Cyril na Methodius Watafsiri wa Biblia Waliobuni Alfabeti
Cyril na Methodius Watafsiri wa Biblia Waliobuni Alfabeti
“Taifa letu limebatizwa na bado hatuna mwalimu. Hatuelewi Kigiriki wala Kilatini. . . . Hatuelewi herufi zilizoandikwa wala maana yake; kwa hiyo tutumieni walimu ambao wanaweza kutufahamisha maneno ya Maandiko na maana yake.”—Rostislav, mkuu wa Moravia, mwaka wa 862 W.K.
LEO, watu zaidi ya milioni 435 ambao huzungumza lugha za jamii ya Waslavonia wanaweza kupata Biblia katika lugha yao ya kienyeji. * Watu milioni 360 kati yao hutumia alfabeti ya Cyril. Hata hivyo, karne 12 zilizopita hakukuwa na lugha iliyoandikwa wala alfabeti katika lahaja za mababu wao wa kale. Watu waliosaidia kurekebisha hali hiyo waliitwa Cyril na Methodius, ambao walikuwa ndugu wa kimwili. Watu wanaopenda Neno la Mungu wataona kwamba jitihada za ujasiri na uvumbuzi wa ndugu hao wawili ni muhimu sana katika historia ya kuhifadhi na kuendeleza Biblia. Wanaume hao walikuwa nani, nao walikabili vizuizi gani?
“Mwana-Falsafa” na Gavana
Cyril (aliyeishi mwaka wa 827-869 W.K., ambaye mwanzoni aliitwa Constantine) na Methodius (aliyeishi mwaka wa 825-885 W.K.) walizaliwa katika familia mashuhuri huko Thesalonike, Ugiriki. Wakati huo wakazi wa jiji la Thesalonike walizungumza lugha mbili; Kigiriki na aina fulani ya Kislavonia. Kuwepo kwa Waslavonia wengi na ushirikiano wa karibu kati ya raia wa Thesalonike na jumuiya za Waslavonia waliokuwa karibu huenda kuliwawezesha Cyril na Methodius kujua kindani lugha ya Waslavonia wa kusini. Naye mwandishi mmoja wa wasifu wa Methodius hata anataja kwamba mama yao alikuwa Mslavonia.
Baada ya kifo cha babaye, Cyril alihamia Constantinople, jiji kuu la Milki ya Byzantium. Huko alisomea kwenye chuo kikuu cha kifalme na kushirikiana na walimu maarufu. Alipata kuwa msimamizi wa maktaba ya Hagia Sophia, kanisa maarufu sana huko Mashariki, na baadaye akawa profesa wa falsafa. Kwa kweli, Cyril alipewa jina la utani, Mwana-Falsafa, kutokana na mafanikio yake kielimu.
Wakati huohuo, Methodius alifuatia kazi ileile aliyofanya babake—usimamizi wa kisiasa. Alifikia cheo cha gavana katika wilaya ya Byzantium ambako Waslavonia wengi waliishi. Hata hivyo, aliondoka huko na kwenda kukaa kati
ka nyumba ya utawa huko Bithinia, Asia Ndogo. Cyril alijiunga naye huko mwaka wa 855 W.K.Katika mwaka wa 860 W.K., askofu mkuu wa Constantinople aliwatuma ndugu hao wawili kwenda kufanya kazi katika nchi ya kigeni. Walitumwa kwa Wakhazar, walioishi kaskazini-mashariki mwa Bahari Nyeusi, ambao walisitasita kuamua kati ya Uislamu, Dini ya Kiyahudi, na Ukristo. Alipokuwa njiani kwenda huko, Cyril alikaa kwa muda fulani huko Chersonese, Krimea. Wasomi fulani wanaamini kwamba alijifunza Kiebrania na Kisamaria alipokuwa huko na kwamba alitafsiri kitabu cha sarufi ya Kiebrania katika lugha ya Wakhazar.
