Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mwe na Imani Kama ya Abrahamu!

Mwe na Imani Kama ya Abrahamu!

Mwe na Imani Kama ya Abrahamu!

“Wale washikamanao sana na imani ndio wale walio wana wa Abrahamu.” —WAGALATIA 3:7.

1. Abramu alikabilianaje na jaribu jingine nchini Kanaani?

ABRAMU alikuwa ameacha maisha ya anasa huko Uru kwa kutii amri ya Yehova. Matatizo aliyopata katika miaka iliyofuata yalikuwa mwanzo tu wa jaribu la imani alilokabili huko Misri. Simulizi la Biblia lasema: “Kulikuwa njaa katika nchi ile.” Ingekuwa rahisi kama nini kwa Abramu kulalamika kwa sababu ya hali yake! Badala yake alichukua hatua zifaazo kuruzuku familia yake. “Abramu akashuka Misri, akae huko kwa muda maana njaa ilikuwa nzito katika nchi.” Jamaa ya Abramu ingetambuliwa kwa urahisi nchini Misri kwa kuwa ilikuwa kubwa. Je, Yehova angetimiza ahadi zake na kumlinda Abramu asipatwe na madhara?—Mwanzo 12:10; Kutoka 16:2, 3.

2, 3. (a) Kwa nini Abramu hakutaka ijulikane Sarai alikuwa nani? (b) Abramu alimtendeaje mkewe kwa kuzingatia hali ilivyokuwa?

2 Twasoma hivi kwenye Mwanzo 12:11-13: “Ikawa alipokuwa karibu kuingia Misri, akamwambia Sarai mkewe, Tazama, najua ya kuwa u mwanamke mzuri wa uso; basi itakuwa, Wamisri watakapokuona watasema, Huyu ni mkewe; kisha wataniua mimi na wewe watakuacha hai. Tafadhali useme, wewe u ndugu [“dada,” NW] yangu, iwe heri kwangu kwa ajili yako, na nafsi yangu iishi kwa ajili yako.” Ingawa Sarai alikuwa na umri uliozidi miaka 65, bado alikuwa mrembo sana. Jambo hilo lilihatarisha maisha ya Abramu. * (Mwanzo 12:4, 5; 17:17) Jambo lililokuwa muhimu zaidi ni kwamba mambo yaliyohusiana na makusudi ya Yehova yalihusika, kwa kuwa alikuwa amesema kwamba kupitia mbegu ya Abramu mataifa yote ya dunia yangejibariki. (Mwanzo 12:2, 3, 7) Kwa kuwa Abramu hakuwa na mtoto, ilikuwa muhimu sana aendelee kuishi.

3 Abramu alizungumza na mkewe kuhusu kutumia mbinu waliyokuwa wamekubaliana hapo awali, yaani, aseme yeye ni dada yake. Ona kwamba ingawa Abramu alikuwa na mamlaka akiwa mzee wa ukoo, hakutumia cheo chake vibaya, bali alitafuta msaada wa mke wake na vilevile kuungwa mkono naye. (Mwanzo 12:11-13; 20:13) Katika jambo hilo, Abramu aliweka kielelezo kizuri kwa waume kutumia ukichwa kwa upendo, naye Sarai aliwawekea wanawake wa leo kielelezo kwa kuwa mtiifu.—Waefeso 5:23-28; Wakolosai 4:6.

4. Watumishi waaminifu wa Mungu leo wanapaswa kutendaje wakati maisha ya ndugu zao yanapokuwa hatarini?

4 Sarai angeweza kusema kwamba alikuwa dada ya Abramu kwa sababu alikuwa kwa kweli dadake wa kambo. (Mwanzo 20:12) Isitoshe, haikuwa lazima atoe habari kwa watu ambao hawakustahili kuambiwa habari hizo. (Mathayo 7:6) Watumishi waaminifu wa Mungu wa siku hizi hutii amri ya Biblia ya kuwa wanyofu. (Waebrania 13:18) Kwa mfano, hawawezi kamwe kuapa kusema kweli kisha waseme uwongo mahakamani. Hata hivyo, wakati maisha ya ndugu zetu yanapokuwa hatarini kiroho na kimwili, kama wakati wa mnyanyaso au msukosuko wa kiraia, wao hutii ushauri wa Yesu wa kuwa “wenye hadhari kama nyoka na bado kuwa wasio na hatia kama njiwa.”—Mathayo 10:16; ona Mnara wa Mlinzi, Novemba 1, 1996, ukurasa wa 18, fungu la 19.

