Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Yosia Mnyenyekevu Alipendwa na Yehova

Yosia Mnyenyekevu Alipendwa na Yehova

Yosia Mnyenyekevu Alipendwa na Yehova

MWANA-MFALME Yosia wa Yuda mwenye umri wa miaka mitano ameogopa sana. Yedida mama yake anaomboleza. Yedida ana sababu ya kulia kwa kuwa babu ya Yosia, Mfalme Manase, amekufa.—2 Wafalme 21:18.

Sasa Amoni, baba yake Yosia ndiye atakuwa mfalme wa Yuda. (2 Mambo ya Nyakati 33:20) Miaka miwili baadaye (659 K.W.K.), Amoni auawa na watumishi wake. Watu wawaua wahaini hao na kumfanya kijana Yosia kuwa mfalme. (2 Wafalme 21:24; 2 Mambo ya Nyakati 33:25) Amoni alipokuwa akitawala, Yosia alikuwa amezoea harufu ya uvumba iliyotanda Yerusalemu kutoka kwenye madhabahu yaliyokuwa juu ya paa za nyumba ambako watu walisujudia miungu isiyo ya kweli. Makuhani wa kipagani wangeonekana wakitembea huku na huku, na waabudu—hata wengine waliodai wanamwabudu Yehova—walikuwa wakiapa kwa mungu Malkamu.—Sefania 1:1, 5.

Yosia anajua kwamba Amoni alitenda uovu kwa kuabudu miungu isiyo ya kweli. Mfalme huyo mchanga wa Yuda apata pia kufahamu vyema ujumbe wa Sefania nabii wa Mungu. Yosia anapokuwa na umri wa miaka 15 (652 K.W.K.), akiwa katika mwaka wake wa nane wa utawala aazimia kutii maneno ya Sefania. Akiwa angali mvulana, Yosia aanza kumtafuta Yehova.—2 Mambo ya Nyakati 33:21, 22; 34:3.

Yosia Atenda!

Miaka minne inapita naye Yosia aanza kuondoa dini isiyo ya kweli kutoka Yuda na Yerusalemu (648 K.W.K.). Aziharibu sanamu, zile nguzo takatifu, na yale madhabahu ya uvumba yanayotumiwa katika ibada ya Baali. Sanamu za miungu isiyo ya kweli zapondwa-pondwa na kutupwa kwenye makaburi ya wale walioitolea dhabihu. Madhabahu yanayotumiwa kwa ibada chafu yatiwa unajisi kisha yabomolewa.—2 Wafalme 23:8-14.

Usafishaji wa Yosia umepamba moto wakati Yeremia, mwana wa kuhani Mlawi, awasilipo Yerusalemu (647 K.W.K.). Yehova Mungu amemweka rasmi Yeremia mchanga awe nabii wake, naye atangaza kwa nguvu iliyoje ujumbe wa Yehova dhidi ya dini isiyo ya kweli! Yosia na Yeremia walikuwa karibu umri sawa. Licha ya usafishaji wa Yosia wenye ujasiri na ujumbe uliotangazwa kwa ujasiri na Yeremia, upesi watu wairudia tena ibada isiyo ya kweli.—Yeremia 1:1-10.

Uvumbuzi Wenye Thamani Sana!

Miaka mitano hivi yapita. Yosia mwenye umri wa miaka 25 amekuwa akitawala kwa miaka 18 hivi. Awaita Shafani, mwandishi; Maaseya, akida wa mji; na Yoa mwandishi wa tarehe. Mfalme amwamuru Shafani hivi: ‘Mwambie Hilkia, kuhani mkuu, aichukue fedha ambayo mabawabu wameipokea kwa watu; wakapewe wafanya kazi ili wapate kuitengeneza nyumba ya BWANA.’—2 Wafalme 22:3-6; 2 Mambo ya Nyakati 34:8.

