Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tulipata Msaada Imani Yetu Ilipojaribiwa

Tulipata Msaada Imani Yetu Ilipojaribiwa

Tulipata Msaada Imani Yetu Ilipojaribiwa

Vicky alikuwa msichana mwenye kupendeza sana—mwenye afya, mwenye kuvutia, na mchangamfu. Tulifurahi sana alipozaliwa katika majira ya kuchipua mwaka wa 1993. Tuliishi katika mji mdogo sehemu ya kusini mwa Sweden, na maisha yetu yalikuwa yenye furaha.

HATA hivyo, Vicky alipokuwa mwenye umri wa mwaka mmoja na nusu matatizo makubwa yalizuka. Alikuwa amekuwa mgonjwa kwa muda, hivyo tukampeleka hospitalini. Hatutasahau kamwe jinsi tulivyohisi daktari alipotuambia kwamba binti yetu ana kansa ya damu aina ya lymphoblastic, ambayo ni aina ya kansa ya utotoni inayoathiri chembe nyeupe za damu.

Ilikuwa vigumu kuelewa na kukubali kwamba msichana wetu mdogo alikuwa na ugonjwa huo mbaya. Alikuwa ameanza tu kutambua kwa kiasi fulani mambo yaliyokuwako karibu naye, na sasa labda angekufa. Daktari alijaribu kutufariji, kwa kutuambia kwamba kuna matibabu bora ambayo yanahusisha tiba ya kemikali pamoja na kuongezwa damu mara kadhaa. Ndipo tuliposhtushwa tena.

Imani Yetu Inajaribiwa

Bila shaka tulimpenda binti yetu na tulitaka apate matibabu bora. Hata hivyo, hatukuweza kukubali hata kidogo aongezwe damu. Tunaamini kabisa Neno la Mungu, Biblia, lisemalo kwa wazi kwamba ni lazima Wakristo ‘wajiepushe na damu.’ (Matendo 15:28, 29) Pia tulijua kwamba kuongeza damu ni hatari. Maelfu ya watu wameshikwa na magonjwa na kufa kwa sababu ya kuongezwa damu. Ilitubidi kutafuta tiba nyingine bora ambayo haingehusisha kuongezwa damu. Kwa hiyo, pigano letu la imani lilikuwa limeanza.

Tungeweza kufanya nini? Ili kupata msaada tuliwasiliana na idara ya Huduma za Habari za Kihospitali kwenye ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova huku Sweden. * Mara moja, habari zilipelekwa kwa njia ya faksi kwa hospitali mbalimbali kotekote Ulaya ili kutafuta hospitali na daktari aliyekuwa tayari kutibu kwa kemikali bila ya kuongeza damu. Tulitiwa moyo sana kuona bidii na upendo wa ndugu zetu Wakristo waliojitahidi kutusaidia. Kwa kweli, tulipata msaada katika pigano letu la imani.

Baada ya muda wa saa chache tu, tulipata hospitali na pia daktari jijini Homburg/Saar, Ujerumani. Mipango ilifanywa ili tusafiri huko kwa ndege siku iliyofuata ili Vicky akapimwe. Tulipowasili, ndugu zetu Wakristo wa kutaniko la Mashahidi wa Yehova wa mahali hapo, na baadhi ya watu wetu wa ukoo walikuwapo ili kutukaribisha. Na mwakilishi wa Halmashauri ya Uhusiano na Hospitali alitukaribisha kwa upendo. Aliandamana nasi tulipokwenda hospitalini na kutusaidia kwa njia zote. Tulifarijika kuona kwamba hata katika nchi ya kigeni tulikuwa na ndugu wa kiroho ambao walituunga mkono.

Tulipokutana na Dakt. Graf hospitalini, tulifarijika tena. Alikuwa mwenye huruma na kutuhakikishia kwamba angefanya yote ambayo angeweza ili kumtibu Vicky bila ya kumwongeza damu. Hata ikiwa kiwango cha madini ya chuma kingepunguka hadi gramu tano kwa desilita moja ya damu, angekuwa tayari kuendelea na matibabu bila ya kuongeza damu. Pia alisema kwamba, kutambuliwa mapema kwa ugonjwa, na kuleta Vicky haraka hospitalini kulifanya iwezekane apone. Alisema kwamba ingekuwa mara ya kwanza kwake kutibu ugonjwa huo kwa kemikali bila kuongeza damu. Tulishukuru sana, na kuthamini ujasiri na azimio la Dakt. Graf.