5. Kwa nini Sarai alikuwa tayari kukubali ombi la Abramu?

5 Sarai aliitikiaje ombi la Abramu? Mtume Petro anafafanua wanawake kama yeye kuwa ‘walitumaini katika Mungu.’ Kwa hiyo Sarai alifahamu masuala ya kiroho yaliyohusika. Licha ya hayo, Sarai alimpenda na kumheshimu mume wake. Hivyo aliamua ‘kujitiisha mwenyewe kwa mume wake’ na kuficha kwamba alikuwa ameolewa. (1 Petro 3:5) Bila shaka, kufanya hivyo kulihatarisha maisha ya Sarai. “Basi ikawa Abramu alipofika Misri, Wamisri wakamwona huyo mwanamke ya kwamba yeye ni mzuri sana. Wakuu wa Farao wakamwona, nao wakamsifu kwa Farao; basi yule mwanamke akachukuliwa nyumbani mwa Farao.”—Mwanzo 12:14, 15.

Ukombozi wa Yehova

6, 7. Abramu na Sarai walijikuta katika hali gani zenye kuhuzunisha, naye Yehova alimwokoaje Sarai?

6 Jambo hilo liliwahuzunisha kama nini Abramu na Sarai! Ilionekana kwamba Sarai alikuwa karibu kunajisiwa. Isitoshe, kwa kutojua kwamba Sarai alikuwa ameolewa, Farao alimpa Abramu zawadi nyingi sana, hivi kwamba “alikuwa na kondoo na ng’ombe , na punda waume, na watumwa, na wajakazi, na punda wake, na ngamia.” * (Mwanzo 12:16) Ni lazima Abramu awe alichukizwa kama nini na zawadi hizo! Ingawa hali zilionekana kuwa mbaya, Yehova hakuwa amemwacha Abramu.

7 “Lakini BWANA akampiga Farao na nyumba yake mapigo makuu, kwa ajili ya Sarai, mkewe Abramu.” (Mwanzo 12:17) Kwa njia fulani ambayo haikufichuliwa, Farao alijulishwa kilichosababisha “mapigo” hayo. Alichukua hatua mara moja: “Ndipo Farao akamwita Abramu, akasema, N’nini hili ulilonitenda? Mbona hukuniambia ya kuwa huyo ni mkeo? Mbona ulisema huyo ni umbu langu, hata nikamtwaa kuwa mke wangu? Basi sasa, huyo mke wako umchukue, uende zako. Farao akawaagiza watu kwa ajili yake, wakampeleka njiani, na mkewe, na kila alichokuwa nacho.”—Mwanzo 12:18-20; Zaburi 105:14, 15.

8. Leo Yehova anaahidi Wakristo ulinzi wa aina gani?

8 Leo, Yehova hatuahidi ulinzi kutokana na madhara ya kifo, uhalifu, njaa, au misiba ya asili. Tumepewa ahadi kwamba sikuzote Yehova atatulinda na mambo yanayoweza kuhatarisha hali yetu ya kiroho. (Zaburi 91:1-4) Yeye hufanya hivyo hasa kwa kututolea maonyo wakati ufaao kupitia Neno lake na “mtumwa mwaminifu na mwenye busara.” (Mathayo 24:45) Vipi tisho la kifo kutokana na mnyanyaso? Ingawa watu mmoja-mmoja wanaweza kuachwa wafe, Mungu hataruhusu kamwe watu wake wote wauawe. (Zaburi 116:15) Na ikiwa waaminifu fulani watakufa, tunaweza kuwa na hakika kwamba watafufuliwa.—Yohana 5:28, 29.

Kujidhabihu ili Kudumisha Amani

9. Ni nini kinachoonyesha kwamba Abramu aliishi maisha ya kuhamahama huko Kanaani?

9 Kwa kuwa njaa iliyokuwa Kanaani ilikuwa imeisha, “Abramu akarudi kutoka Misri, akaingia upande wa Negebu [eneo kavu lililo kusini ya milima ya Yuda]. Alikuwa na mkewe na mali yake yote pamoja na Loti. Wakati huo, Abramu alikuwa ametajirika sana. Alikuwa na mifugo, fedha na dhahabu.” (Mwanzo 13:1, 2, BHN) Hivyo wakazi wa Negebu wangemwona kuwa mtu mwenye uwezo sana, mkuu mwenye nguvu. (Mwanzo 23:6) Abramu hakutamani kukaa huko na kujihusisha na siasa za Wakanaani. Badala yake, ‘aliendelea kusafiri toka eneo la Negebu hadi Betheli. Alifika mahali alipokuwa amepiga kambi ya hema hapo awali, kati ya Betheli na Ai.’ Kama kawaida, Abramu aliiona ibada ya Yehova kuwa muhimu kokote alikokwenda.—Mwanzo 13:3, 4, BHN.

