Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Nimebarikiwa kwa Urithi wa Pekee

Nimebarikiwa kwa Urithi wa Pekee

Simulizi la Maisha

Nimebarikiwa kwa Urithi wa Pekee

KAMA ILIVYOSIMULIWA NA CAROL ALLEN

Nilikuwa peke yangu, nikishikilia kitabu changu kipya. Nilishikwa na hofu, na machozi yakanidondoka. Kwani, nilikuwa mshichana mdogo mwenye umri wa miaka saba tu niliyekuwa nimepotea katika jiji la kigeni huku nikiwa nimezungukwa na watu wengi sana!

HIVI majuzi, karibu miaka 60 baadaye, nilikumbuka vizuri sana jambo hilo lililonipata nikiwa mtoto, kutokana na ziara tuliyofanya na mume wangu Paul, kwenye Kituo cha Elimu cha Watchtower huko Patterson, New York. Alikuwa amealikwa huko kuhudhuria darasa la pili la shule ya waangalizi wasafirio wa Mashahidi wa Yehova.

Tulipotazama-tazama sebule iliyoangazwa kwa nuru ya jua, niliona ishara kubwa iliyoandikwa “MIKUSANYIKO.” Katikati yake kulikuwa na picha ya zamani isiyo na rangi ya watoto waliokuwa wakionyesha nakala zao za kitabu changu cha utotoni! Upesi nikasoma maandishi kwenye picha hiyo: “1941–Huko St. Louis, Missouri, kipindi cha asubuhi kilipoanza, watoto 15,000—kati ya umri wa miaka 5 na 18—walikusanyika katika uwanja mkuu ulioelekeana moja kwa moja na jukwaa. . . . Ndugu Rutherford alitangaza kutolewa kwa kitabu kipya, Children.”

Kila mtoto alipewa nakala yake mwenyewe. Kisha watoto hao wakarudi pale ambapo wazazi wao walikuwa wameketi—wote, isipokuwa mimi. Nilikuwa nimepotea! Mwelekezaji mmoja mwenye urafiki alinichukua na kunisimamisha kwenye sanduku refu la michango na kuniambia nitafute mtu nimjuaye. Nikiwa na wasiwasi, nilitazama-tazama umati uliokuwa unamiminika kupitia ngazi pana. Kwa ghafula, nikaona mtu niliyemtambua! “Mjomba Bob! Mjomba Bob!” Nilikuwa nimepatikana! Bob Rainer alinibeba hadi pale ambapo wazazi wangu wenye wasiwasi walikuwa wakingojea.

Matukio ya Awali Yaliyogeuza Maisha Yangu

Kutazama picha hiyo kulifanya nikumbuke mambo mengi sana—matukio yaliyogeuza maisha yangu na kufanya tufike kwenye majengo yenye kupendeza ya Patterson. Nilikumbuka matukio ya miaka zaidi ya mia moja iliyopita, ambayo niliyasikia hasa kutoka kwa babu na nyanya yangu na wazazi wangu.

Mnamo Desemba 1894 mhudumu wa wakati wote wa Wanafunzi wa Biblia, kama Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo, alimtembelea babu yangu, Clayton J. Woodworth, nyumbani kwake huko Scranton, Pennsylvania, Marekani. Clayton alikuwa ametoka tu kuoa. Alimwandikia barua msimamizi wa Watch Tower Bible and Tract Society, Charles Taze Russell, nayo ikachapishwa katika gazeti la Mnara wa Mlinzi Juni 15, 1895, la Kiingereza. Alieleza hivi:

“Sisi ni wenzi wachanga wa ndoa ambao tumekuwa washiriki wa kanisa la Kiprotestanti kwa miaka kumi hivi; lakini kwa sasa, twaamini kwamba tunatoka kwenye giza kuingia kwenye nuru ya siku mpya ambayo sasa yapambazuka kwa wana waliojiweka wakfu wa Aliye Juu Zaidi. . . . Zamani kabla ya mimi na mke wangu kujuana tulikuwa na tamaa kubwa ya kumtumikia Bwana, ikiwa ni mapenzi yake, tukiwa wamishonari katika eneo la kigeni.”