Mwito Kutoka Moravia
Katika mwaka wa 862 W.K., Rostislav, mkuu wa Moravia (ambayo sasa ni Cheki ya mashariki, Slovakia ya magharibi, na Hungaria ya magharibi), alimpelekea Maliki Michael wa Tatu wa Byzantium ombi lililoko katika fungu la kwanza, akitaka walimu wa Maandiko watumwe huko. Raia wa Moravia wenye kuzungumza Kislavonia walikuwa tayari wamejulishwa mafundisho ya kanisa na mishonari kutoka ufalme wa Frank Mashariki (ambayo sasa ni Ujerumani na Austria). Hata hivyo, Rostislav, alihangaikia uvutano wa kisiasa na wa kidini wa makabila ya Kijerumani. Alitumaini kwamba uhusiano wa kidini na Constantinople ungesaidia taifa lake kuendelea kuwa huru kisiasa na kidini.
Maliki huyo aliamua kutuma Methodius na Cyril kwenda Moravia. Ndugu hao wawili walistahili kitaaluma, kielimu, na kilugha, kuongoza kazi hiyo. Mwandishi mmoja wa wasifu wa karne ya tisa atuambia kwamba maliki aliwahimiza waende Moravia kwa kusababu nao hivi: “Nyote ni wenyeji wa Thesalonike, na Wathesalonike wote huongea Kislavonia sanifu.”
Alfabeti na Tafsiri ya Biblia Zaanzishwa
Wakati wa miezi iliyotangulia kuondoka kwao, Cyril alijitayarisha kwa ajili ya kazi hiyo kwa kuwaandikia Waslavonia alfabeti fulani. * Imesemekana kwamba alikuwa makini sana kuhusu matamshi. Kwa hiyo, akitumia herufi za Kigiriki na Kiebrania, alijaribu kutokeza herufi kwa kila sauti katika matamshi ya Kislavonia. Watafiti fulani wanaamini kwamba tayari alikuwa ametumia miaka mingi akifanya matayarisho ya msingi ya alfabeti hiyo. Na bado kuna shaka kuhusu aina ya alfabeti ambayo Cyril alibuni.—Ona sanduku “Ni Alfabeti ya Cyril au ya Glagol?”
Wakati huohuo Cyril alianzisha programu ya
haraka ya kutafsiri Biblia. Kulingana na desturi, alianza kwa kutafsiri maneno ya kwanza ya Gospeli ya Yohana katika Kislavonia kutoka Kigiriki, akitumia alfabeti iliyokuwa imetoka tu kubuniwa: “Hapo mwanzo kulikuwako Neno . . .” Cyril aliendelea kutafsiri zile Gospeli nne, barua za Paulo, na kitabu cha Zaburi.Je, alifanya kazi hiyo peke yake? Inaelekea sana kwamba Methodius alimsaidia. Isitoshe, kitabu The Cambridge Medieval History chasema: “Yaelekea sana kwamba [Cyril] alikuwa na watu wengine waliomsaidia, ambao ni lazima hasa wawe walikuwa Waslavonia walioelimishwa huko Ugiriki. Tukichunguza tafsiri za zamani zaidi, . . . tunapata uthibitisho bora wa Kislavonia cha hali ya juu, jambo linaloonyesha kwamba ni lazima Waslavonia wawe walihusika.” Sehemu iliyosalia ya Biblia ilikamilishwa na Methodius kama tutakavyoona.
“Kama Kunguru Washambuliavyo Kipanga”
Katika mwaka wa 863 W.K., Cyril na Methodius walianza kazi yao huko Moravia, ambako walikaribishwa kwa uchangamfu. Mbali na kutafsiri Biblia na maandishi ya kawaida ya ibada na sala, kazi yao ilitia ndani pia kufundisha kikundi fulani cha wenyeji alfabeti ya Kislavonia iliyokuwa imetoka tu kubuniwa.
Hata hivyo, mambo hayakuwa rahisi. Makasisi Wafrank huko Moravia walipinga vikali matumizi ya Kislavonia. Waliamini dhana ya lugha tatu, wakisema kwamba Kilatini, Kigiriki, na Kiebrania ndizo lugha pekee zinazokubaliwa kutumika katika ibada. Ndugu hao walisafiri hadi Roma mwaka wa 867 W.K. wakitumaini kwamba papa angeunga mkono lugha yao mpya ya maandishi waliyokuwa wamebuni.
