Je, Unaweza Kuwa Mwenye Furaha Kwelikweli?
Je, Unaweza Kuwa Mwenye Furaha Kwelikweli?
GEORGE alisalimu kila mtu huku akitabasamu. Aliuona uhai kuwa zawadi ya kufurahiwa yenye thamani. Yeye alijulikana kwa furaha yake na hali yake ya kutarajia mema—hasa alipoanza kupatwa na maumivu ya uzee. George alijulikana kuwa mtu mwenye furaha hadi siku alipokufa. Je, wewe ni mwenye furaha kama George? Je, wewe huiona kila siku kuwa zawadi ya kufurahiwa? Au je, matarajio ya siku mpya hukufanya uwe na ubaridi au wasiwasi? Je, kuna kitu kinachokukosesha furaha?
Furaha imefafanuliwa kuwa hali njema ambayo kwa kadiri fulani ni yenye kudumu. Hudhihirishwa na hisia-moyo zinazotia ndani uradhi na furaha nyingi, na hudhihirishwa pia na tamaa ya asili ya kutaka hali hiyo iendelee. Je, kwa kweli kuna furaha kama hiyo?
Leo, jamii huendeleza maoni kwamba watu wangekuwa wenye furaha kama wangekuwa na utajiri wa kutosha. Mamilioni ya watu wana shughuli nyingi sana katika hekaheka zao za kuwa matajiri. Kwa kufanya hivyo wengi hupoteza mahusiano yao na wengine na mambo mengine muhimu maishani. Kama mchwa kwenye kichuguu, wanakuwa na shughuli daima za kwenda hapa na pale, na hukosa wakati wa kutafakari wanayofanya au wa kuwa na watu wengine. Inaeleweka kwamba, “watu wanaobainishwa kuwa wameshuka moyo wanaongezeka,” yasema ripoti moja katika gazeti Los Angeles Times, “na watu wanaanza kupatwa na [mshuko-moyo] wakiwa na umri mdogo zaidi. . . . Dawa za kutibu mshuko-moyo ndizo zinazouzwa kwa wingi zaidi na makampuni ya dawa.” Mamilioni ya watu hutumia dawa haramu au hujaribu kumaliza matatizo yao kwa kunywa vileo. Wengine
hutumia pesa kiholela wanaposhuka moyo. Katika uchunguzi mmoja, “wanawake ndio wanaoelekea sana kufanya ununuzi ili kujituliza,” lasema gazeti la Uingereza The Guardian. “Wanaposhuka moyo, yaelekea watafanya ununuzi mara tatu zaidi ya wanaume.”Hata hivyo, furaha ya kweli haipatikani kwa kununua vitu, kunywa, kutumia dawa za kulevya, wala kwa kuwa na akaunti ya benki. Furaha haiuzwi; hupatikana bila malipo. Tunaweza kupata wapi zawadi hiyo yenye thamani? Tutazungumzia hilo katika makala ifuatayo.