Baadaye, mwaka wa 1903, Sebastian na Catherine Kresge, wazazi wa nyanya yangu, walisikiliza kwa furaha ujumbe wa Biblia ulioletwa na wawakilishi wawili wa Watch Tower katika shamba kubwa mno walimokuwa wakiishi, katika milima yenye kupendeza ya Pocono huko Pennsylvania. Binti zao, Cora na Mary, pia waliishi huko pamoja na waume zao, Washington na Edmund Howell. Wawakilishi hao wa Watch Tower, Carl Hammerle na Ray Ratcliffe, walikaa nao kwa juma zima, wakiwafundisha mambo mengi. Washiriki wote sita wa familia hiyo walisikiliza, wakajifunza, na punde wakawa Wanafunzi wa Biblia wenye bidii.

Mwaka huohuo, 1903, Cora na Washington Howell walipata binti waliyemwita Catherine. Jinsi alivyokuja kuolewa hatimaye na baba yangu, Clayton J. Woodworth, Jr., naamini ni kisa chenye maana na chenye kupendeza. Chaonyesha ufahamu wenye upendo na hangaikio la mzazi la babu yangu Clayton J. Woodworth, Sr.

Baba Yangu Apokea Msaada Wenye Upendo

Baba yangu, Clayton mdogo, alizaliwa huko Scranton mwaka wa 1906, umbali wa kilometa 80 hivi kutoka shamba la Howell. Miaka hiyo ya mapema, Babu Woodworth alijuana vizuri na familia kubwa ya Howell, mara nyingi akifurahia ukaribishaji-wageni wao uliojulikana sana. Alisaidia sana kutaniko la Wanafunzi wa Biblia katika eneo hilo. Muda si muda, Babu akaitwa kuandikisha ndoa za wana watatu wa Howell, na kwa kufikiria masilahi ya mwana wake mwenyewe, aliazimia kuwa akienda naye kwenye kila mojawapo ya arusi hizo.

Wakati huo baba hakuwa amejihusisha sana na huduma ya Wanafunzi wa Biblia. Alimpeleka Babu kwa gari kwenda kufanya ziara zake za huduma, lakini kijapokuwa kitia-moyo cha Babu, Baba hakuchukua hatua yoyote. Wakati huo, baba yangu alipenda muziki kuliko kitu kingine chochote, naye alikuwa akijitahidi kuwa mwanamuziki wa kulipwa.

Catherine, binti ya Cora na Washington Howell, alikuwa pia amekuwa mwanamuziki mashuhuri, akipiga na kufundisha piano. Lakini wakati alipokuwa tu aanze kuwa mwanamuziki wa kulipwa, aliacha muziki, akaanza kushiriki katika huduma ya wakati wote. Babu aliona kwamba Catherine angekuwa mwandamani bora wa mwanawe—angalau kulingana na maoni yangu! Baba alibatizwa na kumwoa Mama miezi sita baadaye, mwezi wa Juni 1931.

Sikuzote Babu alijivunia kipawa cha muziki cha mwanawe. Alifurahi sana Baba alipoombwa kufundisha kikundi cha okestra cha mkusanyiko mkubwa kwa ajili ya mkusanyiko wa kimataifa wa 1946 huko Cleveland, Ohio. Miaka iliyofuata, Baba aliongoza okestra kwenye mikusanyiko kadhaa mingine ya Mashahidi wa Yehova.

Kesi ya Babu na Maisha Yake Gerezani

Katika sebule ya Patterson, mimi na Paul tuliona pia picha iliyo kwenye ukurasa unaofuata. Niliitambua picha hii mara moja, kwa kuwa Babu alinitumia nakala moja miaka 50 iliyopita. Ndiye aliyesimama mwisho kulia.