10. Ni tatizo gani lililotokea baina ya wachungaji wa Abramu na Loti, na ni kwa nini ilifaa tatizo hilo lisuluhishwe haraka?

10 ‘Na Loti aliyesafiri pamoja na Abramu, yeye naye alikuwa na makundi ya ng’ombe na kondoo, na hema. Na ile nchi haikuwatosha, ili wakae pamoja; maana mali zao zilikuwa nyingi, hata wasiweze kukaa pamoja. Kukawako ugomvi kati ya wachunga wanyama wa Abramu na, wachunga wanyama wa Loti; na siku zile Wakaanani na Waperizi walikuwa wakikaa katika nchi.’ (Mwanzo 13:5-7) Nchi hiyo haikuwa na maji wala malisho ya kutosha mifugo ya Abramu na ya Loti. Hivyo kukawa na ugomvi na chuki baina ya wachungaji hao. Haikufaa waabudu wa Mungu wa kweli kugombana. Iwapo ugomvi huo ungeendelea, uhusiano wao ungevunjika kabisa. Hivyo Abramu angesuluhishaje ugomvi huo? Alikuwa amechukua Loti baada ya kifo cha baba ya Loti, na labda kumlea kama mtoto wake mwenyewe. Kwa kuwa Abramu ndiye aliyekuwa na umri mkubwa zaidi kati yao wawili, je hakustahili kuchukua kilichokuwa bora zaidi?

11, 12. Abramu alimtolea Loti pendekezo gani la ukarimu, na ni kwa nini uchaguzi wa Loti haukuwa wa hekima?

11 Lakini ‘Abramu akamwambia Loti, Basi, usiwepo ugomvi, nakusihi, kati ya mimi na wewe, wala kati ya wachungaji wangu na wachungaji wako; maana sisi tu ndugu. Je! Nchi hii yote haiko mbele yako? Basi ujitenge nami, nakusihi; ukienda upande wa kushoto, nitakwenda upande wa kuume; ukienda upande wa kuume, nitakwenda upande wa kushoto.’ Karibu na Betheli kuna ile ambayo imetajwa kuwa “sehemu nzuri sana ya kutazama eneo la Palestina.” Labda ni kutoka hapo ‘Loti aliinua macho yake, akaliona Bonde lote la Yordani, ya kwamba lote pia lina maji, kabla BWANA hajaharibu Sodoma na Gomora, lilikuwa kama bustani ya BWANA, kama nchi ya Misri hapo unapokwenda Soari.’—Mwanzo 13:8-10.

12 Ingawa Biblia husema kwamba Loti alikuwa “mwadilifu,” kwa sababu fulani yeye hakumnyenyekea Abramu kwa staha kuhusiana na jambo hilo, wala haionekani kana kwamba alitafuta ushauri wa Abramu aliyekuwa na umri mkubwa zaidi. (2 Petro 2:7) ‘Loti akajichagulia Bonde lote la Yordani; Loti akasafiri kwenda upande wa mashariki; wakatengana wao kwa wao. Abramu akaa katika nchi ya Kanaani, na Loti akakaa katika miji ya lile Bonde; akajongeza hema yake mpaka Sodoma.’ (Mwanzo 13:11, 12) Mji wa Sodoma ulikuwa na ufanisi na manufaa nyingi za kimwili. (Ezekieli 16:49, 50) Uchaguzi wa Loti ulikuwa mbaya kwa upande wa kiroho japo huenda ukaonekana kuwa wa hekima kwa kuzingatia vitu vya kimwili. Kwa nini? Kwa sababu “watu wa Sodoma walikuwa wabaya, wenye kufanya dhambi nyingi sana juu ya BWANA,” lasema andiko la Mwanzo 13:13. Uamuzi wa Loti wa kuhamia eneo hilo ungehuzunisha sana familia yake hatimaye.

