Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuenea kwa Chuki

Kuenea kwa Chuki

Kuenea kwa Chuki

“Watu hawafahamu kamwe wale wanaochukia.”—JAMES RUSSELL LOWELL, MWANDISHI WA INSHA NA BALOZI.

INAONEKANA kama chuki imetuzunguka pande zote. Majina kama Timor Mashariki, Kosovo, Liberia, Littleton, na Sarajevo—vilevile makundi yenye kufuata sera za Nazi, magenge yenye kunyoa upara, na makundi ya wazungu wenye ubaguzi wa rangi—Maiti pamoja na picha za majengo yaliyoteketezwa, makaburi walimozikiwa watu wengi ambayo yamechimbuliwa karibuni, yamedumu akilini mwetu.

Matazamio ya wakati ujao usio na chuki, mapambano, na jeuri yamevunjika. Danielle Mitterand, mke wa aliyekuwa rais wa Ufaransa aliyekufa, akumbuka hivi kuhusu wakati alipokuwa kijana: “Watu walikuwa na tazamio la kuishi katika jamii huru yenye kutumainika; wakiwa wenye amani ya akili wakiwa miongoni mwa wengine; walitazamia maisha yenye afya, amani na adhama wakilindwa na ulimwengu mkarimu na thabiti.” Mawazo hayo yalipatwa na nini? Aliomboleza hivi: “Miaka hamsini baadaye, kwa wazi tazamio letu limepatwa na pigo.”

Kuibuka tena kwa chuki hakuwezi kamwe kupuuzwa. Imeenea kote na inazidi kuonekana katika njia mbaya zaidi. Usalama wa kibinafsi ambao mamilioni ya watu huchukua kuwa jambo la kawaida umedhoofishwa na wimbi la vitendo vibaya vya chuki, yaonekana kila kitendo kinachofuata ni chenye kuhofisha kuliko kilichotangulia. Hata ikiwa hamna chuki nyumbani kwetu au nchi tunamoishi, kuna chuki kwingineko. Huenda tunaona uthibitisho wa hilo kila siku kwenye televisheni katika habari na programu za matukio. Hata chuki imeenea katika Internet. Fikiria mifano michache.

Mwongo uliopita umekuwa na ongezeko lisilo na kifani la utukuzo wa taifa. “Utukuzo wa taifa,” asema Joseph S. Nye, Jr. mkurugenzi wa Harvard Center for International Affairs, “waendelea kuimarika badala ya kupungua katika sehemu kubwa ya ulimwengu. Badala ya ulimwengu kuwa jamaa moja makundi yanajitenga na kujitofautisha na yale mengine ingawa kunao mfumo mmoja wa kupeleka habari. Hilo nalo hutokeza uhasama.”

Namna nyingine za chuki ni za kichinichini, huwa zimefichika ndani ya nchi au hata katika ujirani. Kalasinga mmoja mzee alipouawa na washiriki watano wa genge lenye kunyoa upara katika Kanada, tukio hilo “lilikazia kile ambacho wengine wanakiona kuwa kuibuka upya kwa uhalifu wenye kutokezwa na chuki katika nchi inayosifiwa mara nyingi kwa ajili ya uvumiliano wake wa kijamii.” Huko Ujerumani, mashambulizi dhidi ya jamii tofauti yanayofanywa na watu wenye itikadi kali yaliongezeka kwa asilimia 27 katika mwaka wa 1997 baada ya kupungua polepole katika miaka iliyopita. “Hilo ni tukio lenye kuvunja moyo,” akasema Waziri wa Mambo ya Ndani Manfred Kanther.

Ripoti moja ilifunua kwamba watoto zaidi ya 6,000 katika sehemu ya kaskazini ya Albania wanaishi kama wafungwa nyumbani kwao kwa kuhofia kupigwa risasi na maadui wa wazazi wao. Watoto hao ni wahasiriwa wa chuki za kifamilia “ambazo zimevuruga maisha ya maelfu ya familia.” Kulingana na Shirika la Upelelezi la Federal Bureau of Investigation (FBI), katika Marekani “ubaguzi wa kijamii ulichochea zaidi ya nusu ya visa 7,755 vya uhalifu wenye kuchochewa na chuki uliofanywa katika mwaka wa 1998 na kuripotiwa kwa shirika la FBI.” Uhalifu mwingine wenye kuchochewa na chuki ulisababishwa na ubaguzi wa kidini, kikabila au wa taifa, na ubaguzi dhidi ya walemavu.

Zaidi ya hayo, kila siku vichwa vya habari magazetini huonyesha ongezeko kubwa la kuhofu wageni kunakoelekezewa hasa wakimbizi ambao sasa wanazidi milioni 21. Kwa kusikitisha, wengi wanaoonyesha chuki kuwaelekea wageni ni vijana wanaochochewa na wanasiasa wasiojali na watu wengine wenye kutafuta visingizio. Ishara zisizo dhahiri sana za jambo hili hutia ndani kutokuwa na itibari, kukosa uvumilivu, na kuwa na maoni yasiyofaa juu ya watu walio tofauti.

Ni nini baadhi ya sababu za kuenea huku kwa chuki? Na ni nini liwezalo kufanywa ili kukomesha chuki? Makala ifuatayo itashughulikia maswali hayo.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]

Cover, top: UN PHOTO 186705/J. Isaac

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Daud/Sipa Press