Wakati wa msisimko wa kizalendo uliotokea wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, hao Wanafunzi wanane wa Biblia—kutia ndani Joseph F. Rutherford (aliyeketi katikati), msimamizi wa Watch Tower Society—walitiwa gerezani kimakosa na kuzuiwa bila dhamana. Mashtaka dhidi yao yalihusu taarifa zilizo katika buku la saba la Studies in the Scriptures, lenye kichwa The Finished Mystery. Taarifa hizo zilieleweka vibaya kuwa zenye kuvunja moyo Marekani isishiriki katika Vita ya Ulimwengu ya Kwanza.

Kwa kipindi cha miaka mingi, Charles Taze Russell aliandika mabuku sita ya Studies in the Scriptures, lakini alikufa kabla hajaandika buku la saba. Kwa hiyo Babu na Mwanafunzi wa Biblia mwingine walipewa maandishi yake, nao wakaandika buku la saba. Hilo lilitolewa mwaka wa 1917, kabla ya mwisho wa vita. Kwenye kesi hiyo, Babu na wengi wa wale wenzake walihukumiwa vifungo vinne, kila mmoja kifungo cha miaka 20, vyote vikiambatana pamoja.

Maelezo ya picha kwenye sebule ya Patterson yasema: “Miezi tisa baada ya Rutherford na wenzake kuhukumiwa—na vita ikiwa imekwisha—Machi 21, 1919, mahakama ya rufani iliamuru washtakiwa wote wanane waachiliwe kwa dhamana, na Machi 26, walifunguliwa huko Brooklyn kwa dhamana ya dola 10,000 kila mmoja. Mei 5, 1920, J. F. Rutherford na wenzake waliondolewa mashtaka.”

Baada ya kuhukumiwa, lakini kabla ya kupelekwa kwenye gereza kuu la serikali la Atlanta, Georgia, ndugu hao wanane walikaa kwa siku chache kifungoni katika jela ya Raymond Street huko Brooklyn, New York. Akiwa huko Babu aliandika akieleza jinsi alivyowekwa ndani ya seli ya meta 1.8 kwa meta 2.4 “katikati ya uchafu wenye kutisha na mvurugo.” Alisema: “Unaona rundo la magazeti, na ukiyapuuza mara ya kwanza, unakuja kugundua kwamba makaratasi hayo na sabuni na kitambaa cha kuogea, humaanisha fursa yako ya kuwa safi na kujipatia heshima.”

Hata hivyo, Babu alidumisha ucheshi wake, akiita jela hiyo “Hôtel de Raymondie” na kusema, “Nitaondoka hapa siku zangu za malazi zitakapokwisha.” Pia alifafanua matembezi yake ya uani. Wakati mmoja aliposimama ili achanwe nywele zake, mnyakuzi wa mifukoni aliiba saa yake ya mfukoni, lakini kama alivyoandika, “Mnyororo wake ulikatika nami nikaiokoa.” Nilipokuwa nikitembelea Betheli ya Brooklyn mwaka wa 1958, Grant Suiter, aliyekuwa mwandishi mweka-hazina wa Watch Tower Society, aliniita kwenye ofisi yake na kunipa saa hiyo. Ningali naithamini sana.

Jinsi Baba Alivyoathiriwa

Babu alipotiwa gerezani isivyo haki mwaka wa 1918, baba yangu alikuwa na umri wa miaka 12 tu. Nyanya alifunga nyumba yao na kumchukua wakaishi naye pamoja na mama yake na dada zake watatu. Jina la familia la mama lilikuwa Arthur, na familia hiyo ilidai kwa fahari kwamba mmoja wa watu wao wa ukoo, Chester Alan Arthur, alikuwa rais wa 21 wa Marekani.

Baada ya Babu Woodworth kuhukumiwa kifungo kirefu kwa madai ya uhalifu dhidi ya Marekani, kwa wazi familia ya akina Arthur ilihisi kwamba ameliaibisha jina lao la familia. Kilikuwa kipindi chenye kuumiza kihisia-moyo kwa baba yangu. Labda jambo hilo ndilo lililomfanya asishiriki katika huduma ya hadharani mwanzoni.

