Miti Inayodumu Muda Mrefu
Miti Inayodumu Muda Mrefu
Haielekei kwamba mwamba ni mahali pazuri pa kuishi, hasa ikiwa mwamba huo upo juu ya mlima mrefu. Hata hivyo, ijapokuwa wanadamu hawangeweza kuishi sehemu kama hiyo, miti mingine inakua katika miamba ya milima ya alps ikuvumilia majira ya baridi kali na ukame wa majira ya kiangazi.
KWA kawaida, miti hiyo si mikubwa kama miti inayokua sehemu za chini. Mashina yake yanaweza kuwa na vifundo vingi venye mikunjo-mikunjo, nayo si mirefu. Ukuzi wa miti hiyo unazuiwa na baridi kali na kwa sababu inakua katika udongo mchache sana.
Huenda ukadhani kwamba miti hiyo haiwezi kudumu muda mrefu kwa sababu inakua katika mazingira magumu kushinda mazingira mengine duniani. Hata hivyo, inadumu kwa muda mrefu sana. Watu fulani wasema kwamba msonobari mmoja aina ya bristlecone, uitwao Methuselah, ambao unakua kwenye kimo cha meta 3,000 juu ya usawa wa bahari katika milima ya White Mountains huko California una umri wa miaka 4,700. Kitabu The Guinness Book of Records 1997 chasema kwamba mti huo ndio mti wa kale zaidi duniani. Edmund Schulman aliyechunguza miti hiyo ya kale alisema hivi: ‘Yaelekea msonobari aina ya bristlecone hudumu muda mrefu kwa sababu ya mazingira magumu. [Misonobari] yote yenye umri mkubwa katika White Mountains inakua kwenye kimo cha meta 3,000 katika pori kame lenye miamba.’ Schulman aligundua pia kwamba misonobari yenye umri mkubwa sana ya aina nyingine, vilevile inakua katika mazingira magumu.
Ijapokuwa mazingira magumu, miti hiyo inafaidika hasa kwa mambo mawili. Inakua mahali pasipo na miti na mimea mingine na kwa hiyo haiathiriwi na mioto ya msitu, ambayo ni hatari kubwa kwa miti iliyokomaa. Na mizizi yake inashikilia mwamba kwa uthabiti hivi kwamba ni tetemeko la ardhi tu linaloweza kuitikisa.
Watumishi waaminifu wa Mungu wanalinganishwa na miti katika Biblia. (Zaburi 1:1-3; Yeremia 17:7, 8) Hata hao wanapatwa na magumu kwa sababu ya hali zinazowakumba. Mnyanyaso, afya mbaya, au umaskini zinaweza kujaribu imani, hasa majaribu hayo yanapoendelea mwaka baada ya mwaka. Hata hivyo, Muumba aliyeumba miti ambayo inaweza kukua katika hali ngumu anawahakikishia wanaomwabudu kwamba atawaimarisha. Biblia inawaahidi wale wanaosimama imara hivi: “Atawafanya imara, atawafanya kuwa wenye nguvu.”—1 Petro 5:9, 10.
Kitenzi cha Kigiriki ambacho mara nyingi hutafsiriwa “kuvumilia” katika Biblia chamaanisha ‘kuwa thabiti, kusimama imara, au kustahimili.’ Miti ya milima ya Alps inahitaji mizizi thabiti ili idumu. Wakristo kwa upande wao, wanahitaji imani thabiti katika Yesu Kristo ili wasimame imara. Paulo aliandika hivi: “Kama ambavyo mmempokea Kristo Yesu Bwana, endeleeni kutembea katika muungano na yeye, mkiwa wenye kutia mizizi na kujengwa katika yeye na kuimarishwa katika imani, kama vile mlivyofundishwa, mkifurikwa na imani katika utoaji-shukrani.”—Wakolosai 2:6, 7.
Paulo alifahamu vizuri umuhimu wa kuwa na mizizi imara ya kiroho. Yeye mwenyewe alikuwa na “mwiba katika mwili,” na alivumilia mnyanyaso mkali muda wote wa huduma yake. (2 Wakorintho 11:23-27; 12:7) Lakini aliona kwamba kwa nguvu ya Mungu aliweza kuendelea. “Kwa mambo yote ninayo nguvu kwa njia ya yeye anipaye nguvu,” akasema.—Wafilipi 4:13.
Mfano wa Paulo unaonyesha kwamba Wakristo wanaweza kuvumilia licha ya hali ngumu. Kama vile miti ya milima ya Alps inavyoweza kuvumilia dhoruba kwa mamia ya miaka, sisi tunaweza kusimama imara katika imani tukiwa na imani thabiti katika Kristo na kutumaini nguvu tunayopokea kutoka kwa Mungu. Zaidi ya hayo, tukivumilia hadi mwisho, tutakuja pia kuona utimizo wa ahadi hii ya Mungu: “Kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu.”—Isaya 65:22; Mathayo 24:13.