwezi kujua kilichomo moyoni mwa mtu. Kwa hivyo, twahitaji kuwa waangalifu tusiwasingizie wengine.

Tukiruhusu mwelekeo wa ubeuzi kutuathiri na hatimaye kuongoza fikira zetu, inawezekana kwamba kutakuwa na migawanyiko kati yetu na waamini wenzetu. Mwelekeo huo unaweza kuharibu amani ya kutaniko la Kikristo. Na tufuate mfano wa Yesu aliyeuona udhaifu wa wanafunzi wake, hata hivyo kupitia matendo yake alionyesha kwamba aliwaamini. Akawa rafiki yao mwenye kutumainika.—Yohana 15:11-15.

“Vile mtakavyo watu wawafanyie nyinyi, wafanyieni wao kwa njia hiyohiyo.” (Luka 6:31) Tunaweza kutumia ushauri huo wa Yesu Kristo katika njia nyingi. Kwa mfano, sisi sote tunataka kutendewa kwa fadhili na heshima. Basi, sisi wenyewe twapaswa kusema na wengine kwa njia ya fadhili na heshima. Yesu alipofunua mafundisho ya uongo ya viongozi wa kidini, alifanya hivyo kwa nguvu lakini hakuwakejeli kamwe.—Mathayo 23:13-36.

Jinsi ya Kushinda Mwelekeo wa Ubeuzi

Ikiwa tumekatishwa tamaa, huenda ikawa rahisi kujiruhusu kuathiriwa na ubeuzi. Tunaweza kuushinda mwelekeo huo tukifahamu kwamba Yehova anawaamini watu wake wasiokamilika. Jambo hilo laweza kutusaidia kuona kwamba waabudu wengine wa Mungu ni watu wasiokamilika wanaojaribu kufanya yaliyo mema.

Baadhi ya watu ambao wametendwa vibaya wanaona ni vigumu kuamini watu. Kwa kweli hatupaswi kamwe kuwatumainia kabisa watu wasiokamilika. (Zaburi 146:3, 4) Hata hivyo, katika kutaniko la Kikristo wengi wanataka kwa moyo mweupe kuwa wenye kutia moyo. Hebu fikiria wale maelfu walio kama mama, baba, dada, ndugu, na watoto kwa wale ambao wamepoteza jamaa zao. (Marko 10:30) Fikiria jinsi ambavyo wengi wamejionyesha kuwa rafiki za kweli katika hali ya taabu. *Mithali 18:24.

Upendo wa kidugu, wala si ubeuzi, ndio unaowatambulisha wafuasi wa Yesu, kwa kuwa alisema hivi: “Kwa hilo wote watajua kwamba nyinyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo miongoni mwenu wenyewe.” (Yohana 13:35) Basi, na tuwe na upendo, na tujitahidi kuziona sifa nzuri za Wakristo wenzetu. Kufanya hivyo, kutatusaidia kuepuka kuwa na tabia za Wabeuzi.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 8 Inawezekana pia, kwamba jina Cynic (Ubeuzi) linatokana na jina la shule mjini Athene iliyoitwa Ky·noʹsar·ges, alipofundisha Antisthenes.

^ fu. 27 Ona makala yenye kichwa “Kutaniko la Kikristo—Chanzo cha Msaada Wenye Kutia Nguvu” katika gazeti la Mnara wa Mlinzi la Mei 15, 1999.

[Picha katika ukurasa wa 21]

Diogenes, Mbeuzi anayejulikana zaidi

[Hisani]

From the book Great Men and Famous Women