Babu alipofunguliwa kutoka gerezani, alihamisha familia yake kwenda kwenye nyumba kubwa iliyokandikwa kwa lipu kwenye barabara ya Quincy Street huko Scranton. Nikiwa mtoto, niliijua vema nyumba hiyo kutia ndani vyombo maridadi vya kauri vya Nyanya vilivyokuwa humo. Tuliviita vyombo vyake vitakatifu kwa sababu hakuna mtu aliyeruhusiwa kuviosha isipokuwa Nyanya. Baada ya Nyanya kufa mwaka wa 1943, Mama alivitumia vyombo hivyo maridadi mara nyingi alipokuwa na wageni.

Mwenye Shughuli Katika Utumishi wa Ufalme

Siku nyingine kwenye chuo cha Patterson, niliona picha ya Ndugu Rutherford akitoa hotuba kwenye mkusanyiko wa 1919 huko Cedar Point, Ohio. Aliwatia moyo wote washiriki kwa bidii kutangaza Ufalme wa Mungu na kutumia gazeti jipya lililotolewa mkusanyikoni, The Golden Age. Babu aliwekwa kuwa mhariri wake, naye alichangia makala zake hadi miaka ya 1940, muda mfupi kabla ya kifo chake. Mwaka wa 1937 jina la gazeti hilo likabadilishwa kuwa Consolation na mwaka wa 1946 likawa Awake!

Babu alifanyia kazi yake ya kuandika akiwa nyumbani huko Scranton na Makao Makuu ya Watch Tower huko Brooklyn yaliyokuwa kilometa 240 hivi kutoka Scranton, akitumia majuma mawili kila mahali. Baba asema kwamba akumbuka mara nyingi alisikia taipureta ya Babu ikichapa saa kumi na moja asubuhi. Hata hivyo, Babu pia alilichukua kwa uzito daraka la kushiriki katika kazi ya kuhubiri. Hata alitengeneza fulana iliyokuwa na mifuko ya ndani mikubwa ya kubebea vichapo vya Biblia. Mke wa mjombangu mwenye umri wa miaka 94, Naomi Howell, angali na fulana moja. Pia alitengeneza mkoba wa vitabu wa wanawake.

Wakati mmoja baada ya mazungumzo ya Biblia yenye kusisimua, mtumishi mwenzi wa Babu alisema hivi: “C. J., umefanya kosa moja.”

“Kosa gani?” Babu akauliza. Akaangalia fulana yake. Mifuko yote miwili ilikuwa mitupu.

“Umesahau kumtolea andikisho la The Golden Age.” Walicheka kwa sababu mhariri alisahau kutoa gazeti lake.

Kumbukumbu za Kukua

Nakumbuka Babu akiniweka kwenye mapaja yake nikiwa mtoto, akiwa ameshika mkono wangu mdogo aliponisimulia “Hadithi ya Vidole.” Kuanzia dole gumba kisha kidole shahada yeye alisema jambo fulani la pekee kuhusu kila kidole. Kisha akavifunga vidole vyote pamoja na kutoa fundisho hili la maadili: “Vyote vyafanya kazi pamoja kwa umoja, kila kimoja kikisaidia mwenzake.”

Baada ya wazazi wangu kuoana, walihamia Cleveland, Ohio, na wakawa marafiki wa karibu zaidi wa Ed na Mary Hooper. Watu wa familia zao walikuwa Wanafunzi wa Biblia tokea mwanzo wa karne ya ishirini. Wazazi wangu na Mjomba Ed na Shangazi Mary, kama nilivyowaita walikuwa marafiki wa karibu sana. Akina Hooper walikuwa wamefiwa na mtoto wao wa pekee, msichana, kwa hiyo nilipozaliwa mwaka wa 1934, nikawa “binti” yao wa pekee. Nikiwa nimelelewa katika mazingira yaliyofana sana kiroho, nilijiweka wakfu kwa Mungu na kubatizwa kabla ya mwaka wangu wa nane.

