Biblia Yafanywa Kuwa Buku Moja
Biblia Yafanywa Kuwa Buku Moja
KWA habari ya kunakiliwa kwa Biblia, Wakristo wa mapema ndio waliokuwa wa kwanza kabisa kutumia codex (kitabu kilichoandikwa kwa mkono) badala ya hatikunjo. Hata hivyo, Wakristo hawakuanza mara moja kunakili vitabu vyote vya Biblia kuwa buku moja. Katika karne ya sita Flavius Cassiodorus alichukua hatua moja muhimu ya kunakili Biblia kwa wingi zikiwa buku moja moja.
Flavius Magnus Aurelius Cassiodorus alizaliwa katika familia tajiri wapata mwaka wa 485-490 W.K. huko Calabria, kwenye ncha ya kusini mwa Italia ya leo. Aliishi kipindi chenye msukosuko sana katika historia ya Italia wakati ambapo nchi hiyo inayozungukwa na maji ilikaliwa kwanza na Wagothi, kisha na watu wa Byzantium. Alipokuwa na umri wa miaka 60 au 70 hivi, Cassiodorus alianzisha makao ya watawa ya Vivarium na maktaba karibu na makao yake huko Squillace, Calabria.
Mhariri Makini wa Biblia
Mojawapo ya mambo ambayo Cassiodorus alihangaikia zaidi ya yote ni jinsi ambavyo Biblia ingeweza kufikia watu. Mwanahistoria Peter Brown aandika, “kulingana na maoni ya Cassiodorus, vichapo vyote vya Kilatini vingetumiwa ili kufanya Maandiko yapatikane kwa watu. Vifaa vyote vilivyokuwa vimetumiwa hapo awali kujifunza na kunakili maandishi ya kale vingetumiwa ili kuyafahamu Maandiko na kuyanakili kwa busara. Utamaduni wote wa Kilatini ulipasa kuzunguka jua kubwa la Neno la Mungu kama vile mfumo wa nyota ambao umetoka tu kubuniwa.”
Cassiodorus aliwakusanya watafsiri na wanasarufi kwenye makao ya watawa ya Vivarium kusudi waunganishe vitabu vyote vya Biblia. Yeye ndiye aliyesimamia kazi iliyohitaji umakini mkubwa kuhusiana na uhariri. Aliwapa kazi hiyo wanaume wachache wenye elimu. Wanaume hao wangepaswa kuepuka kusahihisha harakaharaka mambo yaliyodhaniwa kuwa makosa ya waandishi. Ikiwa walikuwa na swali kuhusiana na sarufi, hati za kale za Biblia ndizo zingekuwa zenye kutegemeka zaidi kuliko matumizi ya kawaida ya Kilatini. Cassiodorus alitoa agizo hili: “Matumizi ya kisarufi yasiyo ya kawaida . . . yapasa kuhifadhiwa, kwa kuwa si rahisi kupotosha maandiko yanayotambuliwa kuwa yalipuliziwa. . . . Lazima njia ambayo Biblia inatumia semi fulani, mifano, na misemo, ihifadhiwe, hata ikiwa njia hiyo yaonekana kuwa isiyo ya kawaida kulingana na viwango vya lugha ya Kilatini. Majina ya ‘Kiebrania’ pia yapasa kuhifadhiwa.”—The Cambridge History of the Bible.
Maandishi ya Codex Grandior
Wanakili kwenye makao ya watawa ya Vivarium walipewa kazi ya kunakili nakala tatu tofauti za Biblia katika Kilatini. Labda mojawapo ya nakala hizo, ambayo ilikuwa na mabuku tisa, iliandikwa kwa Kilatini cha zamani. Nakala hiyo ilinakiliwa mwishoni mwa karne ya pili. Nakala ya pili ilikuwa ile ya Vulgate ya Kilatini, iliyokamilishwa na Jerome mwanzoni mwa karne ya tano. Nakala ya tatu, Codex Grandior, yaani “codex kubwa zaidi” ilinakiliwa kutoka katika Biblia tatu. Nakala hizi mbili za mwisho, Vulgate na Codex Grandior, ziliunganisha pamoja vitabu vyote vya Biblia kuwa buku moja.
