Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tembea Katika ‘Njia ya Unyofu’

Tembea Katika ‘Njia ya Unyofu’

Tembea Katika ‘Njia ya Unyofu’

‘WENYE haki watakuwa heri kwa maana watakula matunda ya matendo yao,’ akasema nabii Isaya. Pia Isaya alisema hivi: “Njia yake mwenye haki [“mwadilifu,” NW] ni unyofu.” (Isaya 3:10; 26:7) Bila shaka, ili tutokeze matunda mema, lazima tutende kwa uadilifu machoni pa Mungu.

Hata hivyo, tunawezaje kutembea katika njia ya unyofu? Tunaweza kutarajia baraka gani kwa kufanya hivyo? Na wengine wanaweza kunufaikaje tunapoishi kupatana na viwango vya uadilifu vya Mungu? Katika sura ya 10 ya kitabu cha Biblia cha Mithali, Mfalme Solomoni wa Israeli la kale atoa majibu ya maswali hayo anapoonyesha tofauti iliyopo kati ya mtu mwadilifu na mwovu. Anaonyesha tofauti hiyo kwa kutumia usemi “mwenye haki” [“mwadilifu,” NW] mara 13. Usemi huo umetumiwa mara tisa katika mstari wa 15 hadi 32. Kwa hiyo basi, ni jambo lenye kutia moyo kuchunguza Mithali 10:15-32. *

Kubali Nidhamu

Solomoni ataja umuhimu wa uadilifu. Asema: “Mali ya mtu tajiri ni mji wake wa nguvu; uangamivu wa maskini ni umaskini wao. Kazi yake mwenye haki [mwadilifu, NW] huuelekea uzima; mazao ya wabaya huuelekea dhambi.”Mithali 10:15, 16.

Kama vile mji uliozingirwa kwa ukuta huandaa usalama wa kiasi fulani kwa watu wanaoishi humo, ndivyo mali inavyoweza kuwa ulinzi dhidi ya mambo fulani maishani yanayoweza kutokea pasipo kutarajiwa. Na umaskini unaweza kutokeza madhara, mambo fulani yasiyotarajiwa yanapotokea. (Mhubiri 7:12) Hata hivyo, yaelekea mfalme huyo mwenye hekima alikuwa anadokeza hatari fulani inayoweza kusababishwa na utajiri na vilevile umaskini. Huenda tajiri akawa na mwelekeo wa kutumaini sana mali zake, akifikiri kwamba vitu vyake vyenye thamani ni “kama ukuta mrefu.” (Mithali 18:11) Na huenda maskini akadhani kimakosa kwamba umaskini humkosesha tumaini la wakati ujao. Hivyo, wote wawili wanakosa kujifanyia jina zuri pamoja na Mungu.

Kwa upande mwingine, matendo ya mtu mwadilifu awe ana mali au la, humwongoza kwenye uhai. Jinsi gani? Anaridhika na vitu alivyo navyo. Yeye haruhusu hali yake ya kifedha iharibu msimamo wake mzuri pamoja na Mungu. Mwenendo wa mtu mwadilifu awe ni tajiri au maskini, humletea furaha sasa na tumaini la uhai udumuo milele wakati ujao. (Ayubu 42:10-13) Mwovu hanufaiki hata akipata mali. Badala ya kushukuru kwa sababu ya ulinzi unaoletwa na mali na kuishi kupatana na mapenzi ya Mungu, yeye hutumia mali zake kuishi maisha ya dhambi.

“Akubaliye kurudiwa [“nidhamu,” “NW”] huwa katika njia ya uzima;” aendelea kusema mfalme wa Israeli, “bali yeye aachaye maonyo hukosa.” (Mithali 10:17) Msomi fulani wa Biblia adokeza kwamba mstari huo unaweza kueleweka kwa njia mbili. Maana moja yaweza kuwa mtu anayekubali nidhamu na kufuatia uadilifu yuko katika njia ya uzima, ilhali mtu anayekataa maonyo huacha njia hiyo. Mstari huo ungeweza pia kumaanisha kwamba “yeye anayekubali nidhamu huonyesha wengine njia ya uzima [kwa sababu kielelezo chake kizuri huwanufaisha wengine], lakini yeyote anayepuuza maonyo hupotosha wengine.” (Mithali 10:17, New International Version) Hata mstari huo uwe unamaanisha nini, ni muhimu kama nini kwamba tukubali nidhamu na tusikatae maonyo!

