Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Matatizo ya Ubaguzi wa Kijamii

Matatizo ya Ubaguzi wa Kijamii

Matatizo ya Ubaguzi wa Kijamii

“USAWA UNAWEZA KUWA JAMBO LINALOFAA, LAKINI HAKUNA SERIKALI YOYOTE DUNIANI INAYOWEZA KUFANYA WATU WOTE WAWE NA USAWA.”

Hivyo ndivyo alivyosema Honoré de Balzac, mwandishi wa vitabu Mfaransa wa karne ya 19. Je, unakubaliana naye? Kwa kawaida, watu wengi huona ubaguzi wa kijamii kuwa haufai. Lakini, hata katika karne hii ya 21, jamii ya kibinadamu bado imegawanyika katika vikundi mbalimbali.

CALVIN COOLIDGE, aliyekuwa rais wa Marekani tangu 1923 hadi 1929, alihangaikia tatizo la ubaguzi wa kijamii na alisema juu ya “kutokomea kabisa kwa jamii za cheo cha juu.” Hata hivyo, miaka 40 hivi baada ya Coolidge kuondoka madarakani, Tume ya Uchunguzi ya Kerner, iliyoteuliwa kuchunguza uhusiano wa kijamii, ilikuwa na wasiwasi kwamba Marekani kwa hakika ingegawanyika katika jamii mbili: “jamii za weusi na weupe—zilizotengana na zisizo na usawa.” Wengine hudai kwamba utabiri huo tayari umetimia na kwamba “tofauti za kiuchumi na za kijamii zinazidi kuongezeka” nchini humo.

Kwa nini ni vigumu kufanya watu wote wawe na usawa? Sababu kuu ni jinsi mwanadamu alivyo. Mbunge mmoja wa zamani wa Marekani, William Randolph Hearst, alisema hivi wakati mmoja: “Watu wote wameumbwa wakiwa na usawa katika angalau jambo moja, nalo ni tamaa yao ya kutokuwa na usawa.” Alimaanisha nini? Labda Henry Becque, mwandishi wa drama Mfaransa wa karne ya 19, alifafanua jambo hilo waziwazi zaidi aliposema: “Kinachofanya usawa uwe jambo gumu hivyo ni kwamba tunataka tu kuwa sawa na wakubwa wetu.” Yaani, watu wanataka kuwa sawa na wale walio na vyeo vya juu katika jamii; lakini si wengi ambao wangetaka kupunguza mapendeleo na hali zao bora ili wawe sawa na watu wa hali ya chini.

Zamani, watu walizaliwa katika cheo cha chini, cha juu, au hata katika familia za kifalme. Hali hiyo bado iko hivyo katika maeneo machache. Hata hivyo, katika nchi nyingi leo, pesa—au ukosefu wa pesa—ndio huamua kama mtu ni wa cheo cha chini, cha kati, au cha juu. Hata hivyo, kuna mambo mengine yanayoonyesha mtu ana cheo gani katika jamii, kama vile asili ya mtu, elimu, na kujua kusoma na kuandika. Na katika maeneo mengine, tofauti ya kijinsia ni sababu kubwa ya kubaguliwa, huku wanawake wakionwa kuwa watu wa cheo cha chini.

Je, Kuna Matumaini Yoyote?

Sheria kuhusu haki za kibinadamu zimesaidia kumaliza ubaguzi fulani wa kijamii. Sheria za kutobagua watu zilipitishwa huko Marekani. Na huko Afrika Kusini, Sera ya Ubaguzi wa Rangi ikapigwa marufuku. Utumwa umepigwa marufuku katika nchi nyingi ulimwenguni ingawa bado unaendelea katika sehemu fulani. Maamuzi fulani ya mahakamani yamefanya haki za wenyeji za kumiliki ardhi zitambuliwe, nazo sheria zinazopinga ubaguzi zimesaidia sana jamii ambazo hali zao ni ngumu.

Je, hatua hizo zinaonyesha kwamba ubaguzi wa kijamii utaisha? La. Ingawa ubaguzi fulani wa kijamii unaweza kupunguzwa sasa, mitengano mipya imeanza kutokea. Kitabu Class Warfare in the Information Age chasema: “Inaonekana kwamba leo haifai tena kutenganisha watu katika jamii ya matajiri na wafanya-kazi, kwa sababu jamii hizo kubwa mbili zimegawanyika kuwa vikundi vingi vidogo-vidogo vya watu wenye hasira.”

Je, ubaguzi wa kijamii utaendelea kugawanya watu milele? Kama makala ifuatayo itakavyoonyesha, kuna matumaini kwamba hali haitakuwa hivyo milele.