Wakiwa njiani, huko Venice, Cyril na Methodius walikabiliana tena na makasisi Walatini walioamini ile dhana ya lugha tatu. Mwandishi wa wasifu wa enzi za kati aliyeandika kuhusu Cyril atuambia kwamba maaskofu wenyeji, makasisi, na watawa walimshambulia kwa maneno “kama kunguru washambuliavyo kipanga.” Wasifu huo wasema kwamba Cyril alijibu kwa kunukuu 1 Wakorintho 14:8, 9: “Kwa maana kwa kweli, tarumbeta ikivuma wito usio dhahiri, nani atajitayarisha kwa ajili ya pigano? Katika njia hiyohiyo pia, nyinyi msipotamka usemi wenye kueleweka kwa urahisi kupitia hiyo lugha, linalosemwa litajulikanaje? Kwa kweli, mtakuwa mkisema hewani tu.”
Hatimaye ndugu hao walipofika Roma, Papa Adrian wa Pili aliwapa kibali kamili cha kutumia Kislavonia. Baada ya miezi kadhaa, na akiwa bado Roma, Cyril akawa mgonjwa sana. Alikufa baada ya muda unaopungua miezi miwili alipokuwa na umri wa miaka 42.
Papa Adrian wa Pili alimtia moyo Methodius arudi kufanya kazi huko Moravia na karibu na mji wa Nitra, sehemu ambayo sasa ni Slovakia. Akitaka kuimarisha uvutano wake juu ya eneo hilo, papa huyo alimpa Methodius barua zilizotoa kibali cha kutumia Kislavonia na kumweka kuwa askofu mkuu. Hata hivyo, katika mwaka wa 870 W.K. Hermanrich, askofu wa Frank, akisaidiwa na Svatopluk, Mkuu wa Nitra, alimkamata Methodius. Alifungwa kwa miaka miwili na nusu katika makao ya watawa huko kusini-mashariki mwa Ujerumani. Hatimaye, Papa John wa Nane, mwandamizi wa Adrian wa Pili, aliagiza Methodius aachiliwe, akamrudisha kwenye dayosisi yake, na kusisitiza tena kwamba papa aliunga mkono kutumiwa kwa Kislavonia katika ibada.
Lakini makasisi Wafrank waliendelea na upinzani wao. Methodius alijitetea kwa mafanikio dhidi ya mashtaka ya uzushi, na hatimaye akapata agizo la Papa John wa Nane, lililoidhinisha waziwazi matumizi ya Kislavonia katika kanisa. Kama papa wa sasa John Paul wa Pili akirivyo, Methodius aliishi maisha ya “kusafiri, ufukara, mateso, uhasama na mnyanyaso, . . . na hata kipindi cha kifungo chenye ukatili.” Kinyume cha matazamio, mambo hayo yalifanywa na maaskofu na wakuu ambao walipendelea Roma.
Biblia Nzima Yatafsiriwa
Licha ya upinzani usiokoma, Methodius alimaliza kutafsiri sehemu ya Biblia iliyosalia katika Kislavonia kwa kusaidiwa na waandishi kadhaa wa hatimkato. Kulingana na mapokeo, alimaliza kazi hiyo kubwa kwa muda wa miezi
minane tu. Hata hivyo, hakutafsiri vitabu vya Wamakabayo ambavyo havijathibitishwa kuwa sehemu ya Biblia.Leo, si rahisi kukadiria kisahihi ubora wa tafsiri iliyofanywa na Cyril na Methodius. Ni hati chache tu zilizoko sasa zilizoandikwa karibu na wakati walipofanya tafsiri ya kwanza. Kwa kuchunguza nakala hizo za kwanza ambazo ni nadra kupatikana, wataalamu wa lugha wanaona kwamba tafsiri hiyo ilikuwa sahihi na sahili. Kitabu Our Slavic Bible chasema kwamba “iliwabidi [ndugu hao wawili] wabuni maneno na semi nyingi mpya . . . Nao walifanya hayo yote kwa usahihi wenye kustaajabisha, wakafanya Kislavonia kiwe na msamiati usio na kifani.”