13. Kielelezo cha Abramu chaweza kuwasaidiaje Wakristo ambao huenda wakawa na ugomvi wa kifedha?

13 Lakini Abramu alionyesha imani katika ahadi ya Yehova kwamba hatimaye mbegu yake ingemiliki nchi hiyo yote; hakugombania sehemu ndogo tu ya nchi hiyo. Kwa ukarimu, yeye alitenda kupatana na kanuni ambayo baadaye ilitajwa kwenye 1 Wakorintho 10:24: “Acheni kila mmoja afulize kutafuta sana, si faida yake mwenyewe, bali ya mtu yule mwingine.” Hili ni kikumbusho kizuri kwa wale ambao huenda wakawa na ugomvi wa kifedha na waamini wenzao. Badala ya kufuata ushauri ulio kwenye Mathayo 18:15-17, wengine wamepeleka ndugu zao mahakamani. (1 Wakorintho 6:1, 7) Kielelezo cha Abramu chaonyesha kwamba ni afadhali kupata hasara kifedha badala ya kufanya jina la Yehova lishutumiwe au kuharibu amani ya kutaniko la Kikristo.—Yakobo 3:18.

14. Abramu angethawabishwaje kwa sababu ya ukarimu wake?

14 Abramu angethawabishwa kwa sababu ya ukarimu wake. Mungu alisema: “Na uzao wako nitaufanya uwe kama mavumbi ya nchi; hata mtu akiweza kuyahesabu mavumbi ya nchi, uzao wako utahesabika.” Ni lazima Abramu ambaye hakuwa na mtoto awe alitiwa moyo kama nini na kufunuliwa kwa jambo hilo! Halafu, Mungu akaamuru: “Ondoka, ukatembee katika nchi hii katika mapana yake, na marefu yake, maana nitakupa wewe nchi hiyo.” (Mwanzo 13:16, 17) La, Abramu hangeruhusiwa kukaa katika mazingira yenye starehe ya mji. Ilimpasa kujitenga na Wakanaani. Ni lazima Wakristo leo pia wajitenge na ulimwengu. Hawajioni kuwa bora kuliko wengine, lakini hawashirikiani kwa ukaribu na yeyote ambaye anaweza kuwashawishi washiriki katika mwenendo ulio kinyume cha Maandiko.—1 Petro 4:3, 4.

15. (a) Kuhamahama kwa Abramu kulikuwa na maana gani? (b) Abramu aliweka kielelezo gani kwa familia za Kikristo leo?

15 Katika nyakati za Biblia, mtu alikuwa na haki ya kukagua ardhi kabla ya kuimiliki. Hivyo, huenda ikawa kuhamahama kulimkumbusha Abramu daima kwamba siku moja nchi hiyo ingemilikiwa na uzao wake. Kwa utii, “Abramu akajongeza hema yake, akaja akakaa kwenye mialoni ya Mamre, nayo ni miti iliyoko Hebroni, akamjengea BWANA madhabahu huko.” (Mwanzo 13:18) Kwa mara nyingine, Abramu alidhihirisha kwamba aliiona ibada kuwa jambo muhimu sana. Je, familia yako huona funzo la familia, sala, na kuhudhuria mikutano kuwa mambo muhimu sana?

Adui Ashambulia

16. (a) Kwa nini maneno ya utangulizi ya Mwanzo 14:1 yanaonyesha kwamba jambo baya li karibu kutokea? (b) Kwa nini wafalme wanne wa mashariki walifanya uvamizi?

16 “Ikawa siku za Amrafeli mfalme wa Shinari, na Arioko mfalme wa Elasari, na Kedorlaoma mfalme wa Elamu * na Tidali mfalme wa Goimu, walifanya vita.” Katika Kiebrania cha awali, maneno hayo ya utangulizi (“Ikawa siku za . . .”) yanaonyesha kwamba jambo baya li karibu kutokea na yanaashiria “kipindi cha majaribu kinacholeta baraka.” (Mwanzo 14:1, 2, NW, kielezi-chini) Jaribu hilo lilianza wakati wafalme hawa wanne wa mashariki pamoja na majeshi yao walipofanya uvamizi wao wenye uharibifu huko Kanaani. Walikuwa na lengo gani? Walitaka kukomesha uasi wa miji mitano ya Sodoma, Gomora, Adma, Seboimu, na Bela. Waliishinda miji hiyo, “wakakutana panapo bonde la Sidimu, kwenye Bahari ya Chumvi.” Loti na familia yake waliishi hapo karibu.—Mwanzo 14:3-7.