Sitawisha Upendo Badala ya Chuki

Kisha Solomoni atoa mithali yenye sehemu mbili zenye wazo moja, sehemu ya pili inakazia sehemu ya kwanza. Asema: “Yeye afichaye chuki ana midomo ya uongo.” Ikiwa mtu fulani anamchukia mwingine kisha anaficha chuki hiyo kwa kumvisha kilemba cha ukoka, yeye ni mdanganyifu—ana “midomo ya uongo.” Mfalme mwenye hekima aongezea kusema hivi: “Yeye asingiziaye ni mpumbavu.” (Mithali 10:18) Badala ya kuficha chuki yao, watu fulani hutokeza mashtaka bandia au hueneza uvumi unaoharibu jina la mtu wanayemchukia. Hilo ni jambo la upumbavu kwa sababu habari hizo za uchongezi haziwezi kumbadili mtu huyo. Msikilizaji mwenye busara atatambua kwamba habari hizo zilikusudiwa kumdhuru mtu mwingine, naye hatamstahi mchongezi huyo. Kwa hiyo mtu anayeeneza habari mbaya anajidhuru mwenyewe.

Mwenendo wa uadilifu ungekuwa kujiepusha na uwongo au uchongezi. Mungu aliwaambia Waisraeli hivi: “Usimchukie ndugu yako moyoni mwako.” (Mambo ya Walawi 19:17) Naye Yesu aliwashauri hivi wasikilizaji wake: “Endeleeni kupenda [hata] maadui wenu na kusali kwa ajili ya wale wanaowanyanyasa nyinyi; ili mpate kujithibitisha wenyewe kuwa wana wa Baba yenu aliye katika mbingu.” (Mathayo 5:44, 45) Ni jambo bora kama nini kusitawisha upendo mwingi sana mioyoni mwetu badala ya chuki!

‘Zuia Midomo Yako’

Akikazia uhitaji wa kudhibiti ulimi, mfalme mwenye hekima asema: “Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu; bali yeye azuiaye midomo yake hufanya akili.”Mithali 10:19.

“Mpumbavu hububujika maneno.” (Mhubiri 10:14, BHN) Kinywa chake “humwaga upumbavu.” (Mithali 15:2) Hiyo haimaanishi kwamba kila mtu ambaye huongea sana ni mpumbavu. Lakini ni rahisi kama nini mtu anayeongea sana kuanzisha na kueneza porojo au uvumi wenye kudhuru! Kuongea kipumbavu kwaweza kuharibu jina la mtu, kuumiza hisia za wengine, kusababisha uhasama, na hata kuwadhuru wengine. “Katika wingi wa maneno hapakosi kuwa na maovu.” (Mithali 10:19) Isitoshe, inaudhi kuwa karibu na mtu ambaye anajua kila kitu. Na tusiwe na maneno mengi.

Mbali na kuepuka uwongo, mtu anayezuia midomo yake hutenda kwa busara. Yeye hufikiri kabla ya kunena. Kwa kuchochewa na upendo kwa viwango vya Yehova na kutaka kumsaidia kikweli mwanadamu mwenzake, yeye hufikiri jinsi maneno yake yatakavyowaathiri wengine. Maneno yake ni yenye upendo na fadhili. Yeye hutafakari jinsi anavyoweza kusema maneno yafaayo na yenye kupendeza. Maneno yake ni kama “machungwa katika vyano vya fedha”—nyakati zote yanasemwa kwa kufikiriwa na kwa heshima.—Mithali 25:11.

“Hulisha Watu Wengi”

“Ulimi wa mwenye haki [“mwadilifu,” “NW”] ni kama fedha teule,” Solomoni aendelea kusema, “moyo wa mtu mbaya haufai kitu.” (Mithali 10:20) Maneno ya mwadilifu ni safi—kama fedha teule, isiyo na taka. Bila shaka, ndivyo ilivyo kwa watumishi wa Yehova wanapowaeleza wengine ujuzi wa Neno la Mungu unaookoa uhai. Mfunzi wao Mtukufu, Yehova Mungu, amewaelimisha na ‘amewapa ulimi wa wafundishwao, wapate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka.’ (Isaya 30:20; 50:4) Kwa kweli, ulimi wao ni kama fedha teule unapozungumza kweli ya Biblia. Maneno yao ni yenye thamani kubwa kama nini kwa watu wenye mioyo minyofu, tofauti na makusudi ya waovu! Acheni tuwe na hamu ya kuzungumza kuhusu Ufalme wa Mungu na kazi za ajabu za Mungu.

