Wanaoharibu Miti
Wanaoharibu Miti
MITI ilionwa kuwa bidhaa yenye thamani nyakati za Biblia. Kwa mfano, miti iliorodheshwa kwenye mkataba wa ununuzi wakati Abrahamu aliponunua sehemu ya kumzika Sara, mkewe mpendwa.—Mwanzo 23:15-18.
Vivyo hivyo leo, miti inathaminiwa sana, na uhifadhi wa misitu unatiliwa maanani sana ulimwenguni kote. Kitabu State of the World 1998, chasema: “Ingawa watu wengi katika sehemu za kaskazini mwa dunia zenye halijoto ya wastani wana wasiwasi kuhusu misitu ya nchi za tropiki, huenda hawajui kwamba misitu ya nchi zao ndiyo yenye kutawanyika na yenye kuathirika zaidi.” Ni nini kinachotisha misitu katika nchi hizo za kaskazini mwa Ulaya na Amerika Kaskazini? Wengi husema tisho hilo linatokana na ukataji wa miti, lakini kuna mambo mengine yanayoharibu misitu polepole. Ni mambo gani hayo? Uchafuzi wa hewa na mvua ya asidi. Uchafuzi huo unaweza kudhoofisha miti polepole, na kuifanya iwe rahisi kuharibiwa na wadudu na magonjwa.
Kwa miaka mingi, wanamazingira na watu wengine wanaojali misitu wametoa tahadhari juu ya uhitaji wa kulinda mazingira. Katika miaka ya 1980, wanasayansi huko Ujerumani walifikia mkataa huu baada ya kuchunguza jinsi uchafuzi wa hewa na mvua ya asidi zinavyoathiri mazingira: ‘Iwapo hatua haitachukuliwa, kufikia mwaka wa 2000, watu watafurahia kuona misitu kwenye picha za zamani na sinema tu.’ Jambo linalofurahisha ni kwamba uwezo wa dunia wa kujifanya upya ni mkubwa kiasi kwamba kufikia sasa dunia haijaathirika sana kama ilivyokuwa imetabiriwa.
Hata hivyo, mwishowe, Mungu ndiye atakayefanya mengi zaidi kudumisha mazingira. “Huinywesha milima toka orofa zake” na “huyameesha majani kwa makundi, na maboga kwa matumizi ya mwanadamu.” Naye ameahidi “kuwaleta kwenye uangamizi wale wanaoiangamiza dunia.” (Zaburi 104:13, 14; Ufunuo 11:18) Itakuwa vizuri kama nini wakati ambapo wakazi wa dunia wataweza kufurahia ulimwengu usio na uchafuzi milele!—Zaburi 37:9-11.