Usomaji wa Biblia ulikuwa sehemu ya miaka yangu ya mapema. Ufafanuzi wa maisha katika ulimwengu mpya wa Mungu upatikanao kwenye Isaya 11:6-9 ulikuwa mojawapo ya vifungu vya maandiko nilivyovipenda zaidi. Jitihada yangu ya kwanza kumaliza kusoma Biblia nzima ilikuwa mwaka wa 1944, baada ya kupokea nakala yangu ya kibinafsi ya American Standard Version, iliyotolewa katika toleo la pekee kwenye mkusanyiko wa Buffalo, New York. Nilisisimuka kama nini kusoma tafsiri hii ambayo jina la Mungu, Yehova, lilikuwa limerudishwa mahali pake pafaapo karibu mara 7,000 katika “Agano la Kale”!

Miisho-juma ilikuwa nyakati za furaha. Wazazi wangu na akina Hooper walinipeleka kuhubiri mashambani. Tulibeba chakula cha mchana na kukila kandokando ya kijito. Kisha tukaenda kwenye shamba la mtu kutoa hotuba ya Biblia ambayo tulikuwa tumewaalika majirani wote waje kuisikiliza. Maisha yalikuwa sahili. Tulikuwa familia zenye furaha. Baadaye baadhi ya marafiki hao wa mapema wa familia yetu walikuja kuwa waangalizi wasafirio, kutia ndani Ed Hooper, Bob Rainer, na wanae wawili. Richard Rainer angali anafanya kazi hii, akiwa na mke wake, Linda.

Nyakati za kiangazi zilikuwa zenye kufurahisha zaidi. Nilikaa shambani kwa akina Howell na binamu zangu. Mwaka wa 1949 binamu yangu Grace aliolewa na Malcolm Allen. Kumbe miaka ya baadaye ningeolewa na ndugu yake Malcolm. Binamu yangu mchanga zaidi Marion alikuwa mmishonari huko Uruguai. Aliolewa na Howard Hilborn mwaka wa 1966. Binamu wote wawili walitumika pamoja na waume zao kwenye makao makuu ya Brooklyn kwa miaka mingi.

Babu na Kuhitimu Kwangu

Wakati wa miaka yangu ya shule ya sekondari, Babu alikuwa mwepesi wa kuandika barua. Barua zake zilitia ndani picha za zamani za familia zikiwa na maandishi yaliyochapwa nyuma, zikieleza historia ya familia. Hivyo ndivyo nilivyopokea nakala yangu ya picha yake akiwa na wenzake waliotiwa gerezani isivyo haki.

Kufikia mwisho wa mwaka wa 1951, Babu alikuwa amepoteza zoloto yake kwa sababu ya kansa. Bado alikuwa na akili ya kuandika mambo kwa njia ya ucheshi, lakini ilimbidi aandike maneno yake kwenye kitabu kidogo alichobeba. Darasa langu la sekondari lilipaswa kuhitimu katikati ya muhula, Januari 1952. Mwanzoni mwa Desemba, nilimtumia Babu hotuba nitakayotoa siku yangu ya kuhitimu. Aliifanyia marekebisho fulani kisha kwenye ukurasa wa mwisho akaandika maneno mawili yaliyonigusa moyo: “Babu afurahia.” Alimaliza mwendo wake wa dunia akiwa na umri wa miaka 81, Desemba 18, 1951. * Ningali nina maandishi hayo yangu yaliyochakaa ya hotuba ya kuhitimu kwangu ikiwa na maneno hayo mawili kwenye ukurasa wa mwisho.