Urithi Wenye Kudumu
Baada ya kifo cha Methodius mwaka wa 885 W.K., wanafunzi wake walifukuzwa Moravia na wapinzani wao Wafrank. Walikimbilia Bohemia, Poland ya kusini, na Bulgaria. Hivyo kazi ya Cyril na Methodius iliendelezwa na hata kuenezwa. Lugha ya Kislavonia, ambayo ndugu hao wawili waliiweka katika maandishi na kuifanya iwe yenye kudumu, ilisitawi, ikakua, na baadaye ikapanuka sana. Leo, kuna lugha 13 za Kislavonia na lahaja nyingi.
Isitoshe, jitihada za ujasiri za Cyril na Methodius za kutafsiri Biblia zilifanikiwa kwa kuwa leo kuna tafsiri mbalimbali za Maandiko ya Kislavonia. Mamilioni wanaozungumza lugha hizo hunufaika kwa kuwa na Neno la Mungu katika lugha yao ya kienyeji. Licha ya upinzani mkali, maneno haya ni kweli kama nini: ‘Neno la Mungu wetu litasimama milele’!—Isaya 40:8.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 3 Lugha za Kislavonia huzungumzwa Ulaya ya Mashariki na ya Kati na zatia ndani Kirusi, lugha ya Ukrainia, Kiserbia, Kipoland, Kicheki, Kibulgaria, na lugha nyingine kama hizo.
^ fu. 13 Neno “-a Kislavonia,” kama linavyotumiwa katika makala hii, ladokeza lahaja ya Kislavonia ambayo Cyril na Methodius walitumia katika kazi yao na uandishi wao. Leo watu fulani hutumia semi “Kislavonia cha Zamani” au “Kislavonia cha Zamani cha Kanisa.” Wataalamu wa lugha hukubali kwamba katika karne ya tisa W.K., Waslavonia wote hawakuzungumza lugha moja.
[Sanduku katika ukurasa wa 29]
Ni Alfabeti ya Cyril au ya Glagol?
Muundo wa alfabeti ambayo Cyril alibuni umezusha mabishano mengi, kwa kuwa wataalamu wa lugha hawana hakika ilikuwa alfabeti gani. Ile inayoitwa alfabeti ya Cyril inategemea sana alfabeti ya Kigiriki, ikiwa na angalau herufi 12 zaidi zilizobuniwa ili kutokeza sauti za Kislavonia ambazo zilikosekana katika lugha ya Kigiriki. Hata hivyo, hati za awali zaidi za Kislavonia hutumia alfabeti tofauti kabisa, inayojulikana kama alfabeti ya Glagol, ambayo wasomi wengi huamini kwamba ndiyo alfabeti iliyobuniwa na Cyril. Yaonekana kama herufi kadhaa za alfabeti hiyo ya Glagol zatokana na Kigiriki au Kiebrania ambacho huandikwa kwa herufi zenye kuunganishwa. Huenda nyingine zatokana na herufi zenye alama za matamshi za enzi za kati, lakini nyingi ni ubuni wa kwanza ambao ni tata. Alfabeti ya Glagol yaonekana kuwa ndiyo ubuni wa kwanza na wa pekee sana. Hata hivyo, alfabeti ya Cyril ndiyo imesitawi na kutokeza herufi za Kirusi, lugha ya Ukrainia, Kiserbia, Kibulgaria, na Kimakedonia, mbali na lugha nyingine 22 za ziada, ambazo baadhi yazo si za Kislavonia.
[Artwork—Cyrillic and Glagolitic characters]
[Ramani katika ukurasa wa 31]
Bahari ya Baltiki
(Poland)
Bohemia (Cheki)
Moravia (Cheki Ms., Slovakia Mg., Hungaria Mg.)
Nitra
UFALME WA MASHARIKI WA FRANK (Ujerumani na Austria)
ITALIA
Venice
Roma
Bahari ya Mediterania
BULGARIA
UGIRIKI
Thesalonike
(Krimea)
Bahari Nyeusi
Bithinia
Constantinople (Istanbul)
[Picha katika ukurasa wa 31]
Biblia ya Kislavonia ya mwaka wa 1581 iliyoandikwa kwa alfabeti ya Cyril
[Hisani]
Biblia: Narodna in univerzitetna knjiz̆nica-Slovenija-Ljubljana