Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Je, Kuna Uhai Baada ya Kifo?

Je, Kuna Uhai Baada ya Kifo?

Je, Kuna Uhai Baada ya Kifo?

“MTU akifa, je! atakuwa hai tena?” akauliza mzee wa kale Ayubu, yapata miaka 3,500 iliyopita. (Ayubu 14:14) Swali hilo limetatanisha wanadamu kwa maelfu ya miaka. Katika vizazi vyote vilivyopita, watu wa jamii zote wametafakari jambo hilo nao wamekisia mambo mbalimbali.

Wengi waitwao Wakristo huamini kuna mbingu na mahali pa moto wa mateso. Kwa upande ule mwingine, Wahindi huamini kuzaliwa upya katika umbo jingine. Akieleza maoni ya Waislamu kuhusu jambo hilo, Emir Muawiyah, msaidizi kwenye kituo cha kidini cha Kiislamu, asema hivi: “Twaamini kwamba kutakuwa na siku ya kiyama baada ya kifo, utakapokwenda mbele za Mungu, Allah, na itakuwa hasa kama kwenda kotini.” Kulingana na imani ya Kiislamu, ndipo Allah atakapokagua maisha ya kila mtu na kumpeleka ama kwenye paradiso ama motoni.

Huko Sri Lanka, Wabudha na Wakatoliki huacha milango yao na madirisha yao wazi kabisa mtu anapokufa katika familia zao. Taa ya mafuta huwashwa, na sanduku la mfu huwekwa miguu ikiangalia upande wa mlango wa mbele. Wao huamini kwamba, hatua hizo hurahisisha roho ya mfu kwenda zake.

Kulingana na Ronald M. Berndt wa Chuo Kikuu cha Western Australia, Wenyeji wa Australia (Waaborijini) huamini kwamba “binadamu wana roho isiyoweza kuharibiwa.” Makabila fulani ya Kiafrika huamini kwamba baada ya kifo watu wa kawaida huwa mazimwi, ilhali watu mashuhuri huwa roho za wazazi wa kale ambao wataheshimiwa na kuombwa dua wakiwa viongozi wasioonekana wa jamii.

Katika nchi nyingine, imani zinazohusu wafu ni mchanganyiko wa desturi za mahali hapo na ule uitwao eti Ukristo. Kwa mfano, miongoni mwa Wakatoliki na Waprotestanti wengi huko Afrika Magharibi, ni desturi ya hapo kufunika vioo mtu anapokufa ili mtu yeyote asivitazame na kuona roho ya mtu aliyekufa.

Kwa kweli, watu hutoa majibu mbalimbali kwa swali hili, ‘Ni nini ambacho hutupata tunapokufa?’ Hata hivyo, imani moja iliyo ya kawaida ni hii: Kuna kitu ndani ya mtu ambacho hakifi nacho huendelea kuishi baada ya kifo. Watu wengine huamini “kitu” hicho ni roho. Kwa mfano, sehemu fulani za Afrika, Asia na maeneo yote ya Pasifiki ya Polynesia, Melanesia, na Mikronesia, watu wengi huamini kwamba ni roho isiyoweza kufa, na si nafsi. Hata lugha kadhaa hazina neno “nafsi.”

Je, kuna roho ndani ya mtu aliye hai? Je, roho hiyo kweli huuacha mwili mtu anapokufa? Ikiwa ndivyo ilivyo, ni nini ambacho huipata? Na kuna tumaini gani kwa wafu? Maswali hayo hayapaswi kupuuzwa. Iwe ulilelewa katika utamaduni gani au dini gani, kifo ni jambo hakika ambalo lazima likabiliwe. Masuala hayo yanakuhusu sana kibinafsi. Twakutia moyo uyachunguze.