17. Kwa nini kutekwa kwa Loti kulijaribu imani ya Abramu?

17 Wafalme wa Kanaani walizuia wavamizi hao kwa ujasiri, lakini wakashindwa vibaya sana. “Basi, wale walioshinda, wakateka mali yote ya Sodoma na Gomora, kadhalika na mazao yao, wakaenda zao. Walimteka hata Loti, mwana wa nduguye Abramu aliyekuwa anakaa Sodoma, pamoja na mali yake, wakaenda zao.” Muda si muda, habari za matukio hayo yenye kuhuzunisha zikamfikia Abramu: “Mtu mmoja aliyeponyoka, akaenda kumwarifu yule Mwebrania Abramu ambaye alikuwa anaishi karibu na mialoni ya Mwamori Mamre. Mamre alikuwa ndugu yake Eshkoli na Aneri. Wote walikuwa wamefanya agano na Abramu. [Hivyo Abramu akapata] habari kwamba mpwa wake amechukuliwa mateka.” (Mwanzo 14:8-14, BHN) Ni jaribu la imani lililoje! Je, Abramu angekuwa na chuki kuelekea mpwa wake kwa kuwa alichukua sehemu ya nchi iliyokuwa bora zaidi? Kumbuka pia kwamba wavamizi hawa walitoka Shina, nchi yake ya asili. Kupigana nao kungefanya isiwezekane kwake kurudi nyumbani. Isitoshe, je, Abramu angeweza kufanya chochote dhidi ya jeshi ambalo majeshi yote ya Kanaani hayakuweza kuyashinda?

18, 19. (a) Abramu aliwezaje kumwokoa Loti? (b) Ni nani aliyepata sifa kwa ushindi huo?

18 Kwa mara nyingine, Abramu alimtumaini Yehova kabisa. ‘Akawapa silaha vijana wake, waliozaliwa katika nyumba yake, watu mia tatu na kumi na wanane, akawafuata mpaka Dani. Akajipanga apigane nao usiku, yeye na watumwa wake, akawapiga, akawafukuza mpaka Hoba, ulioko upande wa kushoto wa Demeski. Naye akarudisha mali zote, akamrudisha na Loti nduguye na mali zake, na wanawake pia, na watu.’ (Mwanzo 14:14-16) Kwa kuonyesha imani yenye nguvu katika Yehova, Abramu alipata ushindi kwa jeshi lake lililokuwa dogo sana, akamwokoa Loti na familia yake. Wakati huo ndipo Abramu alipokutana na Melkizedeki, mfalme-kuhani wa Salemu. “Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana. Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi. Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote.”—Mwanzo 14:18-20.

19 Naam, Yehova ndiye aliyekuwa mshindi. Kwa mara nyingine tena, Abramu aliokolewa na Yehova kwa sababu ya imani yake. Watu wa Mungu leo hawashiriki katika vita halisi, lakini wao hukabili majaribu na magumu mengi. Makala yetu ifuatayo itaonyesha jinsi kielelezo cha Abramu kiwezavyo kutusaidia kukabiliana na magumu hayo kwa mafanikio.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Kulingana na kichapo Insight on the Scriptures (kilichochapishwa na Mashahidi wa Yehova), “funjo moja la kale laeleza kuhusu Farao mmoja aliyeagiza wanaume wenye silaha wamchukue mwanamke mrembo na kumwua mume wake.” Kwa hiyo hofu ya Abramu ilikuwa na msingi mzuri.

^ fu. 6 Huenda ikawa Hagari, ambaye baadaye alikuwa suria wa Abramu, alikuwa mmojawapo wa watumishi ambao Abramu alipewa wakati huo.—Mwanzo 16:1.

^ fu. 16 Wakati mmoja wachambuzi walidai kwamba Elamu haukuwa na uvutano kama huo huko Shina na kwamba simulizi kuhusu shambulizi la Kedorlaoma ni la uwongo. Ili kupata habari zaidi juu ya uthibitisho wa akiolojia unaounga mkono simulizi hilo la Biblia, ona gazeti Mnara wa Mlinzi la Julai 1, 1989, ukurasa wa 4-7.

Je, Umefahamu?

• Njaa iliyokuwa Kanaani ilijaribuje imani ya Abramu?

• Abramu na Sarai waliwawekeaje kielelezo kizuri waume na wake leo?

• Tunaweza kujifunza nini kutokana na jinsi ambavyo Abramu alisuluhisha ugomvi kati ya watumishi wake na wale wa Loti?

[Maswali ya Funzo]

[Picha katika ukurasa wa 22]

Abramu alitanguliza masilahi ya Loti badala ya kudai haki zake

[Picha katika ukurasa wa 24]

Abramu alimtegemea Yehova ili kumwokoa mpwa wake Loti