Mara tu baada ya kuhitimu kwangu, nilianza utumishi wa painia, kama vile ambavyo Mashahidi wa Yehova huita kazi ya kuhubiri wakati wote. Mwaka wa 1958, nilihudhuria mkusanyiko mkubwa zaidi katika New York City, ambapo kilele cha watu 253,922 kutoka katika nchi 123 walijaza Yankee Stadium na Polo Grounds. Nikiwa huko siku moja nilikutana na mjumbe kutoka Afrika aliyevaa beji yenye jina “Woodworth Mills.” Alikuwa amepewa jina hilo la babu miaka 30 iliyopita!

Nafurahia Urithi Wangu

Nilipokuwa na umri wa miaka 14, mama yangu alianza kupainia tena. Alikufa miaka 40 baadaye, mwaka wa 1988, akiwa angali painia! Baba alishiriki katika kazi ya upainia alipoweza. Alikufa miezi tisa kabla ya Mama. Wale tuliojifunza nao wakawa marafiki wapendwa maishani. Baadhi ya wana wao walienda kutumikia kwenye makao makuu ya Brooklyn, na wengine wakawa mapainia.

Kwangu mimi, mwaka wa 1959 ulikuwa wa pekee. Ndio mwaka nilipojulishwa kwa Paul Allen. Alikuwa amewekwa kuwa mwangalizi asafiriye mwaka wa 1946 alipohitimu kutoka darasa la saba la Gileadi, shule ya kuzoeza wamishonari wa Mashahidi wa Yehova. Kufikia wakati tulipofahamiana, hakuna aliyejua kwamba mgawo ufuatao wa Paul ungekuwa Cleveland, Ohio, mahali ambapo nilikuwa nikipainia. Baba alimpenda, na pia Mama. Tulioana Julai 1963 kwenye shamba la Howell, tukizungukwa na familia zetu na Ed Hooper ndiye aliyetoa hotuba. Ilikuwa kama ndoto iliyotimia.

Paul hakuwa na gari lake mwenyewe. Tulipoondoka Cleveland kwenda kwenye mgawo wake, mizigo yetu yote ilitoshea kwenye gari langu aina ya Volkswagen ya 1961. Mara nyingi marafiki walikuja Jumatatu, kututazama tulipokuwa tukifunganya kwenda kwenye kutaniko jingine. Ilikuwa kama sarakasi kuona masanduku, mikoba, taipureta, na kadhalika zikipakiwa katika gari hilo dogo.

Mimi na Paul tumesafiri kilometa nyingi sana, tukifurahia nyakati nzuri na kuvumilia nyakati ngumu za maisha ya sasa—yote yakiwa yamefanywa kwa nguvu ambazo ni Yehova tu awezaye kuandaa. Miaka hiyo imekuwa yenye furaha, ikijawa na upendo kwa Yehova, upendo kati yetu, na kwa marafiki wa kale na wapya. Miezi miwili tuliyokaa Patterson Paul alipokuwa akipokea mazoezi ilikuwa jambo kuu katika maisha yetu kufikia sasa. Kutazama tengenezo la Yehova la kidunia kwa ukaribu kuliimarisha imani yangu niliyopitishiwa ikiwa sehemu ya urithi wangu wa kiroho wenye thamani: Hili kwa kweli ndilo tengenezo la Mungu. Ni shangwe kama nini kuwa sehemu ya tengenezo hilo hata kama ni sehemu ndogo!

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 44 Ona Mnara wa Mlinzi, Februari 15, 1952 la Kiingereza, ukurasa wa 128.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Pamoja na Ed Hooper muda mfupi kabla ya mkusanyiko wa St. Louis wa 1941, nilikopokea nakala yangu ya kitabu “Children”

[Picha katika ukurasa wa 26]

Babu katika 1948

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kwenye shamba la Howell wazazi wangu (kwenye duara) walipooana

[Picha katika ukurasa wa 27]

Wanafunzi wa Biblia wanane waliofungwa kimakosa mwaka wa 1918 (Babu akiwa amesimama mwisho kulia)

[Picha katika ukurasa wa 29]

Mizigo yetu yote ilitoshea katika “Volkswagen” yetu

[Picha katika ukurasa wa 29]

Pamoja na mume wangu, Paul