Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maadili Yanazidi Kupotoka

Maadili Yanazidi Kupotoka

Maadili Yanazidi Kupotoka

“JAMBO la namna hiyo halikuwa likitokea kamwe,” akasema Helmut Schmidt, aliyekuwa waziri mkuu wa Ujerumani. Alikuwa akisikitikia ukosefu mkubwa wa unyofu miongoni mwa maofisa wa umma ambao umekuwa habari motomoto magazetini. “Viwango vya maadili vimepotea kwa sababu ya pupa,” akasema.

Wengi watakubaliana naye. Maadili yanayotegemea Neno la Mungu Biblia, na ambayo kwa muda mrefu yamekubaliwa katika sehemu nyingi kuwa mwongozo wa kupambanua mema na mabaya yanazidi kupuuzwa. Hali iko hivyo hata katika nchi zinazoitwa eti za Kikristo.

Je, Maadili ya Biblia Yanatuhusu?

Maadili yanayotegemea mafundisho ya Biblia yanatia ndani unyofu na uaminifu-maadili. Hata hivyo, ulaghai, ufisadi, na udanganyifu umeenea kote. Gazeti The Times la London laripoti kuwa inadaiwa kwamba “wapelelezi fulani waliiba takriban pauni 100,000 wakati fulani ili kuchukua dawa za kulevya zilizokuwa zimenaswa na polisi na kuwapa wahalifu waziuze tena au kupoteza ushahidi wa kuwashtaki wahalifu mashuhuri.” Inasemekana kwamba katika Austria udanganyifu wa bima ni zoea la kawaida. Nchini Ujerumani wanasayansi walishangaa wakati ambapo hivi karibuni watafiti waligundua “mojawapo ya kashfa mbaya zaidi miongoni mwa wanasayansi Wajerumani.” “Mhusika mkuu miongoni mwa wataalamu Wajerumani wa jeni” ambaye ni profesa, alishtakiwa kwa kubuni au kupotosha habari kwa kiasi kikubwa.

Maadili yanayotegemea Biblia pia yanatia ndani uaminifu katika ndoa ambayo yapasa kuwa uhusiano wa kudumu. Lakini wenzi wengi wanazidi kutalikiana. Gazeti la Katoliki Christ in der Gegenwart (Mkristo wa Kisasa) laripoti kwamba “hata miongoni mwa raia Waswisi ‘wasiopendelea mabadiliko,’ ndoa nyingi zinazidi kuvunjika.” Nchini Uholanzi, asilimia 33 ya ndoa zote huishia katika talaka. Bibi mmoja ambaye ameona mabadiliko ya kijamii nchini Ujerumani katika miaka michache iliyopita, alionyesha hangaiko lake alipoandika hivi: “Sasa ndoa inaonwa kuwa ya kikale. Watu hawafungi ndoa tena na mwenzi wa maisha.”

Kwa upande mwingine, mamilioni huviona viwango vya maadili vinavyofundishwa katika Biblia kuwa vyenye kutegemeka na vyenye kutumika katika maisha ya ulimwengu wetu wa kisasa. Wenzi fulani waliofunga ndoa ambao wanaishi kwenye mpaka wa Uswisi na Ujerumani waligundua kwamba kuishi kupatana na maadili ya Biblia kuliwafanya wawe wenye furaha zaidi. Kulingana na wenzi hao, “kuna mwongozo mmoja tu wa maisha. Mwongozo huo ni Biblia.”

Wewe waonaje? Je, Biblia yaweza kuandaa mwongozo wenye thamani? Je, maadili yanayotegemea Biblia yanafaa leo?