Mtu mwadilifu huwanufaisha watu walio karibu naye. “Midomo ya mwenye haki [“mwadilifu,” “NW”] hulisha watu wengi,” Solomoni aendelea kusema, “bali wapumbavu hufa kwa kuwa hawana ufahamu.”Mithali 10:21.

‘Mwadilifu hulishaje watu wengi’? Neno la Kiebrania linalotumiwa hapa linadokeza wazo la “uchungaji.” (Mithali 10:21, kielezi-chini, NW) Neno hilo linadokeza wazo la kuongoza na vilevile kulisha, kama vile mchungaji wa nyakati za kale alivyotunza kondoo zake. (1 Samweli 16:11; Zaburi 23:1-3; Wimbo Ulio Bora 1:7) Mtu mwadilifu huongoza au huelekeza wengine kwenye njia ya uadilifu, maneno yake hunufaisha wasikilizaji. Matokeo ni kwamba, wanaishi maisha yenye furaha na yenye kuridhisha zaidi, na huenda wakapokea uhai udumuo milele.

Lakini, namna gani mpumbavu? Kwa kutokuwa na ufahamu, hana nia njema au hajali matokeo ya mwenendo wake. Mtu kama huyo hufanya lolote atakalo, pasipo kujali matokeo yatakuwaje. Kwa hiyo, anapata madhara kwa sababu ya matendo yake. Mtu mwadilifu husaidia kuokoa wengine, lakini mtu asiye na ufahamu hawezi hata kujiokoa mwenyewe.

Epuka Mwenendo Mlegevu

Mara nyingi utu wa mtu hujulikana kwa kutegemea mambo anayopenda na asiyopenda. Akizungumzia habari hiyo, mfalme wa Israeli asema: “Kwa mpumbavu kutenda maovu [“kuwa na mwenendo mlegevu,” “NW”] ni kama mchezo; bali mtu mwenye ufahamu ana hekima.”Mithali 10:23.

Watu fulani huona mwenendo mlegevu kama mchezo na kujihusisha nao ili kujifurahisha tu. Watu kama hao humpuuza Mungu kuwa mtu ambaye atawatoza watu wote hesabu, na wanakataa kutambua mwenendo wao mbaya. (Waroma 14:12) Mawazo yao yamepotoka kiasi cha kwamba wanadhani Mungu haoni makosa yao. Kwa kweli, kupitia mwenendo wao, wanasema: “Hakuna Mungu.” (Zaburi 14:1-3; Isaya 29:15, 16) Ni jambo la upumbavu kama nini!

Kwa upande mwingine, mtu mwenye ufahamu anajua kwamba mwenendo mlegevu si mchezo. Anajua kwamba Mungu huchukizwa na mwenendo mlegevu na unaweza kuharibu uhusiano wa mtu pamoja naye. Mwenendo wa namna hiyo ni wa kipumbavu kwa sababu unafanya watu wakose kujistahi, unaharibu ndoa, unadhuru akili na mwili, na kufanya watu wasithamini mambo ya kiroho. Tunakuwa watu wenye hekima tunapoepuka mwenendo mlegevu na kupendezwa na hekima kama vile tunavyopendezwa na dada mpendwa.—Mithali 7:4.

Jenga Juu ya Msingi Unaofaa

Akizungumzia umuhimu wa kujenga maisha juu ya msingi unaofaa, Solomoni asema: “Aogopacho mtu asiye haki ndicho kitakachomjilia; na wenye haki [“waadilifu,” “NW”] watapewa matakwa yao. Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena; bali mwenye haki [“mwadilifu,” “NW”] ni msingi wa milele.”Mithali 10:24, 25.