Tangu asubuhi na mapema, watu wanaotengeneza hekalu wafanya kazi kwa bidii. Yosia amshukuru Yehova kwa sababu wafanyakazi hao wanarekebisha uharibifu ambao baadhi ya wazazi wake wa kale waliifanyia nyumba ya Mungu. Kazi inapoendelea kufanywa, Shafani afika kuleta ripoti fulani. Lakini amebeba nini mkononi? Kumbe, amebeba kunjo! Yeye aeleza kuwa Hilkia Kuhani wa Cheo cha Juu amekiona “kitabu cha torati ya BWANA iliyotolewa kwa mkono wa Musa.” (2 Mambo ya Nyakati 34:12-18) Huo ni uvumbuzi ulioje—kwa wazi ni nakala ya asili ya Torati!

Yosia ana hamu ya kusikia kila neno katika kile kitabu. Shafani anaposoma, mfalme ajaribu kuona jinsi kila moja ya sheria hizo inavyotumika kwake mwenyewe na kwa wale watu wengine. Hasa avutiwa na namna kitabu hicho kinavyokazia ibada safi na kutabiri mapigo na uhamisho ambao ungefika ikiwa watu wangeshiriki dini isiyo ya kweli. Aking’amua kwamba si amri zote za Mungu zimetekelezwa, Yosia ayararua mavazi yake na kuwapa Hilkia, Shafani, na wengineo amri hii: ‘Mwulizeni BWANA habari za maneno ya kitabu hiki; kwa kuwa hasira ya BWANA ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki.’—2 Wafalme 22:11-13; 2 Mambo ya Nyakati 34:19-21.

Neno la Yehova Lawasilishwa

Wajumbe wa Yosia wamwendea Hulda nabii wa kike huko Yerusalemu na warudi na ripoti. Hulda amewasilisha neno la Yehova, linaloonyesha kwamba maafa yaliyotajwa katika kitabu kile kilichopatikana hivi karibuni yatalikumba taifa hilo lenye kuasi. Hata hivyo, kwa sababu Yosia amejinyenyekeza mbele ya Yehova Mungu, hatayaona maafa hayo. Yeye atakusanywa pamoja na baba zake na kuwekwa kaburini mwake kwa amani.—2 Wafalme 22:14-20; 2 Mambo ya Nyakati 34:22-28.

Kwa kuwa Yosia alikufa vitani, je, unabii wa Hulda ulikuwa sahihi? (2 Wafalme 23:28-30) Ndiyo, kwa sababu “amani” aliyokusanywa nayo kaburini ni kinyume cha “mabaya” ambayo yangeletwa juu ya Yuda. (2 Wafalme 22:20; 2 Mambo ya Nyakati 34:28) Yosia alikufa kabla ya yale maafa ya miaka ya 609-607 K.W.K. wakati Wababiloni walipozingira na kuharibu Yerusalemu. Na ‘kukusanywa pamoja na baba zake’ si lazima kuwe kifo kisicho cha jeuri. Maneno yenye kufanana na hayo yametumiwa kuhusiana na vifo vyenye jeuri na vilevile vingine visivyo vya jeuri.—Kumbukumbu la Torati 31:16; 1 Wafalme 2:10; 22:34, 40.

Ibada ya Kweli Yasonga Mbele

Yosia awakusanya watu wa Yerusalemu kwenye hekalu na kuwasomea “maneno yote ya kitabu cha agano” kilichopatikana katika nyumba ya Yehova. Kisha afanya agano la “kumfuata BWANA, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho.” Watu wote wanalikubali agano hilo.—2 Wafalme 23:1-3.

Mfalme Yosia sasa aanzisha kampeni nyingine kali sana dhidi ya ibada ya sanamu. Makuhani wa Yuda wa miungu ya kigeni wafukuzwa. Makuhani Walawi wenye kuhusika na ibada isiyo ya kweli wapoteza pendeleo lao la kutumikia katika madhabahu ya Yehova, na mahali pa juu palipojengwa wakati wa utawala wa Mfalme Solomoni paharibiwa pasitumike tena katika ibada. Usafishaji huo waenea hadi nchi iliyokuwa hapo awali ya ufalme wa makabila kumi ya Israeli uliokuwa umepinduliwa na Waashuri (740 K.W.K.).

