Madhara ya Vita
Madhara ya Vita
“VITANI hakuna washindi,” akasema askari mmoja wa zamani aliyepigana katika Vita ya Ulimwengu ya Pili. “Ni washinde tu.” Wengi wanakubaliana naye. Madhara ya vita yanaogofya; washindi hali kadhalika washinde huteseka sana. Hata baada ya mapigano ya kutumia silaha kukoma, mamilioni huendelea kuteseka kutokana na madhara mabaya sana ya vita.
Madhara gani? Vita inaweza kuangamiza watu wengi, ikiacha mayatima na wajane wengi. Waokokaji wengi hupatwa na madhara mabaya sana ya kimwili na kiakili. Huenda mamilioni wakaachwa fukara au wakalazimika kuwa wakimbizi. Je, tunaweza kuwazia chuki na majonzi ambazo lazima zidumu katika mioyo ya wale wanaookoka mapigano hayo?
Madhara Yanayozidi Kuchochea Chuki
Madhara yanayosababishwa na vita katika mioyo ya watu huendelea kuchochea chuki muda mrefu baada ya mapigano kwisha na askari kurudi nyumbani. Vizazi vinavyofuata vyaweza kuchukiana sana. Kwa njia hiyo madhara ya vita moja yaweza kusababisha vita nyingine.
Kwa mfano, mkataba uitwao Treaty of Versailles, uliotiwa sahihi mwaka wa 1919 ili kumaliza rasmi Vita ya Ulimwengu ya Kwanza, uliwekea Ujerumani masharti ambayo raia wake waliyaona kuwa makali na ya kulipiza kisasi. Kichapo The Encyclopædia Britannica chasema kwamba masharti ya mkataba huo “yalifanya Wajerumani wawe na chuki, ambayo iliwachochea watake kulipiza kisasi.” Miaka kadhaa baadaye, “chuki kwa mkataba huo wa amani iliandalia Hitler msingi,” ikawa mojawapo ya mambo yaliyosababisha Vita ya Ulimwengu ya Pili.
Vita ya Ulimwengu ya Pili ilianza Poland na kuenea kutia ndani nchi za Balkani. Madhara ambayo makabila mbalimbali katika eneo hilo yalisababishiana katika miaka ya 1940 yalichangia kuanza kwa vita katika nchi za Balkani katika miaka ya 1990. “Hali yenye kuendelea ya chuki na kulipiza kisasi imezidi kuwa mbaya hadi wakati wetu,” likasema gazeti la Ujerumani liitwalo Die Zeit.
Kwa kweli, ni lazima madhara ya vita yamalizwe ikiwa mwanadamu ataishi kwa amani. Jambo hilo laweza kutimizwaje? Ni nini kiwezacho kufanywa kuondoa chuki na majonzi? Ni nani awezaye kumaliza madhara ya vita?
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 2]
COVER: Fatmir Boshnjaku
[Picha katika ukurasa wa 3]
U.S. Coast Guard photo; UN PHOTO 158297/J. Isaac