Matatizo ya Kifedha

Sasa swali hili lilizuka, Fedha za kulipa matibabu ya Vicky zingetoka wapi? Tuliduwaa tulipojulishwa kwamba matibabu ya miaka miwili yangegharimu fedha za Ujerumani, deutsche mark 150,000 hivi. Hatukuwa na kiasi kikubwa hivyo cha fedha, hata hivyo ilikuwa muhimu kuanza kumtibu Vicky mara moja. Kwa sababu tuliondoka Sweden ili Vicky atibiwe huko Ujerumani, hatukustahili kupokea malipo yoyote ya bima ya afya nchini Sweden. Kwa hiyo, wataalamu wa kitiba waliokuwa tayari kusaidia msichana wetu mgonjwa sana walikuwa wamepatikana, ila sisi hatukuwa na fedha za kutosha.

Hospitali ilitusaidia kwa kutujulisha kwamba matibabu yangeanza mara moja ikiwa tungelipa mark 20,000 na kutia sahihi dhamana kwa fedha zilizosalia. Tulikuwa na kiasi fulani cha fedha akibani, na kwa msaada wa marafiki na watu wa ukoo wenye upendo tuliweza kulipa mark 20,000—lakini vipi zile nyingine?

Kwa mara nyingine tulikumbushwa kwamba hatukuwa peke yetu katika pigano letu la imani. Ndugu wa kiroho, ambaye hatukumfahamu wakati huo, alikuwa tayari kulipa kiasi kilichosalia. Hata hivyo, tulifaulu kufanya mipango mingine, kwa hiyo hatukuhitaji kutegemea ukarimu wake.

Wataalamu wa Kitiba Kazini

Tiba ya kemikali ilianzishwa. Siku na majuma yalipita. Mara kwa mara, sisi na binti yetu mdogo tulihitaji kujikakamua sana kwa sababu ya hali hiyo ngumu. Kwa upande mwingine, tulifurahi sana na kushukuru kila alipokuwa na dalili ya kupata nafuu. Tiba ya kemikali iliendelea kwa muda wa miezi minane. Kiwango cha madini ya chuma cha damu ya Vicky kilipunguka hadi gramu sita kwa desilita moja ya damu, naye Dakt. Graf akatimiza ahadi yake.

Zaidi ya miaka sita imepita, na uchunguzi wa mwisho wa umajimaji wa uti wa mgongo wa Vicky hauonyeshi dalili zozote za kansa ya damu. Sasa yeye ni msichana mchangamfu ambaye hana dalili zozote za ugonjwa huo. Kupona kabisa kwa Vicky ni kama mwujiza. Tunajua kwamba watoto wengi wenye ugonjwa huo hufa hata ingawa hutibiwa kwa kemikali na pia kuongezwa damu.

Tumeshinda katika pigano letu la imani, kwa msaada wa watu wa ukoo, ndugu na dada Wakristo na wataalamu wa kitiba. Ndugu wa Huduma za Habari za Kihospitali walituunga mkono wakati wote. Dakt. Graf na madaktari wenzake walitumia ustadi wao kumsaidia Vicky kupona. Tunashukuru kwelikweli kwa hayo yote.

Imani Yetu Imeimarishwa

Zaidi ya yote, tunamshukuru Mungu wetu Yehova kwa upendo na utunzaji wake na kwa nguvu tuliyopata kwa kusoma Neno lake Biblia. Tunapokumbuka mambo hayo, tunatambua jinsi ambavyo tukio hilo gumu maishani limetufundisha mengi na jinsi lilivyoimarisha imani yetu.

Sasa tamaa ya mioyo yetu ni kudumisha uhusiano wetu wa karibu na Yehova Mungu, na kufundisha binti yetu kuona manufaa ya kuishi kwa kupatana na matakwa yake. Naam, tunataka kumpa urithi mzuri wa kiroho wa kuishi milele katika Paradiso itakayokuja hapa duniani siku zijazo.—Imechangwa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Idara ya Huduma za Habari za Kihospitali husimamia mfumo wa kimataifa wa Halmashauri za Uhusiano na Hospitali mbalimbali. Halmashauri hizo zimefanyizwa na wajitoleaji Wakristo ambao wamezoezwa kuendeleza ushirikiano baina ya madaktari na wagonjwa ambao ni Mashahidi. Kuna Halmashauri za Uhusiano na Hospitali zaidi ya 1,400 ambazo husaidia wagonjwa katika nchi zaidi ya 200.