Kwa utimizo wa maneno yaliyotamkwa miaka 300 mapema na “mtu wa Mungu” asiyetajwa jina lake, Yosia aiteketeza mifupa ya makuhani wa Baali kwenye madhabahu iliyokuwa imesimamishwa na Mfalme Yeroboamu wa Kwanza huko Betheli. Mahali pa juu paondolewa hapo na katika miji mingine, na makuhani waabudu sanamu watolewa kuwa dhabihu kwenye madhabahu zilezile walizokuwa wanazitumikia.—1 Wafalme 13:1-4; 2 Wafalme 23:4-20.

Sikukuu Kubwa ya Kupitwa Yafanywa

Matendo ya Yosia ya kuendeleza ibada safi yanategemezwa na Mungu. Muda wote wa maisha yake mfalme atamshukuru Mungu kwa sababu watu “hawakuacha kumfuata BWANA, Mungu wa baba zao.” (2 Mambo ya Nyakati 34:33) Naye Yosia angewezaje kusahau tukio la ajabu sana lililofanyika katika mwaka wa 18 wa utawala wake?

Mfalme awaamuru watu hivi: “Mfanyieni BWANA, Mungu wenu, pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki [kilichopatikana hivi karibuni] cha agano.” (2 Wafalme 23:21) Yosia ashangilia watu wanapoitikia vizuri. Kwa ajili ya sherehe hiyo, yeye binafsi atoa wanyama wa Sikukuu ya Kupitwa 30,000 na ng’ombe 3,000. Ni Sikukuu ya Kupitwa iliyoje! Matoleo yake, mipango yake ya hali ya juu na idadi ya watu waliosherehekea Sikukuu hii ya Kupitwa, ilipita yote iliyowahi kufanywa tangu siku za nabii Samweli.—2 Wafalme 23:22, 23; 2 Mambo ya Nyakati 35:1-19.

Aombolezewa Sana Anapokufa

Kwa muda uliobaki wa miaka 31 ya utawala wake (659-629 K.W.K.), Yosia atawala akiwa mfalme mwema. Kuelekea mwisho wa utawala wake, Yosia apata habari kwamba Farao Neko ana mipango ya kupitia Yuda ili kukutana na majeshi ya Babiloni na kusaidia mfalme wa Ashuru huko Karkemishi karibu na Mto Frati. Kwa sababu ambayo haijulikani, Yosia aondoka kwenda kupigana na Mmisri huyo. Neko awatuma wajumbe kwake, akisema: “Acha basi kumpinga Mungu, aliye pamoja nami, asikuharibu.” Lakini Yosia ajifanya kuwa mtu mwingine na kujaribu kuwarudisha nyuma Wamisri huko Megido.—2 Mambo ya Nyakati 35:20-22.

Ole wake mfalme wa Yuda! Wapiga-upinde wa upande wa maadui wamlenga shabaha, naye awaambia watumishi wake hivi: “Niondoeni; kwani nimejeruhiwa sana.” Wanamtoa Yosia katika gari lake la vita na kumweka kwenye gari jingine, na kuelekea Yerusalemu. Akiwa hapo au wakiwa njiani kwenda mjini, Yosia akata pumzi. “Naye akafa, akazikwa makaburini mwa babaze,” lasema simulizi lenye kupuliziwa, “wakamlilia Yosia Yuda wote na Yerusalemu.” Naye Yeremia akamlilia kwa nyimbo, na huyo mfalme akawa mwenye kutajwa katika nyimbo za maombolezo zilizoimbwa kwenye sherehe maalumu za baadaye.—2 Mambo ya Nyakati 35:23-25.

Naam, kwa kusikitisha Mfalme Yosia alikosea alipofanya vita na Wamisri. (Zaburi 130:3) Hata hivyo, unyenyekevu wake na uthabiti wake kwa ibada ya kweli zilimletea kibali cha Mungu. Jinsi maisha ya Yosia yanavyoonyesha vyema kwamba Yehova huwapenda watumishi wake wenye moyo mnyenyekevu na wenye bidii!—Mithali 3:34; Yakobo 4:6.

[Picha katika ukurasa wa 29]

Mfalme Yosia mchanga alimtafuta Yehova kwa bidii

[Picha katika ukurasa wa 31]

Yosia aliharibu mahali pa juu na akaendeleza ibada ya kweli