Yaonekana Cassiodorus ndiye aliyekuwa wa kwanza kuunganisha Biblia za Kilatini kuwa buku * Bila shaka alitambua kwamba lilikuwa jambo la busara kuunganisha vitabu vyote vya Biblia kuwa buku moja, hivyo usomaji wa Biblia ukawa jambo lisilochukua muda mwingi.
moja moja, na kuziita pandectae.Kutoka Kusini mwa Italia Hadi Visiwa vya Uingereza
Muda mfupi baada ya kifo cha Cassiodorus (yapata mwaka wa 583 W.K.), Codex Grandior ilianza kusafirishwa. Wakati huo, inaaminika kwamba vitabu fulani vya maktaba ya Vivarium vilikuwa vimehamishwa na kupelekwa kwenye maktaba ya Lateran huko Roma. Katika mwaka wa 678 W.K., mkuu wa makao ya watawa wanaume Ceolfrith, aliyekuwa Mwingereza, alikuja na codex hiyo kwenye Visiwa vya Uingereza aliporudi kutoka Roma alikokaa kwa muda fulani. Hivyo, codex hiyo ikaletwa kwenye makao ya watawa ya Wearmouth na Jarrow, ambayo yalisimamiwa na Ceolfrith. Makao hayo yalikuwa katika eneo ambalo sasa ni Northumbria, Uingereza.
Ni lazima Biblia ya Cassiodorus, ambayo ilikuwa buku moja, iwe ilimvutia sana Ceolfrith na watawa wake, ambao yaelekea waliipenda kwa kuwa ingeweza kutumiwa kwa urahisi. Hivyo, baada ya miongo michache tu, wakanakili Biblia nyingine tatu nzima kuwa buku moja moja. Kati ya nakala hizo tatu, nakala kubwa sana iitwayo Codex Amiatinus ndiyo pekee inayoweza kupatikana. Ina kurasa 2,060 za karatasi ya ngozi zenye urefu wa sentimeta 51 na upana wa sentimeta 33. Buku hilo, kutia ndani jalada lake, lina upana wa sentimeta 25 na uzito wa kilogramu 34. Hiyo ndiyo Biblia ya zamani zaidi ya Kilatini inayopatikana ikiwa buku moja. Mtaalamu mmoja maarufu wa mambo ya Biblia wa karne ya 19, Fenton J. A. Hort aliitambulisha codex hiyo mwaka wa 1887. Hort alieleza: “[Hati] hiyo ya ajabu inaweza kuduwaza hata mtu wa kisasa.”
Yarudishwa Italia
Ile Codex Grandior ya kwanza ambayo Cassiodorus aliagiza inakiliwe imepotea. Lakini Codex Amiatinus iliyonakiliwa Uingereza, ilirudishwa Italia punde tu baada ya kukamilishwa. Muda mfupi kabla ya kufa, Ceolfrith aliamua kurudi Roma. Alibeba moja kati ya hati zake tatu za Biblia ya Kilatini kumpelekea Papa Gregory wa Pili zikiwa zawadi. Ceolfrith alikufa akiwa safarini mwaka wa 716 W.K., huko Langres, Ufaransa. Lakini wasafiri wenzake wakabeba hati hiyo ya Biblia katika safari yao. Hatimaye codex hiyo ikawa mojawapo ya vitabu vya maktaba ya makao ya watawa ya Mlima Amiata, huko Italia ya kati ambako inaitwa Codex Amiatinus. Mwaka wa 1782 hati hiyo ya Biblia ilipelekwa kwenye Maktaba ya Medicean-Laurentian huko Florence, Italia, na imekuwa mojawapo ya vitabu vyenye thamani kubwa katika maktaba hiyo.
Tumeathiriwaje na Codex Grandior? Tangu wakati wa Cassiodorus, wanakili na wachapaji wamependelea sana kuitoa Biblia ikiwa buku moja moja. Hata wakati huu, kuwa na Biblia ikiwa buku moja kumefanya iwe rahisi watu kuisoma na hivyo kunufaika na nguvu zake maishani mwao.—Waebrania 4:12.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 9 Yaonekana Biblia nzima katika Kigiriki zilikuwa zikitumiwa tangu karne ya nne au ya tano.
[Ramani katika ukurasa wa 29]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Safari ya Codex Grandior
Vivarium makao ya watawa
Roma
Jarrow
Wearmouth
Safari ya Codex Amiatinus
Jarrow
Wearmouth
Ml. Amiata
Florence
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 30]
Juu: “Codex Amiatinus” Kushoto: Picha ya Ezra katika “Codex Amiatinus”
[Hisani]
Biblioteca Medicea Laurenziana, Firenze