Mwovu anaweza kuwaogopesha sana wengine. Hata hivyo, hatimaye jambo ambalo anaogopa humpata. Kwa kuwa haishi kulingana na kanuni za uadilifu, yeye ni kama jengo lisilo imara ambalo huporomoka wakati wa dhoruba kali. Yeye hushindwa kukinza msongo. Kwa upande mwingine, mtu mwadilifu ni sawa na yule mtu anayetenda kupatana na maneno ya Yesu. Yeye ni “mtu mwenye busara, aliyejenga nyumba yake juu ya tungamo-mwamba.” Yesu akasema, “na mvua ikamwagika na mafuriko yakaja na pepo zikavuma na kudunda dhidi ya nyumba hiyo, lakini haikuporomoka, kwa maana ilikuwa imepigwa msingi juu ya tungamo-mwamba.” (Mathayo 7:24, 25) Mtu huyo ni thabiti—mawazo na matendo yake yana msingi thabiti katika kanuni za Mungu.

Kabla ya kuendelea kuonyesha tofauti kati ya mwovu na mwadilifu, mfalme mwenye hekima atoa onyo lililo wazi lakini fupi. Asema: “Kama siki menoni, na kama moshi machoni, ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao.” (Mithali 10:26) Siki humfanya mtu ahisi vibaya kwenye meno. Asidi ya asetiki iliyo katika siki hutokeza ladha yenye gwadu mdomoni na inaweza kufanya meno yawe na ganzi. Moshi hufanya macho yawashe. Vivyo hivyo, yeyote anayeajiri mvivu au kumtumia kuwa mwakilishi wake yaelekea atakasirika na kupata hasara.

Njia ya Bwana Ni Kimbilio”

Mfalme wa Israeli aendelea kusema: “Kumcha BWANA kwaongeza siku za mtu; bali miaka ya wasio haki itapunguzwa. Matumaini yao wenye haki [“waadilifu,” “NW”] yatakuwa furaha; bali kutaraji kwao wasio haki kutapotea.”Mithali 10:27, 28.

Mtu mwadilifu huongozwa na hofu ya kimungu naye hujaribu kumpendeza Yehova kwa mawazo, maneno, na matendo yake. Mungu humjali na humtimizia matarajio yake ya uadilifu. Hata hivyo, mwovu huishi bila kumhofu Mungu. Nyakati nyingine huenda matumaini yake yakaonekana kuwa yametimizwa kwa muda mfupi tu, kwa kuwa mara nyingi yeye hufa kwa sababu ya jeuri au ugonjwa unaosababishwa na mtindo wake wa maisha. Matumaini yake yote huisha siku anapokufa.—Mithali 11:7.

“Njia ya BWANA ni kimbilio lake mtu mkamilifu,” asema Solomoni, “bali ni uharibifu kwao watendao maovu.” (Mithali 10:29) Njia ya Yehova inayotajwa hapa, hairejezei njia ya maisha tunayopaswa kufuata, bali njia ya Mungu ya kushughulika na wanadamu. “Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; maana, njia zake zote ni haki,” akasema Musa. (Kumbukumbu la Torati 32:4) Njia za Mungu za haki humaanisha usalama kwa waadilifu na uharibifu kwa waovu.

Yehova ni kimbilio lililoje kwa watu wake! “Mwenye haki [“mwadilifu,” “NW”] hataondolewa milele; bali wasio haki hawatakaa katika nchi. Kinywa cha mwenye haki [“mwadilifu,” “NW”] hutoa hekima; bali ulimi wa ukaidi utakatiliwa mbali. Midomo ya mwenye haki [“mwadilifu,” “NW”] huyajua yatakayokubaliwa; bali kinywa chao wasio haki hunena ukaidi.”Mithali 10:30-32.

Bila shaka waadilifu hufanikiwa nao hubarikiwa kwa sababu ya kutembea katika njia ya unyofu. Kwa kweli, “baraka ya BWANA hutajirisha, wala hachanganyi huzuni nayo.” (Mithali 10:22) Acheni sikuzote tutende kwa uangalifu kupatana na kanuni za Mungu. Acheni pia tuzuie midomo yetu na kutumia ulimi wetu kulisha wengine kweli zenye kuokoa uhai za Neno la Mungu na kuwaongoza kwenye njia ya uadilifu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 3 Kwa habari kamili kuhusu Mithali 10:1-14, ona gazeti Mnara wa Mlinzi la Julai 15, 2001, ukurasa wa 24-27.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Ulimi unaweza kuwa kama “fedha teule”